ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, February 3, 2018

SHERIA MPYA YA MADINI YA MWAKA 2017 INATAKA KURUDISHA UCHUMI KWA WANANCHI: MHE BITEKO


Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akizungumza na Uongozi wa Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga ambapo amesisitiza viongozi kusimamia Kanuni na taratibu juu ya usimamizi wa madini, leo 3 Februari 2018. Picha Zote Na Mathias Canal
Kamati ya ulinzi na usalama Wilaya ya Kahama ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe Fadhil Nkulu wakisikiliza maelekezo mbalimbali kutoka kwa Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko alipozuru Wilayani humo kwa ziara ya kikazi, Leo Februari 2018.
Mgeni Rasmi-Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akizungumza wakati wa kikao cha kazi na Uongozi wa Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga aakiwa katika ziara ya kikazi, leo 3 Februari 2018.

Na Mathias Canal, Shinyanga

"Sheria mpya ya madini ya mwaka 2017 inataka kurudisha uchumi wa madini kuwa uchumi fungamanishi kwa sekta nyingine, Hatuwezi kuwa na Mgodi ndani ya nchi ambao ajira zote zinapelekwa nje ya nchi kupitia huduma mbalimbali, unaweza kuagiza bidhaa za kila aina kutoka nje ya nchi lakini huwezi kuagiza ajira za wananchi wako zitoke nje kuja ndani, kamwe haiwezekani" 

Ni Kauli ya Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko leo 3 Februari 2018 wakati akizungumza na Uongozi wa Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga ambapo amesisitiza zaidi viongozi wa serikali katika maeneo yao kusimamia Kanuni na taratibu juu ya usimamizi wa madini.

Mhe Biteko alikaririwa akisema kuwa usimamizi madhubuti wa sheria na taratibu zilizowekwa ni sehemu imara na makini itakayowanufaisha watanzania ambapo watakuwa wamemuunga mkono kwa vitendo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli ambaye amejidhatiti kwa mtazamo wa kuwanufaisha watanzania kupitia rasilimali zao.

Kanuni ya madini ya mwaka 2018 imeelekeza kuwa mgodi wowote unapoanza asilimia 100% za watoa huduma za chakula wanapaswa kuwa watu wa wananchi wa Tanzania, Pia huduma za ulinzi kwa asilimia 100% zinapaswa kutolewa na kampuni za ndani. Hivyo wataalamu wa sekta ya madini ni lazima kusimamia Kanuni hizo kwa usahihi.

Mhe Biteko aliongeza kuwa kampuni ya kigeni inaweza kufanya huduma hizo lakini ni lazima iingie ubia na wananchi wa Tanzania na kanuni hizi serikali imeziweka kwa makusudi kabisa ikiwa na mtazamo wa kuwanufaisha wananchi kupitia rasilimali zao.

Mhe Biteko alisema kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndicho kimeingia mkataba na wananchi katika kuwatumikia kwa usimamizi madhubuti kupitia ilani ya uchaguzi ya mwaka 2015-2020 hivyo viongozi wa CCM wanapaswa kusimamia vyema serikali ili kuongeza tija katika utendaji.

Sambamba na CCM kusimamia vyema serikali pia Naibu Waziri huyo wa Madini amewataka watendaji wote wa serikali kuwa na umoja katika utendaji wao kwa usimamizi madhubuti wa rasilimali madini huku akitoa onyo Kali kwa watendaji wa serikali, Viongozi, vyama vya siasa na wananchi kujihusisha na rushwa kwani kufanya hivyo ni kuzififisha juhudi za serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Magufuli ya kuwainua wananchi wanyonge ili kila mtanzania aweze kunufaika na rasilimali zilizopo.

"Ndugu zangu ni aibu mno dhahabu na madini yetu mengine kuchimbwa nchini lakini yanajenga nchi nyingine, Uhakika wa barabara bado hatuna katika maeneo mengi, maji bado hatuna, sekta ya afya haijaimarika, Zahanati zina shida lakini pia Karibu kila maeneo hatujajidhatiti kwa asilimia 100% Kwa hiyo Mhe Dc naomba sana msicheke na mtu yeyote anayecheza na rasilimali zetu This Must be a Serious business, Mimi najua we have the same spirit lazima tufanye kazi kwa weledi.

Aidha, Naibu Waziri huyo wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe Fadhil Nkulu sambamba na Mbunge wa Jimbo la Msalala Mhe Ezekiel Maige kwa jukumu kubwa la utendaji wao katika kuimarisha juhudi na ufanyaji kazi uliotukuka katika sekta ya madini kwa maslahi ya wananchi na Taifa kwa ujumla huku akisisitiza kuwa kila kiongozi atapimwa kwa matokeo ya utendaji kazi wake na si kwa cheo chake.

" Waheshimiwa Viongozi, Mhe. Rais na wanatanzania watatupima kwa matokeo si kwa nafasi na vyeo vyetu" alisisitiza Mheshimiwa Biteko wakati akihitimisha hotuba yake kwa uongozi wa serikali wilayani Kahama.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.