ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, March 23, 2015

MAKAMU WA RAIS DKT. BILAL AHITIMISHA KILELE CHA MAADHIMISHO YA 27 YA WIKI YA MAJI MKOANI MARA.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, Balozi wa Ufaransa nchini, Malika Berak (wa pili kulia) wakikata utepe kwa pamoja kuashiria kuzindua rasmi mradi mkubwa wa maji wa Musoma mjini uliogharimu jumla ya Sh. Bilioni 41, wakati wa sherehe za Kilele cha maadhimisho ya 27 ya Wiki ya Maji zilizofanyika Kitaifa Mkoani Mara jana Machi 22, 2015. Picha na OMR
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, Balozi wa Ufaransa nchini, Malika Berak (katikati) na Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe (kushoto) kwa pamoja wakifunua kitambaa kuweka Jiwe la Msingi la kata mradi mkubwa wa maji wa Musoma mjini uliogharimu jumla ya Sh. Bilioni 41, wakati wa sherehe za Kilele cha maadhimisho ya 27 ya Wiki ya Maji zilizofanyika Kitaifa Mkoani Mara jana Machi 22, 2015. Picha na OMR
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akipata maelezo ya mradi huo kutoka kwa Mkurugenzi wa Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Musoma, Gantala Said, wakati wa sherehe za Kilele cha maadhimisho ya 27 ya Wiki ya Maji zilizofanyika Kitaifa Mkoani Mara jana Machi 22, 2015. Picha na OMR
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisalimiana na wananchi wa Musoma wakati akiondoka baada ya kuzindua mradi huo mkubwa wa maji jana wakati wa sherehe za Kilele cha maadhimisho ya 27 ya Wiki ya Maji zilizofanyika Kitaifa Mkoani Mara jana Machi 22, 2015. Picha na OMR
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisikiliza maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Idara ya Maji wa Wizara ya Maji, Nadhifa Sadiki, wakati makamu alipokuwa akitembelea mabanda ya maonesho kwenye sherehe za Kilele cha maadhimisho ya 27 ya Wiki ya Maji zilizofanyika Kitaifa kwenye Viwanja vya Mkendo mjini Musoma Mkoani Mara jana Machi 22, 2015. Picha na OMR
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisikiliza maelezo kutoka kwa Meneja wa Bohari Kuu Boko Dar es Salaam, Clepline Bulamo, wakati makamu alipokuwa akitembelea mabanda ya maonesho kwenye sherehe za Kilele cha maadhimisho ya 27 ya Wiki ya Maji zilizofanyika Kitaifa kwenye Viwanja vya Mkendo mjini Musoma Mkoani Mara jana Machi 22, 2015. Picha na OMR
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisikiliza maelezo kutoka kwa Meneja Mauzo wa Kampuni ya Pipe Industries Co. Ltd, Ezra Chiwelesa, wakati makamu alipokuwa akitembelea mabanda ya maonesho kwenye sherehe za Kilele cha maadhimisho ya 27 ya Wiki ya Maji zilizofanyika Kitaifa kwenye Viwanja vya Mkendo mjini Musoma Mkoani Mara jana Machi 22, 2015. Picha na OMR
Makamu wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akimkabidhi Kikombe cha mshindi wa pili kwa kutoa huduma kwa Jamii, Meneja wa Tawi la Davis & Shictliff Ltd, Ellison Malyi, wakati wa  sherehe za Kilele cha maadhimisho ya 27 ya Wiki ya Maji zilizofanyika Kitaifa kwenye Viwanja vya Mkendo mjini Musoma Mkoani Mara jana Machi 22, 2015. Picha na OMR
Makamu wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akimkabidhi Kikombe cha mshindi wa kwanza  kwa kutoa huduma kwa Jamii, Afisa Ugavi wa Bohari Kuu Dar es Salaam, Sophia Mtumbi,  wakati wa  sherehe za Kilele cha maadhimisho ya 27 ya Wiki ya Maji zilizofanyika Kitaifa kwenye Viwanja vya Mkendo mjini Musoma Mkoani Mara jana Machi 22, 2015. Picha na OMR
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akihutubia wananchi wakati wa sherehe za Kilele cha maadhimisho ya 27 ya Wiki ya Maji zilizofanyika Kitaifa kwenye Viwanja vya Mkendo mjini Musoma Mkoani Mara jana Machi 22, 2015. Picha na OMR
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa sherehe hizo za kilele cha maadhimisho ya 27 ya wiki ya maji baada ya kuhutubia na kufunga rasmi sherehe hizo jana. Picha na OMR
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akifurahia ngoma za asili wakati aliwapowasili kwenye uwanja wa ndege wa Musoma jana kwa ajili ya kuhudhuria sherehe za Kilele cha maadhimisho ya 27 ya Wiki ya Maji zilizofanyika Kitaifa kwenye Viwanja vya Mkendo mjini Musoma Mkoani Mara jana Machi 22, 2015. Picha na OMR

HOTUBA YA MHE. DKT. MOHAMMED GHARIB BILAL, MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA KILELE CHA MAADHIMISHO YA 27 YA WIKI YA MAJI MKOANI MARA
TAREHE 22.03.2015

Mheshimiwa Prof. Jumanne A. Maghembe (Mb)
Waziri wa Maji;

Mheshimiwa Prof. Peter Msolla
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji;

Mheshimiwa Kapteni Mstaafu Aseri Msangi
Mkuu wa Mkoa wa Mara;

Mheshimiwa Malika Berak,
Balozi wa Ufaransa Nchini Tanzania;

Waheshimiwa Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa;

Inj. Mbogo Futakamba
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji;

Waheshimiwa Wabunge na Madiwani wa Mkoa wa Mara na Mikoa Jirani;

Viongozi wa Vyama vya Siasa na Serikali;

Washirika wetu wa Maendeleo katika Sekta ya Maji;

Ndugu Wananchi;

Mabibi na Mabwana
Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kutuwezesha kukutana hapa siku ya leo katika Kilele cha Maadhimisho ya 27 ya Wiki ya Maji Kitaifa kwa mwaka 2015 yanayofanyika Mkoani Mara. Namshukuru sana Waziri wa Maji, na Mkuu wa Mkoa na Wananchi kwa kunipa heshima kubwa ya kunialika nije kuungana na wananchi wa Manispaa ya Musoma na Watanzania kwa ujumla kushiriki katika Kilele cha Maadhimisho haya yanayofanyika hapa katika Viwanja vya Mkendo mjini Musoma. Vilevile, niwashukuru wananchi wote wa Mkoa wa Mara kwa mapokezi mazuri waliyonipatia Nasema Asanteni Sana.

Ndugu Wananchi;
Leo hii nchi yetu inaungana na nchi nyingine kote duniani kuadhimisha Siku ya Maji Duniani, ambayo ndiyo kilele cha Wiki ya Maji kwa hapa nchini. Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Wiki ya Maji kwa mwaka huu wa 2015 ni Maji Kwa Maendeleo Endelevu, ambayo inakwenda sambamba na umuhimu na mchango wa Sekta ya Maji kwa Maendeleo ya Sekta nyingine za Kiuchumi na Kijamii.

Tumeanza leo kwa kuweka  Jiwe la Msingi katika Mradi mkubwa wa Maji hapa Mjini Musoma, na mradi huu unatarajiwa kukamilika mwezi Aprili, 2015 na utagharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 41. Ni mategemeo yetu kuwa Manispaa ya Musoma itakuwa na maji ya uhakika kwa asilimia 100 baada ya mradi huu kukamilika.  Tena, mafanikio yatakayopatikana kutokana na kukamilika kwa mradi huu ni pamoja na:
(i)                             Kuongezeka kwa uzalishaji wa maji kutoka mita za ujazo 10,000 za
sasa kwa siku, hadi mita za ujazo 36,000 kwa siku.

(ii)                                Kupanua huduma ya maji katika baadhi ya maeneo ambayo hayana huduma, na maeneo ya mpakani mwa Manispaa ya Musoma kama vile Bisumwa, Etaro na Nyabange.

(iii)                             Ubora wa maji yanayosambazwa kwa wananchi utaongezeka na hivyo kupunguza milipuko ya magonjwa.

(iv)                             Kuongezeka kwa mapato ya Mamlaka mara mbili yatakayosaidia kuimarisha na kustawisha huduma endelevu ya maji kwa wakazi wa Manispaa ya Musoma.

(v)                               Kuimarika kwa huduma ya maji kwenye maeneo yote ya Manispaa ya Musoma na maeneo yaliyokuwa yanapata maji kwa mgao kama vile Buhare, Kigera Rwamlimi, na Bweri.

(vi)                              Muda wa utoaji wa huduma ya majisafi utaongezeka kutoka wastani wa saa 22 kwa siku za sasa hadisaa 24 kwa siku.

Naomba nitoe rai kwa Wananchi wa Manispaa ya Musoma na Mkoa wa Mara kwa ujumla, tuutunze mradi huu na miradi yote inayoendelea kutekelezwa ili iendelee kuwasaidia ninyi na vizazi vijavyo.

Ndugu Wananchi;
Sekta ya Maji kama Sekta nyingine imeendelea kukua kwa kadri ya maendeleo ya nchi yetu kijamii na kiuchumi. Imetoa mchango mkubwa katika ustawi wa jamii zetu mijini na vijijini kwa afya za wananchi na matumizi ya majumbani; maendeleo ya kiuchumi katika kilimo, viwanda, utalii, usafiri na usafirishaji; na kubwa zaidi ni umuhimu wa maji katika utunzaji wa mazingira na hali ya hewa. Maji yana umuhimu mkubwa katika ustawi na maendeleo ya Taifa lolote lile hapa duniani.

Hivi karibuni tumeshuhudia ongezeko kubwa la mahitaji ya maji kwa matumizi ya nyumbani katika miji yetu. Vilevile, sote tunaona  mahitaji makubwa ya maji katika uzalishaji wa chakula; uzalishaji wa bidhaa za viwandani; uzalishaji wa nguvu za umeme kwa kutumia nguvu za maji, na kuongezeka kwa uzalishaji katika nyanja za gesi na mafuta; na matumizi ya rasilimali ya maji katika mazingira. Hii ina maana kwamba matumizi ya rasilimali maji yasiyo endelevu yana athari kubwa kwa mazingira. Hivyo, kuna umuhimu mkubwa wa kutunza mazingira yetu, ili tuendelee kupata huduma endelevu ya maji.

Ndugu Wananchi;
Takwimu zilizopo zinatia hofu; kati ya mwaka 2000 hadi mwaka 2050, mahitaji ya maji kidunia yataongezeka kwaasilimia 55. Hali hii itasababisha kuongezeka kwa migogoro ya matumizi ya maji baina ya watumiaji wa rasilimali za maji. Nitoe rai  kwa Wataalam wa Sekta ya Maji pamoja na Sekta nyingine zinazohusiana, kuhakikisha kuwa wanatafuta suluhisho la upatikanaji wa maji, nishati, na uhakika wa chakula na kuwa na mipango makini, matumizi ya teknolojia sahihi na kubwa zaidi ni ushirikiano wa karibu baina ya wadau mbalimbali wa maji. Na juu ya haya yote, ni msisitizo katika utunzaji endelevu wa mazingira yetu ili yaendelee kutuhifadhi. Aidha, teknolojia za uvunaji wa maji ya mvua na ujenzi wa mabwawa ni maeneo ambayo yatatuhakikishia kwamba tunakuwa na huduma endelevu ya rasilimali ya maji.

Ndugu Wananchi;
Maji ni rasilimali inayotumika sana, na ni msingi wa upatikanaji wa karibu wa kila huduma inayotolewa humu duniani. Katika karne ya 20, idadi ya watu duniani imeongezeka mara nne zaidi wakati mahitaji ya maji yameongezeka mara tisa zaidi. Kasi hii ya ongezeko la matumizi ya maji, pamoja na sababu nyingine imeathiri hali ya upatikanaji wa maji. Mwaka 2014, Jukwaa la Uchumi Duniani liliazimia kuwa uhakika wa upatikanaji wa maji ni moja ya changamoto zinazokuwa kwa kasi duniani. Sisi kama nchi hatuna budi kuwa na mikakati ya makusudi kukabiliana na changamoto hizo, jambo ambalo Serikali imeanza kulifanyia kazi.

Uhaba wa maji na kutopatikana kwake kwa uhakika kunaleta athari mbaya katika shughuli zote za kiuchumi. Utoaji wa huduma ya maji usiosimamiwa ipasavyo na kwa umakini unaleta changamoto kubwa za kiuchumi na kijamii. Hivyo basi, usimamizi mzuri wa rasilimali za maji utakuwa chachu na chanzo cha maendeleo ya haraka ya jamii na Taifa letu. Kwa sababu ya umuhimu wa maji kwa shughuli za kiuchumi za nchi yetu; upungufu au makosa yoyote yatakayofanyika katika mipango, usimamizi na matumizi yanaweza kuwa na athari za muda mrefu kwa jamii na nchi. Hali hii inaweza kwenda mbali zaidi, hata kuziathiri nchi za jirani tunazochangia nazo rasilimali za maji.

Mfano wa karibu ni hapa kwetu Mkoa wa Mara, Mto Mara unaanzia safari yake ya kuingia Ziwa Victoria kutokea nchi jirani ya Kenya; hivyo kama kuna mipango duni, basi athari zake zitaonekana kwenye nchi zote mbili.

Ndugu Wananchi;
Sekta ya Maji inayoratibiwa na Wizara ya Maji bado ina jukumu kubwa la kuhakikisha miji na hasa vijiji vyetu, vinapatiwa huduma ya maji safi na salama na huduma ya usafi wa mazingira katika umbali usiozidi mita 400, ili akinamama na dada zetu waondokane na maisha yenye kuonekana yana suluba. Tusisahau ule msemo wetu, Maji ni Uhai, Usafi wa Mazingira ni Utu na Utunzaji wa Vyanzo vya Maji ni Ustaarabu.

Mabadiliko ya tabianchi kupitia uwepo au uhaba wa maji yanaathiri binadamu, jamii na mazingira. Usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji ulio makini na endelevu ni muhimu katika kukabili athari mbaya za mabadiliko ya hali ya hewa. Isitoshe, maji yana mchango mkubwa katika kukabili mabadiliko ya hali ya hewa, kwani upatikanaji wa uhakika wa rasilimali za maji unapunguza kwa kiasi kikubwa uchafuzi wa hali ya hewa.

Majanga yanayohusiana na maji kama vile, mafuriko na ukame kwa kiwango kikubwa ni maafa yanayojitokeza mara nyingi katika sehemu mbalimbali duniani hivi sasa. Vifo, uharibifu wa mali, makazi na miundombinu vina athari kubwa kwa maendeleo ya mtu mmoja mmoja, kikundi, jamii na hata Taifa. Katika miaka ya hivi karibuni, tumeshuhudia ongezeko la wingi na athari mbaya za majanga haya. Hivyo, kusababisha kuwepo kwa uhaba mkubwa wa rasilimali za maji kwenye baadhi ya maeneo. Kwa mfano, athari zimeshaanza kuonekana katika uzalishaji wa nishati ya umeme katika vinu vya kufua umeme vya Kidatu, Mtera, Hale na Nyumba ya Mungu. Vilevile, kasi ya kupungua kwa maeneo ya misitu yetu kwa hivi sasa ni kubwa.

Ndugu Wananchi;
Hivyo, bila ya kuwa na mipango mikubwa ya pamoja kwa sekta zote ili kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, majanga haya yatazidi kuongezeka. Natoa wito kwa wadau wote kujiunga pamoja katika kukabiliana na athari mbaya za mabadiliko ya hali ya hewa. Kwani, mabadiliko haya yana athari kuanzia kwenye kupungua kwa misitu na vyanzo vya maji; kupungua kwa rasilimali za maji juu na chini ya ardhi; kuathirika kwa ubora wa maji ya kunywa; hadi kukua kwa utoaji wa gesi ya ukaa. Athari hizi zinakwenda mbali kwenye maendeleo ya jamii zetu na Taifa kwa ujumla.

Ndugu Wananchi;
Mwenendo wa mvua kwa kiasi kikubwa unaathiriwa na mabadiliko haya ya hali ya hewa, na wakati huohuo mahitaji ya rasilimali maji yanaongezeka. Kulingana na takwimu za Shirika la Chakula Duniani (FAO) inatarajiwa kwamba ifikapo mwaka 2050, asilimia 60 zaidi ya chakula kitahitajika ili kulisha idadi ya watu watakaoongezeka duniani. Hivi sasa, watu milioni 800 wana lishe duni na wengi wao wanatoka kwenye jamii zenye vipato duni.

Hivyo, wataalam wa sekta zote wana jukumu kubwa la kutumia taaluma zao ili kuwa na matumizi bora ya maji kwa upatikanaji wa mavuno makubwa ya chakula. Hapa nisisitize kwamba matumizi ya njia za kilimo zisizo na tija na ufanisi, zitasababisha matumizi makubwa ya maji. Kwa hiyo basi, kuna umuhimu wa kuandaa sera thabiti na makini katika kushughulikia masuala haya ili matumizi ya maji yafanywe kwa ufanisi.

Ndugu Wananchi;
Serikali yetu itaendeleza juhudi za kuhakikisha tunawafikishia wananchin wetu maji safi na salama katika maeneo ya nchi yetu. Naamini inawezekana kabisa kuongeza huduma ya maji kwenye maeneo ambayo hivi sasa haipo au haitoshelezi mahitaji. Tunajua kuwa ipo changamoto kubwa hasa vijijini lakini kinachohitajika zaidi ni ushirikiano kutoka kwa wadau wetu wote wakiwemo wananchi, Washirika wa Maendeleo, Vyama Visivyo vya Kiserikali na vya Kijamii, na Uongozi wa Serikali katika ngazi zote.

Napenda kusisitiza kuwa dhamana kubwa kwenu wananchi ni kutoa mchango unaostahili katika usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji. Pia, tunalo jukumu kubwa la kutunza vyanzo vya maji popote pale vinapopatikana. Ili kuongeza ufanisi wa kutekeleza mipango yenu, nawashauri mshirikiane kwa karibu zaidi na sekta zote zinazohusiana na Sekta ya Maji; na vilevile, watumiaji wa maji wakubwa na wadogo nchini ili kuepusha migogoro ya kugombea maji.

Ndugu Wananchi;
Mwisho kabisa napenda tena kutoa shukrani kwa Uongozi wa Wizara ya Maji na Mkoa wa Mara kwa kunialika kushiriki nanyi kwenye Kilele cha Maadhimisho ya 27 ya Wiki ya Maji Kitaifa. Napenda pia, kuwashukuru wote walioshiriki kwenye Maonesho ya Wiki ya Maji na kuwapongeza Washindi wa Maonesho hayo. Niwashukuru pia wale wote waliochangia katika kuandaa Maadhimisho ya mwaka huu, ikiwa ni pamoja na Wadau wetu wa Maendeleo.Naipongeza pia Kamati ya Maandalizi kwa kazi yao nzuri iliyohakikisha maadhimisho yanafanyika katika hali ya usalama na amani.

Baada ya kusema hayo, ninayo furaha sasa kutamka kuwa Maadhimisho na Maonesho ya 27 ya Wiki ya Maji Kitaifa yamefungwa rasmi.

ASANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.