Na Emmanuel J. Shilatu
Ni miaka 53
imetimia tangu jahazi lililowabeba Watanganyika na Wazanzibar liweke
historia ya kung’oa nanga mara baada ya Jamhuri Muungano wa Tanzania
kuzaliwa rasmi mnamo April 26,1964.
Hii ilitokana na ujasiri, ushupavu na nia ya dhati waliyokuwa nayo waasisi wa Muungano huu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (Tanganyika) na Abeid Aman Karume (Zanzibar).
Hii ilitokana na ujasiri, ushupavu na nia ya dhati waliyokuwa nayo waasisi wa Muungano huu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (Tanganyika) na Abeid Aman Karume (Zanzibar).
Hatua hiyo
ilifikiwa kutokana na mtiririko wa kimazingira na mahusiano ambayo
yalishabihiana kama sio kufanana kabisa kwa pande zote mbili (Tanganyika
na Zanzibar). Zipo sababu za kijiografia, kisayansi, kitamaduni na
kihistoria zilizochangia huu muungano wetu.
Kutokana na
sababu za kijiografia na kisayansi inaaminika kabisa kwamba Visiwa vya
Zanzibar (Pemba na Unguja) vilikuwa vimeungana na hata kushikamana kwa
pamoja pembezoni mwa pwani ya ardhi ya Tanganyika. Hivyo tangu awali
tulikuwa ni kitu kimoja, tulio katika ardhi moja na ya pamoja.
Pia kuna historia
(isiyo na shaka) ya muingiliano wa kiutamaduni baina ya Wakazi wa
Tanganyika na Zanzibar ambapo hali nzima ya kuoa ama kuolewa ilizidi
kushamiri baina yao.
Halikadhalika
harakati za kudai ukombozi wa uhuru wetu ili tuweze kujitawala wenyewe
kutoka kwa dudu la wakoloni nazo zilichangia kutuunganisha. Inaaminika
(na ndiyo ilivyo) ya kuwa asilimia kubwa ya Wazanzibar walishiriki
kwenye harakati za kudai Uhuru wa Tanganyika kutoka kwa Mwingereza
ambapo kutokana na nia, ushupavu na nguvu ya pamoja walifanikiwa kupata
Uhuru wa Tanganyika mnamo Desemba 9, 1961.
Lakini pia licha ya asilimia kubwa ya Wazanzibar kushiriki
katika mchakato wa Mapinduzi ya Zanzibar lakini pia kulikuwepo na
asilimia kubwa ya mchango wa ushiriki kutoka kwa Watanganyika. Hatimaye
matunda yake yalionekana ya mapinduzi matukufu yaliyofikia kilele katika
uwanja wa Gombani Pemba yaliyofanyika Jamhuri 12, 1964, baada ya
kuchoshwa na hila na ghiliba za Waarabu uliotamalaki visiwani humo kwa
zaidi ya karne mbili na hatimaye waliwaacha wazalendo watwana katika
ardhi yao.
Pia tusisahau lengo na nia ya dhati aliyokuwa nayo Mwalimu
Nyerere ya kutaka kuiunganisha Afrika mzima kwa hatua lakini jitihada
zake zilianza kuzaa matunda ambayo hayatakaa yatokee tena Afrika kwa
kuiunganisha Tanganyika na Zanzibar.
Mnamo April 22, 1964, Maraisi wa nchi hizi mbili ambazo
sasa zinaunda Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (wa Jamhuri ya
Tanganyika) na Abeid Amani Karume (wa Jamhuri ya watu wa Zanzibar )
walitia sahihi Mkataba wa kimataifa wa kuunganisha nchi zao,
unaojulikana kama “Hati ya Muungano” (Articles of union) na hivyo kuunda
Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ama United Republic of
Tanganyika and Zanzibar (URTZ) ambao ni muungano sahihi kabisa kisheria
na unaotambulika Kikatiba.
Siku ya Jumatatu ya tarehe 26 Aprili, 1964 viongozi wa nchi
zote mbili walikutana katika ukumbi wa Karimjee kwa nia ama lengo moja
tu la kubadilishana “Hati za Muungano”.
Wananchi wa
Tanzania walipiga kura kwa mara ya kwanza katika uchaguzi wa kwanza
kabisa wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo mwaka 1965.
Kama nilivyodokeza kwamba Muungano wa Tanzania ulifikiwa
kwa kutiwa sahihi mkataba unaoitwa Hati ya Muungano (Articles of the
Union) na wakuu wa nchi hizi mbili, Mwalimu Nyerere (Tanganyika) na
Abeid Karume (Zanzibar) Aprili 22,1964 na kuridhiwa na mabunge ya nchi
hizo Aprili 25, 1964 na hatimaye kuwa sheria ya Muungano ya (Acts of
Union) ya mwaka 1964.
Kimsingi sheria ya Muungano ndiyo iliyoanzisha na ndiyo
iliyopewa haki ya chombo cha kikatiba kinachodhibiti katiba zote mbili
za Serikali ya Muungano.
Mwanzoni kabisa
Hati ya Muungano (Articles of Union) iliyomo ndani ya sheria ya Muungano
iliorodhesha na hata kudadavua mambo 11 ya Muungano. Mambo hayo ni kama
vile:- Mambo ya nchi za nje, Ulinzi na usalama (lakini si usalama wa
Taifa); Polisi, Uraia, uhamiaji, mikopo na biashara za nchi za nje,
utumishi katika serikali ya Muungano, kodi ya mapato, usimamizi wa
fedha, Bandari, Usafiri wa anga, Posta na simu.
Kwa nia safi na malengo mazuri yanayojitokeza Hati ya
Muungano imekuwa ikiboreshwa zaidi kwa kadri siku zinavyozidi kusonga
mbele kwa malengo kusudi ya kuleta umoja, mshikamano, amani na utulivu
wetu ule ule tulioanza nao awali na halikadhalika maridhiko
yanayoendelea kuufanya Muungano huu uendelee kudumu hadi hii kesho.
Ndio maana mtu timamu hatoshangaa sana kuona Hati ya
Muungano ikiendelea kuboreshwa kila siku (na itaendelea hivyo) ambapo
ilianzia na mambo 11 ambapo hii leo yamefikia takribani 23.
Mengineyo ama baadhi ya yale yalioongezeka ni kama vile;-
Noti; Elimu ya juu,; Maliasili na mafuta (mafuta) yasiyochujwa, bidhaa
za mafuta na gesi asilia , ya mwaka 1968; Baraza la Mitihani ya Taifa;
utafiti; utabiri wa hali ya hewa; Takwimu,; Mahakama ya Rufaa ya juu ya
mwaka 1979; pamoja na uandikishwaji wa vyama vya kisiasa .
Tusisahau mwaka 1965 iliundwa katiba ya muda ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania (The Interim Constitution of The United Republic of
Tanzania) mpaka kufikia mwaka 1977 ndipo ilipoundwa katiba ya kudumu ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ndiyo inaendesha nchi hadi sasa.
Mwaka huo huo wa 1977 (yaani miaka 13 baada ya Muungano
kutokea) kulikuwa na muungano wa vyama vikubwa viwili kuungana kutoka
pande zote mbili (Bara na Visiwani). Vyama hivyo ni TANU (Tanganyika
African National Union) pamoja na ASP (Afro Shiraz Party) cha Zanzibar
kuungana na kuunda Chama cha Mapinduzi (CCM) .
Hatua ama vitendo na mafanikio hayo si tu kwamba
yalidumisha bali hata yaliendeleza kukuza Muungano wetu ambao Jahazi
lake liligubikwa na misukosuko ya mawimbi makubwa baharini uliojaa uzito
wa mambo mbalimbali uliokuja kwa sera ya kero zilizoleta chokochoko
mbalimbali katika Muungano wetu., ambao hatutakiwi kamwe kuusahau
maishani mwetu.
Tusisahau mchezo
mchafu uliojaa rafu za kutisha uliotaka kufanywa na Bunge miaka ya 1990
na 1992 ya kutaka kuyakubali madai yaliyotolewa na kundi la G55 ambalo
lilitaka kuundwa kwa Serikali ya Tanganyika , hali hii ingetuvuruga
kwani ilihitaji uwepo na serikali tatu yaani Serikali ya Tanganyika,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Hakika yatupasa tuzishukuru hekima na busara za Mwalimu
Nyerere kwa kutuokoa na chokochoko ya kero hii.
Pia tusiisahau kero ama chokochoko nyingine ya Muungano
wetu iliyoibuka Decemba 1, 1992, ambayo Zanzibar ilitaka kujiunga na
umoja wa Nchi za Kiislam Duniani (OIC) kama nchi nje ya Muungano.
Tuendelee kukumbuka ni kwa jinsi gani Zanzibar iliyokuwa
inasaka ukuu nje ya Muungano kwa kuibua madai ya Bendera ya Taifa lake
(Zanzibar), wimbo wa Taifa, na nembo yao ya Taifa.
Kwa nyakati tofauti tofauti tumekuwa tukisikia baadhi ya
Wazanzibari walio wachache wakiilalamikia hali nzima ya ongezeko la
mambo kwenye Hati Muungano (Articles of Union) kutoka mambo 11 hadi
kufikia 23 ambalo ni sawa na ongezeko la mambo 12 ambao kwa baadhi yao
hawaoni umuhimu wa wa uwepo wake na hata kutishia kujitoa. Ila asilimia
kubwa ya Wazanzibari wanayaunga mkono, hali iliyo sababisha hoja ya
wachache kuzidiwa nguvu.
Pia tumekwisha sikia jinsi gani Wazanzibari wanavyotaka
jambo la maliasili ya mafuta pamoja na mafuta yasiyochujwa na aina
nyingine za mafuta au bidhaa na gesi asilia iondolewe katika masuala ya
Muungano ili Zanzibar ipate kunufaika zaidi na maliasili zake.
Kukuru kakara za
Wazanzibari zinatookana na madai yao ya kuwa Tanganyika(Bara) imeimeza
Zanzibar (Visiwani) katika masuala mazima yahusuyo Muungano. Ikumbukwe
Ubaguzi wa dhana ya Tanganyika umeimeza Zanzibar si ya kweli na hii
imebainishwa katika katiba ya Muungano kuwa kuna Serikali ya Jamhuri ya
Muungano na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Haya ni mapenzi
ya dhati waliyoonyesha kwa Wazanzibari kwa kuwaruhusu wawe na serikali
yao ya Mapinduzi ya Zanzibar. Ikumbukwe Serikali ya Muungano inaongozwa
na katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar inaongozwa na Baraza la Mapinduzi ya Zanzibar na chombo chao
cha kutunga sheria kinaitwa Baraza la Wawakilishi.
Ndugu zangu hali
ya kupuuzia na hata kuuchezea Muungano wetu ni hatari sana tena ni
dhambi iliyotukuka. Mathalani Wazanzibari wakiamua kujiengua kwenye huu
Muungano ili wawe kivyao vyao,hawatabaki salama.
Mwalimu Nyerere
alishawahi kusema ya kuwa “wakifika kwenye hatua hiyo watagundua kuwa
ndani yao kuna Wazanzibari na Wazanzibara”. Nao wataamua kuwafukuza wale
wa Wazanzibara, lakini hiyo haitakuwa mwisho. Punde si punde
watajigundua kuwa nao (Wazanzibari) wamegawanyika kwani kuna Wapemba na
Waunguja, na wakifikia hapo pia hawatakuwa salama ni lazima machafuko
yatatokea.
Daima Wazanzibari watambue ya kuwa dhambi ya kutokutamalaki
kwa dhana ya Unguja na Pemba unatoka na kufunikwa na kivuli cha
mwamvuli cha Muungano. Hivyo umoja, mshikamano, amani na utulivu wao
unategemea sana uwepo wa nguzo hii imara ya Muungano huu tulionao.
Vivyo hivyo kwa
watu wa Bara (Tanganyika) ni rahisi kwao kutafunwa na dhambi ile ile ya
ubaguzi watakayo ianzisha nje ya uwepo wa Muungano ni rahisi sana kwa
ukabila, udini, ukanda na hata U-rangi kutamalaki ndani ya jamii
wakishafikia hapo, hawatabaki salama kwani watachafuana tu.
Muungano huu tulionao unawafanya wale wageni, mataifa ya
nje na watu wote wenye hila, donge, roho ya korosho kuogopa kutugusa na
kutuvuruga kutokana na kuwepo kwa nguvu kubwa ya umoja, ushirikiano na
mshikamano baina yetu.
Muungano huu wetu
unatupatia fursa kubwa ya uhuru wa kusafiri kwa pande zote iwe ni bara
ama ni visiwani. Leo hii ni rahisi sana kwa mtu wa bara kwenda Visiwani
na hata wale wa Visiwani kuja Bara kwa uhuru zaidi kwani Uhuru huo wa
uwepo wa nafasi hiyo umeshalipiwa na huu Muungano wetu tulionao.
Kutokana na uwepo
wa uhuru wa kusafiri usio na mipaka baina yetu, pia Muungano wetu
tulionao unazidi kutuongezea fursa na nafasi zaidi ya uwanja mpana wa
ufanyaji biashara. Hali hii imesababisha uwepo wa mzunguko mkubwa wa
pesa ndani yetu kwani si jambo la ajabu kuona pesa zikitoka Visiwani
(Zanzibar) kuja Bara (Tanganyika) kupitia mabadilishano ya bidhaa kama
vile nafaka, kahawa, matunda, vipuri vya magari na kadhalika.
Pia si jambo geni
tena kwa sasa kuona pesa zikivuka Bahari na kwenda visiwani Zanzibar
kwa ajili ya ufanyaji ama ununuzi wa biashara kama vile Magari, nazi,
Karafuu, Tende na kadhalika.
Muungano huu
unatuzidishia fursa ya mianya ya uwanja mpana tena usio na kikomo wa
ufanyaji biashara, Muungano huu hautubagui ama kutojulisha au kuwa na
upendeleo wa upatikanaji wa Elimu bora, huduma za kijamii bora, Muungano
hautugawi wala kuwa na upendeleo bali umejaa uwiano sahihi wa
upatikanaji wa mabo yote ya msingi yaliyomo ndani ya “Hati ya Muungano”
(Articles of union).
Muungano huu ni nguzo imara katika muktadha mzima
wa nyanja za kimaisha yetu.
Ni ukweli
uliodhahiri kuwa haitakaa itokee Muungano kama huu (wa Tanganyika na
Zanzibar) hapa Barani Afrika umoja ushirikiano, ushikamano, amani na
utulivu ni sehemu mojawapo ya manufaa ya Muungano huu.
Njia mojawapo ya
kuwaenzi vyema waasisi wetu ni kwa kuudumisha Muungano wetu ambao ni
urithi wa aina yake waliotuachia. Watanzania yatupasa tuenzi Muungano
wetu kwa kuulinda na kuudumisha kwa vitendo kwani ni nguzo na fahari ya
kipekee na ya aina yake Barani Afrika.
Tuadhimishe Miaka 53 ya Muungano kwa kuudumisha, kupiga vita madawa ya kulevya na kufanya kazi kwa bidii.
Endapo itatokea
kiongozi yeyote Yule ama utawala wowote ule utakaokuwa na malengo ya
kuubomoa ama kuuvunja Muungano huu, basi ajue dhambi hii itamtafuna yeye
na kizazi chake milele.
Mungu atuepushe
na mawazo ya kuuvunja Muungano huu vichwani mwa viongozi/watawala wetu,
atuepushe na balaa hili lisijitokeze kwenye Katiba Mpya ijayo. Kheri ya
Miaka 53 ya maadhimisho ya Muungano!!
Tuwasiliane 0767 488622 www.ndgshilatu.blogspot.com
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.