Takwimu iliyotolewa na serikali ya India ni ya kushtua baada ya kuonyesha kwamba, ndani ya kila saa moja mwanafunzi mmoja hujiua nchini humo.
Gazeti la Times of India limeandika kuwa, idadi ya vijana wanaojiua imezidi kuongezeka kiasi cha kuwafanya viongozi wa serikali ya nchi hiyo kuanza kuzitahadharisha familia. Kwa mujibu wa takwimu za mwisho zilizotolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya India kuhusiana na suala hilo, sababu ya vijana wengi kujiua ni utumiaji wa madawa ya kulevya, matatizo ya kisaikolojia yanayosababishwa na kuachana wazazi wawili, kugombana na watu wakubwa, masuala nyeti na matatizo yanayohusiana na masomo.
Aidha ripoti hiyo imeeleza kuwa, idadi ya wanafunzi waliojiua mwaka 2016 pekee ilikaribia 9500 ambapo inaonyesha kwamba, karibu kila saa moja, hujiua mwanafunzi mmoja. Kadhalika ripoti hiyo, imeyataja majimbo ya Maharashtra na Bengal kuwa yanayoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaojiua. Weledi wa mambo nchini humo wanaamini kwamba, mabadiliko ya haraka katika jamii ya India yamekuwa na taathira hasi kwa vijana wa nchi hiyo ambapo kutokana na kutokuwa na uwezo wa kufanya mawasiliano chanya na watu wa familia na marafiki zao, huamua kujiua.
Hii ni katika hali ambayo India pia inaongoza kwa kuwa na kiwango cha juu cha vijana wanaojiua duniani. Weledi wa mambo wanaamini kwamba kabla ya serikali kutatua tatizo la kisaikolojia kwa vijana, inatakiwa kwanza kushughulikia hali ya uchumi na kutatua matatizo ya kijamii nchini humo.
KWA HISANI YA http://parstoday.com/sw/news/world
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.