Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo amewashukuru Viongozi na Waumini wa Kanisa la Anglikana na Madhehebu mengine ya Dini hapa nchini kwa kuendelea kuliombea Taifa na kudumisha amani na utulivu.
Rais Magufuli amezungumza hayo mara baada ya kumalizika kwa Ibada katika kanisa la Angilikana la Mtakatifu Albano lilipo Jijini Dar es salaam ambapo Rais Magufuli aliongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli.
Dkt. Magufuli amesisitiza kuwa Viongozi wa Dini wanafanya kazi kubwa na muhimu katika Taifa na kwamba Watanzania wote bila kujali dini zao, itikadi za kisiasa, makundi na kanda zao wana wajibu wa kuungana na Viongozi hao ili nia hiyo njema iendelee kufanikiwa.
“Ninawashukuru kwa sababu mnaendelea kuliombea Taifa hili, ninawashukuru kwa sababu siku zote mmekuwa mkipiga magoti na kumtanguliza Mungu mbele, ninawashukuru kwa sababu mnaendelea kuombea amani ya nchi yetu na upendo udumu ndani yetu sisi sote.
“Makanisa yote, Madhehebu yote, Dini zote, Vyama vyote, upendo tukiujenga ndiyo tutaiendeleza vizuri Tanzania yetu” amesema Rais Magufuli.
Kwa upande Padre Jackson Sostenes aliyeongoza Ibada hiyo amemshukuru Rais Magufuli kwa kuungana na waumini wa Kanisa hilo katika Ibada ya Jumapili na ameahidi kuwa Viongozi na Waumini wa Kanisa hilo wataendelea kumuombea na kuliombea Taifa.
Katika Ibada hiyo Rais Magufuli ametoa Shilingi Milioni 1 kuchangia vikundi vya kwaya vya kanisa hilo.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.