NAIBU WAZIRI WA HABARI UTAMADUNI SANAA NA MICHEZO AZINDUA MAZOEZI YA
MWILI KWA WAKAZI WA WILAYA YA ILEMELA
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mh.
Anastazia James Wambura leo tarehe 14.01.2017 ikiwa ni jumamosi ya pili ya
mwezi amezindua mpango wa mazoezi kwa wananchi na wakazi wa Wilaya ya Ilemela
ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Amewataka wananchi na wakazi wa
Ilemela ambao leo waliongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Dr. Leonard Masale,
kufanya mazoezi ya mwili kama afanyavyo Rais mstaafu wa awamu ya Pili ambaye
kwa sasa ana Zaidi ya miaka 90 na amekuwa akifanya mazoezi takribani saa moja
kila siku, kwani mazoezi humfanya mtu kuwa mkakamavu na pia kuzifanya seli za
mwili kuufanya mwili kutozeeka/kutochoka mapema.
Tukumbuke kuwa MAZOEZI NDIYO AFYA YAKO, NA AFYA YAKO NDIYO
MTAJI WAKO, hivyo ukiwa unafanya mazoezi kutakufanya uwe na afya njema
itakayokufanya ushiriki kikamilifu katika shughuli zako za kila siku
zinazokuingizia kipato na ndiyo maana tunasema afya yako ndiyo mtaji wako.
Ukiugua magonjwa hasa haya ambayo
si ya kuambukizwa kama vile Shinikizo la damu (pressure), Kiharusi au kisukari,
ni magojwa ambayo yatakufanya kutofanya kazi kwa muda mrefu lakini pia utatumia
gharama kubwa kujitibu, hivyo amewataka wananchi wote kwa ujumla kuyafanya
mazoezi kuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku.
Amesema pia, serikali imekuwa
ikitumia gharama kubwa ya kununua madawa na kutibu wananchi wake, fedha ambayo
ingeweza kuwekwa katika shughuli nyingine za kimaendeleo endapo wagonjwa wa
magonjwa haya yangeweza kuepukika kwa kufanya mazoezi.
Akizungumza kwa niaba ya
watumishi wa Manispaa ya ilemela na wakazi/wananchi wa Wilaya hii, Mkuu wa
Wilaya ya Ilemela Dkt. Leonard Masale, kwanza amemshukuru Naibu Waziri kwa
kuzindua mpango wa mazoezi katika wilaya ya Ilemela, na kuwaelekeza watendaji
wa Kata washirikiane na waheshimiwa madiwani kuwaongoza na kuwahamisha wananchi
walio katika kata zao kushiriki mazoezi hasa kila jumamosi ya pili ya kila
mwezi. Lakini pia amehaidi mazoezi ya mwezi ujao yatashirikisha wananchi wengi
kwani leo waliojitokeza wengi ni watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya
Ilemela, na baada ya mazoezi hayo wananchi wote watakuwa wakifanya mazoezi
katika kata zao.
Pamoja nae, kamanda wa polisi wa
Wilaya ya Ilemela, Mrakibu wa Polisi, Evodius Kasigwa, amesema wao polisi
wamekuwa wakifanya mazoezi haya kila jumamosi ya wiki.
Mazoezi haya yalianzia katika
kiwanja cha Furahisha kwa kutembea matembezi ya Kilomita 3 kwa kupitia mtaa wa
Ghana, Kitangiri na kisha kurudi katika uwanja wa Furahisha na kufanya mazoezi
ya viungo.
Imetolewa na:
Kizito Bahati
Afisa Michezo
Manispaa ya Ilemela.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.