ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, June 6, 2013

VIJANA WENGI WAJITOKEZA USAJILI AIRTEL RISING STARS

Vijana wengi wajitokeza kwenye usaliji wa  Airtel Rising Stars

USAJILI wa timu za mikoa inayoshiriki mashindano ya soka ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Airtel Rising Stars mwaka huu umekuwa na mwitikio mkubwa miongoni mwa vijana wa umri huo katika mikoa ya Temeke, Ilala, Kinondoni na Tanga.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti makatibu wa mikoa hiyo ambao ndiyo wanaoratibu zoezi hilo la usajili wamesema kuwa vijana wengi wamejitokeza kiasi cha kulazimika kufanya mchujo ili kupata timu sita zinazotakiwa kushiriki Airtel Rising Stars ngazi ya mkoa.

Katibu wa mkoa wa kisoka wa Temeke, Mbarouk Mohamed alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa kumekuwa na mwitikio wa ajabu ambapo zaidi ya timu mia zimejitokeza na kuwalazimu kuanza kufanya mchujo kwa kuzingatia vipaji ili kupata idadi ya timu sita zinazohitajika kushiriki.

“Kwa kweli ni vijana wengi mno wanaotaka kushiriki mashindano haya ya Airtel Rising Stars na tunaamini kuwa kujitokeza kwao kwa wingi kunatupa wigo mpana wa kupata wachezaji wazuri watakao tuwezesha kutetea ubingwa wetu katika fainali za ARS Taifa”

Naye Katibu wa Mkoa wa Ilala, Kanuti Daudi alisema kuwa mchakato usajili unaendelea vizuri na vijana wengi kujitokeza kwenda kujisajili. “Kutokana mwitikio huu tunatarajiza kumaliza usajili mapema kabla ya muda wa mwisho uliowekwa ambao ni Juni 11, 2013”, alisema Daudi.

Kwa upande wake Katibu wa Mkoa wa kisoka wa Kinondoni, Isack Mazwile alisema kuwa wameanza rasmi zoezi la usajili Jumapili iliyopita na kulingana na mwitikio wa vijana wengi wanatarajia kukamilisha zoezi hilo wiki hii. “Tutalazimika kufanya mchujo ili kupata vijana wenye vipaji vya soka wataounda timu sita za mkoa wetu”

Mkoa wa Tanga unaoshirikisha timu za wasichana pekee umeanza kuendesha ligi ambayo ndiyo inayotumika kubaini wachezaji wenye vipaji na hatimaye kuunda timu sita kwa ajili ya Airtel Rising Stars mkoani humo.

“Sisi huku tumeshaanza mchakato wa kutafuta timu kwa upande wa wasichana , na kwakweli nimefurahi kuona mwitikio wa timu umekuwa mkubwa na hapa tunajiandaa kuzichuja ili tuweze kupata timu bora, “ alisema katibu wa soka mkoa wa Tanga Beatrice Shabani.

Mbali na mkoa wa Tanga mikoa mingine inayoshirikisha wasichana pekee ni Kigoma na Ruvuma wakati mikoa ya kisoka ya Kinondoni, Ilala na Temeke inashirikisha wavulana na wasichana huku Morogoro, Mwanza na Mbeya ikijumuisha wavulana pekee.

Mikoa ya Morogoro, Mwanza, Kigoma, Ruvuma na Mbeya pia imeshaanza usajili na inatarajia kukamilisha zoezi hilo kabla ya siku ya mwisho Juni 11.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.