ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, August 30, 2013

MWILI WA ASKOFU KULOLA KUWASILI JIJINI MWANZA KESHO

Dar es Salaam. Mwili wa Askofu Kulola utasafirishwa kutoka jijini Dar es salaam hadi jijini Mwanza kesho Jumamosi ya tarehe 31/08/2013 majira ya jioni kwa ndege mara baada ya kuagwa katika kanisa la EAGT Temeke. Atazikwa kwenye Uwanja wa Kanisa la EAGT Bugando.

Vilio, simanzi na maombi ya kunena kwa lugha vilitawala jana katika Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT), Temeke Dar es Salaam wakati waumini na ndugu wa Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Dk Moses Kulola (83) walipopata taarifa za kifo cha kiongozi huyo.
Katibu Mkuu wa EAGT, Brown Mwakipesile alisema kuwa Askofu Kulola alifariki dunia jana saa tano asubuhi kwenye Hospitali ya Africa Medical Invesment (AMI), Dar es Salaam.
Mwakipesile alisema afya ya Askofu Kulola ilianza kubadilika Mei mwaka huu akiwa mkoani Mwanza ambako alipelekwa Hospitali ya Rufaa Bugando ambako alibainika kuwa na matatizo ya moyo.
Alisema kifo hicho kimeacha pengo kubwa ambalo haliwezi kuzibwa kwa sasa. Hata hivyo, wanafarijika kwa upande mwingine wakiamini kwamba Mungu amemchukua mtumishi wake kwa wakati alioukusudia.
Askofu Kulola ni mmoja wa viongozi wa dini waliokuwa na jina kubwa nchini na alifanya kazi za utumishi wa kanisa kwa miaka 53 kwa kuhubiri na kuwaombea wenye matatizo mbalimbali.
Mtoto wa kwanza wa askofu huyo, Goodluck Kulola alisema wamejifunza mambo mengi katika maisha ya baba yao, ikiwamo upendo na unyenyekevu ulioongozwa na uchaji Mungu.
Askofu Kulola ameacha mke wake aitwaye Elizabeth, ambaye alibarikiwa kupata naye watoto 10 na wengine wawili wa kuasili. Hata hivyo, watoto watatu walishafariki dunia. Ameacha wajukuu 44 na vitukuu 10.
Askofu Kulola, ambaye alizaliwa 1928, alianza Shule ya Misheni ya Ligsha Sukuma mwaka 1939, baadaye alijiunga na Shule ya Bwiru kabla ya kusomea Usanifu Majengo huko Israel kisha kuanza kazi ya kumtumikia Mungu mwaka 1950.
Alifuzu Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Theolojia katika Chuo Kikuu cha California State Christian Marekani.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.