ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, October 31, 2015

TAARIFA YA ZADIA KUHUSU KUFUTWA KWA MATOKEO YA UCHAGUZI ZANZIBAR

Logo ya Zadia
Jumuiya ya Wazanzibari Waishio Nchini Marekani (ZADIA), imekuwa ikifuatilia kwa karibu na makini zaidi zoezi zima la Uchaguzi Mkuu visiwani Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Kwa kiasi kikubwa mchakato wa uchaguzi ulifanyika kwa njia za amani na utulivu. Hata hivyo ZADIA imeshtushwa mno na tamko la Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Mh. Jecha Salim Jecha la kutangaza kuufuta Uchaguzi Mkuu Zanzibar na matokeo yake.
Ama kwa hakika kitendo hicho hakikuwa cha busara na kinapelekea kurudisha nyuma maendeleao ya demokrasia Zanzibar, na vilevile hakiashirii mustakbali mwema kwa nchi yetu tuipendayo. Wazanzibari wameelezea maoni na matakwa yao kwenye visanduku vya kupigia kura, na maoni na matakwa yao hayo yanapaswa kusikilizwa na kuheshimiwa.
Kwa hivyo, ZADIA inatoa wito kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar, kumalizia mchakato mzima wa kuhesabu kura kwa majimbo yaliyobakia na kutoa matokeo ya mwisho ya Uchaguzi na kumtangaza mshindi ili kuiepusha Zanzibar yetu tuipendayo kuingia katika hali ya mtafaruku na mifarakano isiyokuwa na tija bali kuleta hasara.
ZADIA pia inaungana na jumuiya zote za kimataifa ambazo zimetoa msimamo wao juu ya uchaguzi wa Zanzibar, hasa ubalozi wa Marekani nchini Tanzania, ambao ni kiungo madhubuti kati ya Wazanzibari walioko Zanzibar na wenzao wanaoishi nchini Marekani.
Aidha, tunapenda kumkumbusha Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Dakta Ali Mohammed Shein kuwa Wazanzibari walimpa amana kubwa ya kuwaongoza, na kwa hivyo ni wajibu wake kuienzi amana hiyo kwa kuchukuwa hatua za kiungwana za kuitoa Zanzibar kwenye mgando huu wa kisiasa. Hali hii iliyopo sasa inaleta wasiwasi miongoni mwa raia na imekua ikiathiri maisha yao ya kila siku, na ikiachwa kuendelea huenda ikaathiri pia mustakbali maisha yao kwa jumla.
ZADIA pia inamtolea wito Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kutumia mamlaka yake aliyonayo kuhakikisha Zanzibar inatoka kwenye mkwamo huu wa kisiasa na kwamba anaondoka madarakani akiiacha Zanzibar ikiwa katika hali ya amani na utulivu. Kwa kufanya hivyo atauthibitishia ulimwengu kuwa kweli Tanzania ni kisima cha amani.
Na mwisho tunawaomba Wazanzibari, wapenzi wa Zanzibar, na Watanzania wote kwa ujumla popote pale walipo, wajitahidi kufanya mawasiliano na Jumuiya nyengine za Kimataifa ili ziingilie kati suala hili kabla nchi yetu haijaingia kwenye mtafaruku mkubwa wa kisiasa na kijamii na hata kupelekea kuhatarisha amani ya nchi yetu.
Mungu Ibariki, Zanzibar.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.