Ngassa AZAM sasa wa Simba |
Na Mahmoud
Zubeiry
MRISHO Khalfan Ngassa
ameuzwa Simba kwa dau la Sh. Milioni 25 mchana wa leo, Azam
imethibitisha.
Habari za ndani kutoka
Azam, ambazo BIN ZUBEIRY imezipata kutoka klabu hiyo, zimesema kwamba
Simba wamelipa fedha hizo na wamesainiwa fomu za uhamisho na sasa Mrisho
anafuata nyayo za baba yake Khalfan Ngassa, ambaye aliichezea Simba SC
1991/1992.
Azam ilifikia uamuzi wa
kumuuza Ngassa, baada ya mchezaji huyo iliyemsajili kutoka Yanga miaka miwili
iliyopita, kubusu jezi ya Yanga baada ya kufunga bao la pili katika Nusu Fainali
ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, dhidi ya AS Vita ya
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Na uamuzi huo, ni wa mzee
Said Salim Bakhresa mwenyewe, ambaye alikerwa na kitendo hicho akawaagiza
wanawe, Wakurugenzi wa bodi ya timu wamuuze mchezaji huyo popote, haraka
iwezekanavyo.
Ngassa alikuwa amebakiza
mwaka mmoja katika mkataba wake aliosaini na Azam FC, akitokea Yanga miaka
miwili iliyoipita kwa dau la Sh. Milioni 55, lakini wasiwasi unakuja kwamba,
Ngassa ana mapenzi na Yanga na kwa Simba kumsajili, kuna hatari yaliyotokea
akiwa Azam, yatajirudia hata akiwa kwa Wekundu wa
Msimbazi.
Mapema leo mchana, Stewart
Hall, kocha Muingereza wa Azam FC jana alifukuzwa katika klabu hiyo kwa kosa la
kukaidi maagizo ya Bodi ya Ukurugenzi ya klabu hiyo, kumpanga Mrisho katika
mechi ya fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la
Kagame.
Habari ambazo BIN
ZUBEIRY ilizipata kutoka ndani ya Azam, zilisema kwamba kikao cha jana cha
pamoja baina ya Bodi ya Ukurugenzi ya Azam FC, Mwanasheria wa kampuni na kocha
Stewart kimeafiki kuvunja ndoa hiyo na sasa Azam FC itakuwa chini ya kocha
kutoka India, Vivek Nagul ambaye alikuwa anafundisha timu ya
vijana.
Habari zinasema kwamba,
mapema baada ya mechi ya Nusu Fainali ya Kagame, kati ya Azam na AS Vita ya DRC,
Stewart aliitwa na kuambiwa asimtumie tena Ngassa kwa kitendo cha mchezaji huyo
kwenda kuibusu na kuivaa jezi ya Yanga, baada ya kufunga bao la
ushindi.
Lakini Stewart katika kikao
hicho, kwanza alimtetea Ngassa kutokana na kufunga bao la ushindi na kumuelezea
kama mchezaji muhimu kwake, lakini msimamo wa bodi ulikuwa ni asipangwe
tena.
Katika fainali, Stewart
alimvalisha jezi Ngassa akamuanzishia benchi, lakini kama ilivyokuwa kwenye Nusu
Fainali alimuingiza kipindi cha pili timu ikiwa nyuma kwa 1-0 na mwisho wa
mchezo ikashinda 2-1 yeye akifunga la pili, dhidi ya Yanga pia alimuingiza timu
ikiwa nyuma kwa 1-0.
Lakini Ngassa alishindwa
kurudia kile alichofanya kwenye mechi na AS Vita na Yanga ikashinda
2-0.
Mbali na Ngassa, kiungo
Salum Abubakar ‘Sure Boy’ pia yuko katika wakati mgumu na jana inadaiwa
alionekana akilia wakati anazungumza na kiongozi mmoja wa Azam, akiuliza ni lipi
kosa lake.
Sure Boy, ambaye ni mtoto
wa kocha wa timu ya vijana ya Yanga, Abubakar Salum ‘Sure Boy’ jana hajafanya
mazoezi na leo pia, naye pia akituhumiwa kucheza kinazi katika mechi dhidi ya
Yanga.
Stewart anakuwa kocha wa
nne ndani ya miaka minne kufukuzwa Azam, tangu Neider dos Santos, Sylvester
Marsh na Itamar Amorin, Mbrazil mwingine. Lakini ni Stewart angalau
anaacha kumbukumbu ya taji na Medali Azam, baada ya kuiwezesha kutwaa Kombe la
Mapinduzi Januari, kushika nafasi ya pili katika Ligi Kuu Aprili, kabla ya
kushika nafasi ya pili Kombe la Urafiki na Kagame mwezi uliopita.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.