MCHUNGAJI Ambilikile Mwasapile amesema hivi karibuni atahamisha utoaji wa tiba katika eneo analoishi sasa na kwenda sehemu ambayo itakuwa na nafasi kubwa zaidi, kwa lengo la kupanua huduma na kubadilisha mazingira anayoishi.
Akizungumza juzi mchana kijini hapo, mchungaji huyo alisema yeye si mganga wa kienyeji, bali anatibu kwa miujiza ya Mungu na kusisitiza kwamba ili mgonjwa apone anatakiwa kuwa na imani katika huduma hiyo.
“Kwa wale wanaoumwa Ukimwi wanapokunywa dawa hii wanapona kabisa. Tiba itaanza kujidhihirisha ndani ya siku saba. Lakini wadudu hata kama bado watakuwapo, hawatakuwa na nguvu na katika kipindi cha miezi mitatu, wadudu wote watakufa kabisa.
Kwa wale wenye kansa, dawa inamaliza kabisa tatizo hilo, dawa hii inaponya kichaa, kifafa na magonjwa mengine ambayo mgonjwa atataka apone."Idadi ya wagonjwa wanaomiminika kwa Mchungaji Mwasapile inazidi kuongezeka siku hadi siku.
Wengi wanailalamikia Serikali kwa kushindwa kumsaidia mchungaji huyo kuboresha mazingira ya utendaji kazi wake. Mmoja wa wagonjwa waliokuwa wakisubiri tiba hiyo, Sara Ibrahim alisema: "Huduma ni nzuri lakini hakuna ulinzi wa maana. Hakuna 'ambulance' (gari la wagonjwa), watu wanafia kwenye magari kwa kukosa msaada wa karibu kuwafikisha kwa mchungaji. Tunaiomba Serikali isaidie huduma hiyo pia kwa kujenga vyoo, kusambaza maji na kutoa jenereta."
Licha ya malalamiko hayo, barabara ya kufika huko inazidi kuharibika na kusababisha mamia ya wagonjwa na jamaa zao kukwama porini. Zaidi ya abiria 600 waliokuwa wanatoka Arusha kwenda huko wamekwama umbali wa kilometa 306 kutokana na ubovu huo.
Barabara ya Arusha kwenda Loliondo, hasa katika Kijiji cha Samunge anakofanyia matibabu mchungaji huyo itaendelea kuwa mbaya kiasi cha kukosa mawasiliano kabisa katika siku za hivi karibuni kama hakutakuwa na jitihada za kuitengeneza.
Mmoja wa wagonjwa, Anna Ibrahim alisema: "Kila gari linalofika Samunge linatozwa Sh2,000 lakini barabara bado ni mbovu na hatujui fedha hizo zinakwenda wapi? Serikali inatakiwa itumie kodi yetu kutuletea maendeleo,” alisema. Hadi kufikia juzi, idadi ya magari yanayopeleka wagonjwa kwa Mchungaji Mwasapile yanakadiriwa kufikia 40,000.
Akizungumzia ongezeko hilo la wagonjwa wanaokwenda kwake kupata tiba, Mchungaji Mwasapile alisema hiyo ni sehemu tu ya watu watakaotoka maeneo mbalimbali duniani kuifuata huduma hiyo kwake... "Watu wataendelea kufurika hapa kutoka kila pembe ya dunia na maajabu ya Mungu yataendelea kujionyesha."
KWA HISANI YA www.mwananchi.co.tz
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.