ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, September 25, 2017

DC HANDENI, GONDWIN GONDWE AKABIDHI ARDHI YENYE HEKARI 282 KWA UZALENDO KWANZA


UZALENDO KWANZA wakiongozwa na mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Godwin Gondwe wakielekea katika kijiji cha Kitumbi wilaya ya Handeni mkoa wa Tanga, ambapo walipatiwa Mashamba yenye ukubwa wa hekari 282 za ardhi kwa ajili ya uwekezaji wa Kilimo. Picha zote na Kajunason/MMG-Handeni.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Godwin Godwe akiongea mara baada ya kuwakabidhi ardhi yenye ukubwa wa hekari 282 katika kijiji cha kitumbi kwa wasanii na wadau wengine wanaofanya kampeni ya UZALENDO KWANZA. Tukio hilo lilifanyika kijijini Kitumbi, Muheza - Tanga mwishoni mwa wiki iliyopita.
Mwenyekiti wa UZALENDO KWANZA, Msanii Steve Nyerere akitoa shukrani zake za pekee kwa mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Godwin Gondwe mara baada ya kuwakaribisha wana- UZALENDO KWANZA na kuwapatia hekari 282 za ardhi kwa ajili ya uwekezaji wa kilimo katika kijiji cha Kitumbi wilaya ya Handeni mkoa wa Tanga.
Diwani wa Kata ya Kitumbi, Charles Abeid akiwakaribisha wasanii na wadau wengine wanaofanya kampeni ya UZALENDO KWANZA.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Godwin Gondwe akiwatambulisha viongozi wa kijiji cha Kitumbi, Handeni -Tanga.
Eneo ambalo wasanii na wadau wa Kampeni ya Uzalendo Kwanza wamepewa kwa ajili ya kuwekeza katika sekta ya kilimo.

Na Kajunason/MMG-Handeni-Tanga.

Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Godwin Godwe amekabidhi ardhi yenye ukubwa wa hekari 282 katika kijiji cha Kitumbi kwa wasanii na wadau wengine wanaofanya kampeni ya UZALENDO KWANZA.

Akizungumza wakati akikabidhi ardhi hiyo katika kijiji cha Kitumbi, Handeni mkoani Tanga, alisema kuwa hatua hiyo inalenga kukuza kilimo na maendeleo katika kijiji hicho ikiwa ni jitihada za kumuunga mkono Dkt. John Pombe Magufuli kuendeleza nchi ya viwanda na biashara.

Wadau wa Kampeni ya Uzalendo Kwanza wakiwemo wasanii wa filamu, muziki na wachezaji mpira wa zamani wameamua kushiriki katika maendeleo ya taifa kwa kujihusisha na kilimo tofauti na kazi zao za kila siku za sanaa.

"Handeni ni sehemu ambayo korosho, alizeti, ndizi vinakuwa sana na niwaambie tu mapema mwakani kiwanda kutengeneza juisi ya nanasi kinafunguliwa Kwa Msisi, tena kitakuwa na uwezo wa kuchukua tani 80,000 za nanasi kwa mwaka na kitakuwa cha pili Afrika kwa kuzalisha juisi ya nanasi, hapo kazi kwenu kuchangamkia fursa," Alisema Mhe. Gondwe.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa UZALENDO KWANZA, msanii Steve Nyerere alimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Martine Shigella, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Gondwe na vingozi wa kijiji kwa kuwapa eneo la kuwekeza katika sekta ya kilimo.

"Sisi tunawashukuru wote kwa moyo mliotuonyesha, hatuna cha kuwalipa bali tutapambana kwa nguvu zetu ili kutimiza malengo ya eneo mlilotupa, Uzalendo Kwanza Oyeeee!," alisema Msanii Steve Nyerere.

Nae diwani wa Kata ya Kitumbi, Charles Abeid amewakaribisha wasanii hao kwa mikono miwili na kuwaomba wawasaidie kumalizia ujenzi wa zahanati yao ambao umekuwa ukisua sua kutokana na kukosekana kwa fedha.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.