Dar es Salaam / Dodoma. Ripoti ya Kamati ya Maliasili, Ardhi na Mazingira iliyowasilishwa jana asubuhi bungeni mjini Dodoma, imewang’oa madarakani mawaziri wanne ambao wizara zao zilishindwa kusimamia vizuri utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili.
Kung’oka kwa mawaziri hao kulitangazwa bungeni jana usiku na Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliyeeleza kuwa Rais Jakaya Kikwete ametengua uteuzi wao baada ya kuwasiliana naye kwa mashauriano akiwa nchini Marekani kwa matibabu.
Mawaziri waliong’olewa kutokana na ripoti ya kamati hiyo iliyoongezewa shinikizo na michango ya wabunge wengi ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamisi Kagasheki, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David Mathayo.
Waziri wa kwanza kutangaza kujiuzulu alikuwa ni Kagasheki huku uamuzi wa mawaziri watatu kujiuzulu ukitangazwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Kagasheki alitangaza kujivua wadhifa huo sa 2:09 usiku alipokuwa akichangia majumuisho ya ripoti ya kamati hiyo iliyowasilishwa na mwenyekiti wa kamati hiyo James Lembeli ambaye ni Mbunge wa Kahama (CCM).
Katika maelezo yake Kagasheki alisema: “…Mimi ni mtu mzima nimesikia hisia nzito sana kwa waliyoyasema wabunge. Rais Kikwete aliponiteua ilikuwa ni kwa furaha yake na operesheni hii, yaliyotokea yametokea hali ya wanyama huko si nzuri;
Mimi mwenyewe nimewasikia na nachukua fursa hii kuteremka ngazi hii ya uwaziri na nitachukua taratibu za kawaida kuijulisha sehemu inayohusika(Rais).
Baada ya Kagasheki kutangaza hatua hiyo, Spika aliwaita mawaziri Dk Nchimbi na Nahodha kuchangia hoja hiyo, hata hivyo hawakuwepo ndipo alipoitwa Dk Mathayo na kutoa maelezo yake.
Katika maelezo yake Dk Mathayo alisema kuwa ripoti hiyo haikumtendea haki kwani kamati ya Lembeli haikumwita kumhoji na kwamba hata ripoti nzima haikueleza kuhusika na kashfa hiyo. Hata hivyo akihitimisha hoja hiyo Lembeli alisema Dk Mathayo ameshindwa kusimamia mapendekezo tisa, yakiwemo matatizo ya wafugaji aliyopewa na Rais Jakaya Kikwete Januari 18, 2006 alipoteuliwa kushika nafasi hiyo.
Akitoa maelezo ya kutenguliwa kwa uteuzi wa mawaziri hao, Waziri Mkuu Pinda alisema: “Niliona nimtafute mkuu wa nchi (Rais Jakaya Kikwete), nilimpa picha yote ya kinachoendelea, alikubali ushauri wa Bunge; ..amekubali kuchukua ya uamuzi wa kutengua uteuzi wao(mawaziri).”
Akihitimisha mjadala huo wa ripoti ya kamati yake, Lembeli alisema: “...Katibu Mkuu na watendaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii nao wawajibishwe kutokana na kuhusika kwao na unyama uliotokea kwenye mpango wa Operesheni Tokomeza Ujangili. Rushwa iliyopo ndani ya wizara hiyo ni kubwa inakusanywa kwa kutumia simu, hivyo Serikali izichunguze simu zao kuanzia leo.”
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.