Rais na Mkurugenzi Mtendaji wa Makampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL Group), Mohammed Dewji ametangazwa na Jarida la African Leadership kuwa mshindi wa tuzo ya African Leadership Magazine Person of the year 2016 baada ya kuibuka mshindi katika kinyang’anyiro kilishohusisha watu nane.
MO Dewji ambaye ni Mtanzania anayejihusisha na biashara kupitia kampuni yake ya MeTL Group na kusaidia jamii kupitia Taasisi ya MO Dewji ameibuka mshindi kwa kupata asilimia 60.8 ya kura zote zilizopigwa akifuatiwa na Rais mstaafu wa Ghana, Dramani Mahama ambaye alipata asilimia 30.2.
Wengine waliowania tuzo hiyo ni Strive Masiyiwa, Chris Kirubi, Akinwumi Adesina, Cyril Ramaphosa, Atiku Abubakar na Aisha Mohammed.
Akizungumza kuhusu MO Dewji, Mjumbe wa Bodi ya Ushauri wa Jarida la African Leadership, Joe Beasley amemtaja MO Dewji kama mtu ambaye anaumuhimu mkubwa kutokana na dhamira yake ya kusaidia bara la Afrika kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira kwa kutoa nafasi nyingi za kazi.
“Dhamira ya Dewji ni kutengeneza ajira jambo ambalo ni kiini cha tatizo kubwa linalokabili Afrika la ukosefu wa ajira … kupitia biashara zake amesaidia kupunguza ukosefu wa ajira, kupata utajiri na kutoa ajira kwa vijana ambao hawana ajira barani [Afrika],” alisema Beasley.
Mohammed Dewji anakuwa mshindi wa tuzo hiyo kwa mwaka 2016 ambapo kwa mwaka 2015 ilichukuliwa na Rais Mstaafu wa Nigeria, Goodluck Jonathan.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.