Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa amesema anawatakia kila la heri wanaobeza nguvu ya umma.
Kutokana
na umati wa watu waliojitokeza jana kumlaki kuanzia Uwanja wa Ndege wa
Mwanza alikowasili saa saba mchana, iliuchukua zaidi ya saa mbili
msafara wake kuingia Viwanja vya Furahisha saa tisa alasiri, ambako ni
takriban kilomita nane.
Katika hotuba yake iliyochukua
dakika 14 kuanzia saa 11.53 hadi 12.07 jioni, Lowassa alisema
anawasikitikia wanaobeza nguvu hiyo ya umma.
“Haya siyo mapenzi, haya ni mahaba. Wanaobeza nguvu hii ya umma nawatakia kila la heri,” alisema Lowassa huku akishangiliwa na umati huo.
“Haya siyo mapenzi, haya ni mahaba. Wanaobeza nguvu hii ya umma nawatakia kila la heri,” alisema Lowassa huku akishangiliwa na umati huo.
Akizungumzia
idadi hiyo ya wananchi, mke wa mgombea huyo, Regina Lowassa alisema
haijawahi kutokea maeneo yote waliyotembelea Dar es Salaam, Mbeya na
Arusha.
“Mwanza nimewapenda, nafikiri baba (Lowassa) akitoka hapa atalala usingizi mzuri mzito,” alisema Regina.
Lowassa
aliwataka polisi kutoingilia mchakato wa uchaguzi na kutumiwa na CCM
kupambana na wapinzani na kwamba, wakiendelea watakuwa wanajitafutia
tiketi ya kupelekwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), mjini The
Hegue.
“Nimesikitishwa sana kuwa watu wamepigwa mabomu
asubuhi. Mkiendelea na mchezo huu tukimaliza uchaguzi tutawapeleka The
Hague mkakipate cha mtoto na huko hamtarudi tena,” alisema.
Mabomu yarindima
Polisi
mkoani hapa jana walilazimika kutumia mabomu ya machozi, kuwatawanya
wafuasi wa vyama vinavyounda Ukawa ambao walifurika Uwanja vya Ndege wa
Mwanza kumpokea Lowassa.
Lowassa aliwasili akiwa
ameambatana na mgombea mwenza, Juma Duni Haji, Mwenyekiti wa Chadema,
Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia, Kaimu
Mwenyekiti wa CUF, Twaha Taslima na Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel
Makaidi.
Mabomu ya machozi yalianza kurindima saa tano
asubuhi, baada ya baadhi ya wafuasi wa Ukawa kutaka kuingia kwenye lango
la uwanja wa ndege, huku wengine wakijaribu kuwatunishia misuli polisi
kwa kuwatupia mawe.
Hekaheka za mapokezi ya Lowassa
zilianza saa mbili asubuhi, baada ya maelfu ya wafuasi wa Ukawa wakiwa
na mabango yenye ujumbe mbalimbali ikiwamo: “Oil chafu ni kiboko ya
mchwa” kutanda kwenye barabara inayoelekea uwanja wa ndege.
Magari
ya polisi aina ya Land Rover Defender na Landcruiser yapatayo matano
yalitanda kwenye barabara ya uwanja wa ndege, huku yakizuia magari
kuingia uwanjani.
Kabla ya muda wa mkutano wa mgombea
huyo wa urais kuanza kwenye Viwanja vya Furahisha, uwanja ulianza kujaa
maelfu ya wakazi wa Mwanza kuanzia saa tatu asubuhi.
Msafara
wa Lowassa kutoka uwanja vya ndege uliongozwa na pikipiki ambazo
zilikuwa zinapeperusha bendera za vyama vya CUF, Chadema ,NCCR Mageuzi
na NLD, huku viongozi hao wakiwa kwenye magari ya wazi.
Lowassa
alisema ziara yake hiyo inahusu kujitambulisha na asingependa kuwapa
nafasi wapinzani wake kumtafsiri kuwa hajui sheria, lakini kero za
Mwanza anazifahamu hivyo akaahidi kurejea na mikakati ya kuzitatua.
Alisema
anafahamu Wamachinga, meli ya Mv Victoria, kiwanda kikubwa cha
kusindika nyama, reli, ujenzi wa uwanja mkubwa wa ndege, bei ndogo ya
pamba na tatizo la umeme.
Kuhusu suala la umeme,
Lowassa alisema Mbunge wa Nyamagana, Ezekia Wenje ni kijana anayefanya
uamuzi mgumu kama yeye hivyo alimtaka leo kwenda kwa Meneja wa Tanesco
Mwanza ili kujua tatizo, asipopewa majibu ya kuridhisha ampigie simu
yeye (Lowassa).
Aliyewahi
kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Mbunge wa Nyamagana, Lawrence Masha
alisema: “Ndugu zangu nimerudi nyumbani, naomba niwaambie Watanzania
wote kwa ujumla hapa tulipo tupo kwenye harakati za kuikomboa nchi yetu.
Leo
nasimama hapa kama mwana Mwanza, lengo ni kuhakikisha tunapambana na
kuikomboa Tanzania, naomba Oktoba 25 tufanye kazi moja tu ya kuchagua
viongozi wa Ukawa.”
Masha kwa mara ya kwanza aliahidi
kumsaidia Wenje kwenye kampeni na kueleza kuwa, atakuwa bega kwa bega na
Wenje, jambo ambalo lilisababisha umati kulipuka kwa nderemo.
Mgeja: Makapi yanafua umeme
Aliyekuwa
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja alisema alipotangaza
kuhama CCM alipigiwa zaidi ya simu 800 za kumpongeza na sita za
kumlaumu, lakini amejifunza kuwa alikuwa kwenye nyumba inayoteketea.
“Wanasema
makapi, hivi hawajui kuwa hivi sasa makapi ndiyo mali, yanafua umeme,”
alisema na kuongeza: “Wanamlinganisha Lowassa na mgombea wao (bila
kumtaja), wanamdhalilisha Lowassa huyo siyo saizi yake.”
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.