ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, January 17, 2012

MAANDALIZI YA KUAGA MWILI WA MAREHEMU MHE. REGIA E MTEMA (MB), TAREHE 17 JAN VIWANJA VYA KARIMJEE NA MAZISHI IFAKARA, KILOMBERO

Spika wa Bunge Mhe. Anne Makinda (Mb) akiongoza kikao cha kamati ya Uongozi kujadili ratiba ya maandalizi ya mazishi ya Mhe. Regia Mtema katika ofisi za Bunge jana. walioko kulia ni Naibu Spika Mhe. Job Ndugai (Mb), Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni Mhe. Freeman Mbowe (Mb) na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge Mhe.William Lukuvi.

Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni Mhe. Freeman Mbowe akifafanua jambo wakati wa kikao cha kamati ya uongozi kilichokaa jana chini ya uenyekiti wa Mhe. Spika kujadili ratiba ya maandalizi ya mazishi ya Mhe. Regia Mtema katika ofisi za Bunge. Kulia ni Mhe. Zaituni Buyogela (Mb) na Mhe. Maua Daftrari. mwenye suti kushoto ni Mhe. William Lukuvi. Picha na Owen Mwandumbya wa Bunge.---
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
YAH: MAANDALIZI YA KUAGA MWILI WA MAREHEMU MHE. REGIA ESTELATUS MTEMA, (MB), TAREHE 17 JANUARI, 2012 KATIKA VIWANJA VYA KARIMJEE NA MAZISHI IFAKARA, KILOMBERO, MOROGORO – TAREHE 18 JANUARI, 2012
UTANGULIZI
Marehemu Mheshimiwa Regia Estelatus Mtema alifariki kwa ajali ya gari katika eneo la Ruvu, mkoani Pwani mnamo majira ya saa 5.30 asubuhi tarehe 14 Januari, 2012. Ofisi ya Bunge baada ya kuthibitisha kifo hicho kupitia Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani na baada ya Kuwasiliana na familia, mara moja ilituma Maafisa Waandamizi kwenda katika Hospitali ya Tumbi mkoani Pwani kuuchukua Mwili wa marehemu na kuuleta Muhimbili kuhifadhiwa ikiwa ni pamoja na kufanya maandalizi ya mazishi. Baada ya maandalizi hayo na kwa ushirikiano na familia na uongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni yafuatayo yamekubaliwa kufanyika:-

MWILI KUAGWA NA FAMILIA TAREHE 16 JANUARI, 2012 KATIKA KANISA KATOLIKI SEGEREA
Familia imeandaa Misa ya Marehemu katika Kanisa Katoliki Segerea siku ya Jumatatu tarehe 16 Januari, 2012 kuanzia saa 9 alasiri mpaka saa 11 jioni. Mwili wa Marehemu utaondoka Hospitali ya Muhimbili saa 7 mchana na baadae kurejeshwa tena kwa hifadhi baada ya Misa.

MWILI KUAGWA RASMI KATIKA VIWANJA VYA KARIMJEE TAREHE 17 JANUARI, 2012
Ofisi ya Bunge imeandaa utaratibu kwa viongozi wa kitaifa, Waheshimiwa Wabunge, Wananchi kuuaga rasmi Mwili wa Marehemu katika viwanja vya Karimjee siku ya Jumanne tarehe 17 Januari, 2012. Shughuli hiyo inatarajiwa kuanza saa 3.00 asubuhi na kuhitimishwa saa 5.30 asubuhi (Ratiba imeambatanishwa kama kiambatisho A). Kama ratiba inavyoonesha, Mwili wa Marehemu utaondoka katika viwanja vya Karimjee saa 5.30 asubuhi mara tu baada ya kuaga katika viwanja vya Karimjee kuelekea Ifakara, Kilombero mkoani Morogoro kwa mazishi.

RATIBA YA MAZISHI YATAKAYOFANYIKA IFAKARA
Ratiba ya tarehe 18 Januari, 2012 ambayo ndio siku ya Mazishi nyumbani kwa Marehemu Ifakara, Kilombero Mkoani Morogoro imepangwa kwa kuzingatia mila na desturi za familia. Ratiba hiyo ni kama ilivyo katika kiambatisho B. Kwa ratiba hiyo, shughuli zimepangwa kuanza saa 5 kamili asubuhi na kukamilika saa 10.30 alasiri.

MAANDALIZI MENGINEYO
Mpaka hivi sasa familia imearifu kuwa Msiba huo umepokelewa kwa hisia kubwa katika eneo alilozaliwa Marehemu Mheshimiwa Regia Estelatus Mtema na kwamba tujiandae kwa ushiriki kwa wakazi wa Kilombero takriban 1000. Aidha, Ofisi inaendelea na Maandalizi ikiwa imejiandaa kwa ushiriki wa viongozi wa kitaifa Mkoani Morogoro.

SHUGHULI ZA KAMATI ZA BUNGE SIKU YA JUMANNE TAREHE 17 JANUARI, 2012
Kutokana na uzito wa tukio hili, Ofisi ya Bunge inapenda kuutangazia Umma kuwa shughuli za Kamati za Bunge kwa jumanne tarehe 17 Janauari, 2012 ambazo zinafanyika katika Ofisi ya Bunge , Dar es Salaam, zitasitishwa hadi jumatano tarehe 18, Januari, 2012

Ofisi ya Bunge inaungana na familia ya marehemu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi. Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu Mhe. Regia Estelatus Mtema, (MB) mahali pema peponi. Amina.

Imetolewa na,
Idara ya Habari, Elimu kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa
DAR ES SALAAM
16 Januari, 2012

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.