ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, April 7, 2017

FARU FAUSTA ALITIKISA BUNGE.

WAKATI kishindo cha faru dume aitwaye John kikitulia baada ya kubainika kuwa alifariki na serikali kuchukua hatua kadhaa kuhusiana na chanzo cha kifo chake, faru mwingine jike aitwaye Fausta alitwaa nafasi ya mjadala bungeni mjini Dodoma jana kuhusiana na gharama za kumtunza kwa mwezi.

Kwa mujibu wa kile kilichoelezwa kuhusiana na faru huyo ambaye pia yupo katika Hifadhi ya Ngorongoro mkoani Arusha kama ilivyokuwa kwa faru John, ni kwamba gharama za kumtunza kwa mwezi ni Sh. milioni 64 na hivyo kushtua baadhi ya wabunge kiasi cha kuibua maswali.

Kwa mujibu wa chanzo cha Nipashe, mshahara wa mbunge mmoja kwa mwezi kabla ya makato ni takribani Sh. milioni 3.6, hivyo gharama hizo za kumtunza Faru Fausta ni sawa na wastani wa mishahara ya wabunge 17 kabla ya makato.

Aliyeibua suala hilo la Faru Fausta ni Mbunge wa Babati Mjini(Chadema),Pauline Gekul, ambaye alidai kushtushwa na kitendo cha Hifadhi ya Ngorongoro kutumia kiasi cha Sh. Milioni 64 kwa mwezi sawa na Sh.Milioni 768 kwa mwaka kumlisha na kumtunza faru huyo.

Akiuliza swali la nyongeza kwa Waziri wa Maliasili na Utalii bungeni jana, Gekul alisema faru huyo amekuwa akigharimiwa fedha nyingi na kuhoji serikali ina mpango gani kuhusiana naye.

Akijibu swali hilo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe, alikiri faru huyo kutunzwa kwa gharama kubwa kwa ajili ya kumlisha kwa sababu ni mzee.

Alisema mbali na hilo, mnyama huyo pia huandamwa na magonjwa mbalimbali na ndiyo maana ana gharimiwa kwa fedha zinazoonekana kuwa ni gharama kubwa.

Aidha, Prof. Maghembe alisema wanafanya hivyo pia kwa sababu wanyama wa aina hiyo ni wachache katika hifadhi nchini.

“Hivi sasa utafiti unafanyika kwa kumtumia faru Fausta juu ya namna ya kuishi na wanyama wa aina hiyo ili waweze kuishi maisha marefu… ni kweli kufanya hivi ni gharama kubwa lakini takwimu zinazopatikana zina thamani halisi,”alisema.

Pamoja na majibu hayo, Waziri Maghembe aliendelea kubanwa kuhusiana na gharama za faru huyo. Mbunge wa Tunduma (Chadema), Frank Mwakajoka, aliomba mwongozo baada ya kipindi cha maswali na majibu kuhusu majibu ya waziri huyo juu ya faru Fausta kutunzwa kwa fedha hizo huku ikielezwa kuwa ni mzee ilhali ikifahamika kuwa kwa hali yake, kamwe mnyama huyo hawezi kuingiza faida yoyote.

Akijibu muongozo huo, Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema katika hifadhi hiyo yupo pia Faru Ndugai na kumwambia waziri kwa kutania kuwa siku faru huyo (Ndugai) akitoweka patachimbika bungeni.

Hata hivyo, kuhusiana na swali kuhusu faru Fausta, Ndugai alisema suala hilo analiachia wizara ili wakalifanyie kazi.

TAARIFA ZAIDI KUHUSU FARU FAUSTA
Kwa mujibu wa Mhifadhi Mkuu wa Ngorongoro, Dk Freddy Manongi, ambaye alizungumza na Nipashe hivi karibuni, ni kwamba faru Fausta ni mzee mwenye miaka 54 na kwamba, alipokuwa porini alikuwa akishambuliwa na fisi na kupata vidonda vingi.

Alisema baada ya kumwona fausta akiwa katika hali mbaya kiafya na pia kuwa katika hatari kubwa ya kuuawa na fisi kutokana na uzee wake, askari wa uhifadhi walimchukua na kumtengea eneo maalum huku wakilazimika kimnunulia chakula kama miwa kutoka wilayani Babati na pia kumpatia huduma nyingine muhimu.

Alisema kutokana na jitihada zinazofanyika katika kumtunza, hivi sasa vidonda aliyokuwa navyo vimepona na anaendelea vizuri.

Hata hivyo, taarifa nyingine kutoka kwenye hifadhi hiyo jana zilidai kuwa kutokana na umri wake mkubwa, faru huyo hivi sasa ana tatizo la kutoona na jambo hilo linamuweka katika wakati mgumu kimaisha ikiwa ataachiwa aishi porini bila ya uangalizi maalumu.

*Taarifa ya ziada na John Ngunge (Arusha) na Salome Kitomari (Dar)

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.