Serikali yaahidi kuikarabati Sekondari ya
Wasichana Iringa
Na Atley
Kuni OR TAMISEMI
Waziri wa
Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo ameahidi kuwa shule ya
sekondari ya Wasichana Iringa iliyopo mkoani Iringa itafanyiwa ukarabati ikiwa
ni muendelezo wa serikali katika kuzikarabati shule zake kongwe hapa nchini.
Waziri
Jafo alitoa kauli hiyo jana wakati akiwa njiani kurudi Dodoma akitokea mkoani
Iringa ambapo pamoja na kuhudhuria sherehe za Mei Mosi alihudhuria pia ufunguzi
wa hospitali ya Wilaya ya Kilolo.
Ilimlazimu
Waziri Jafo kufanya ziara ya kushtukiza shuleni hapo, ili aweze kujionea
miundombinu mbalimbali katika shule hiyo iliyo anzishwa toka mwaka 1967.
Akizungumza
na walimu, watumishi wasio walimu pamoja na wanafunzi wa shule hiyo mara baada
ya kujionea hali ya miundombinu ya shule hiyo, Mhe. Jafo alieleza kuwa shule
hiyo ni miongoni mwa shule kongwe zilizo kwenye mpango wa ukarabati mkubwa ili
kuwa na mazingira bora ya kusoma na kujifunzia.
“Katika mwaka wa fedha wa 2017/18 tulikarabati shule kongwe
43 na katika mwaka huu wa 2018/19, shule hii pamoja na zingine kongwe 45 hapa
nchini zitakuwa katika mpango kamambe wa kukarabatiwa kama tulivyokwisha fanya
kwenye shule kama 43 za awali ambapo shule 89 zote kongwe tuwe tumezimaliza”
alisema Waziri Jafo.
Aliongeza
kuwa shule ya Wasichana Iringa imekuwa ni moja ya shule bora na hivyo kufanya
wanafunzi wengi kupenda kuhamia kwenye shule hiyo.
Sambamba
na ukarabati huo Mhe. Jafo ameahidi kuzifanyia kazi changamoto zote ambazo
ziliainishwa mbele yake ikiwepo upungufu wa walimu wa Fizikia na Hisabati
pamoja na stahiki za walimu.
“Mama yetu
Nkondola amewasilisha changamoto za walimu wa Hesabu na Fizikia lakini pia
maslahi ya walimu, naomba nieleze kuwa suala hilo nimelichukua lakini niwaahidi
kutuma wataalam kutoka kwenye wizara yangu pamoja na wizara nyingine za kisekta
kuja kufanya tathmini ya kina juu ya haya mliyoniambia,” alisema waziri Jafo.
Aliwataka
wanafunzi hao kusoma kwa bidii huku akitoa ahadi kwa jumuiya hiyo
kuwa endapo katika mitihani yao ya mwisho ya kidato cha sita watapata daraja la
kwanza (DV.1) zaidi wanafunzi ya 30 atawandalia sherehe ndogo ya kujipongeza na
wale watakaopata daraja la kwanza kati ya pointi 3-5 wataalikwa bungeni kwa
gharama zake yeye Mhe.Jafo.
Mhe. Jafo
akiwa katika ziara hiyo, alikagua miundombinu ya shule ikiwapo Mabweni, Vyoo,
Bwalo la Chakula, Jiko na Ofisi za Walimu na kisha kufanya mazungumzo na
walimu, watumishi wasio walimu wanafunzi sambamba na wananchi wanaozunguka eneo
la shule hiyo.
Huo
umekuwa ni utamaduni wa kiongozi huyo mwenye dhamana na OR TAMISEMI kila
anapopata fursa kutembelea mikoani kutembelea shughuli za maendeleo kwa
wananchi na sekta zote ili kujionea maendeleo ya watu na shughuli zao.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.