ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, April 10, 2024

VIONGOZI NA WANACHAMA WA CCM KATA YA MSANGANI WAMFAGILIA MWENYEKITI NYAMKA

 


NA VICTOR MASANGU,KIBAHA


BAADHI ya wanachama na viongozi wa chama cha mapinduzi na wananchi wa  Kata ya Msangani wamempongeza kwa dhati Mwenyekiti wa CCM Kibaha mji Mwajuma Nyamka kwa upendo wake wa kuwakutanisha kwa pamoja katika kusherekea sikukuu ya Iddy mosi nyumbani kwake.

Baadhi ya viongozi hao akiwemo Diwani mteule wa kata ya Kata ya Msangani Gunze Yohana ambaye amechaguliwa hivi karibuni kwa kishindo cha asilimia 99.20.

Gunze aliongeza kuwa amefanya jambo la upendo la kuamua kuwakutanisha baadhi ya wanachama,viongozi na wananchi ili kuweza kujumuika katika chakula cha mchana  katika kusherekea sikukuu ya Iddy mosi.

"Kiukweli Mwenyekiti wetu wa chama ameonyesha upendo maana kitendo tu cha kutukutanisha nyumbani kwake  sisi kiukweli tumefarijika na Mungu ambariki kwa moyo wake wa kujitolea ,"alisema Gunze.

Naye balozi wa mtaa wa Kidenge Said Mbunju alisema kwamba Mwenyekiti Nyamka amekuwa mstari wa mbele katika kushirikiana na jamii na kwamba amefarijika sana kushiriki chakula cha mchana nyumbani kwa Mwenyekiti.

"Nafahamu leo hii ni sikukuu lakini sisi tumekuja kwa niaba ya wengine lakini nipende kuchukua fursa hii kumshukuru kwa moyo wangu wote maana tumeweza kukutana na kubadilishana mawazo mbali mbali ",alisema Said.

Mjumbe huyo alisema katika sikukuu watu wengi wamekuwa wakikutana na ndugu zao lakini kwa upendo wa Mwenyekiti akaona akutane na jamii ili kuweza kula chakula cha mchana sambamba na kubadilishana mawazo.

Kwa upande wake Mwenyekiti huyo wa CCM Kibaha mji aliwahimiza viongozi na wanachama wa ccm kuhakikisha wanakuwa na umoja na upendo kipindi chote.

Nyamka alisema kwamba anatambua kwamba katika siku za siku kuu kila mtu anakuwa na majukumu mengi lakini akaona awashirikishe baadhi ya watu ili aweze kujumuika nao katika chakula cha mchana.

 "Mimi kiukweli nawashukuru wale wote ambao baadhi yao niliwaomba tujumuike kwa pamoja na wote mimi ninawapenda japo niliita baadhi tu kwa niaba ya wengine Mungu awabariki sana,"alisema Nyamka.

Kadhalika Nyamka pamoja na kuwapongeza aliwakumbusha viongozi na wana ccm kwa ujumla  umuhimu wa kuhakikisha kwamba wanajipanga vizuri katika kuelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani.

Mwenyekiti huyo wa CCM Kibaha mji ametumia sikukuu ya Iddy mosi kuwakaribisha baadhi ya viongozi wa ccm,wanachama na wananchi lengo ikiwa ni kula chakula cha mchana pamoja na kubadilishana mawazo.

Barrick yakabidhi msaada wa vifaa vya kisasa vya kupima ulevi wa madereva kwa Jeshi la Polisi

Meneja Mawasiliano (Corporate Communication and Country Liaison Manager) wa Barrick, Georgia Mutagahywa (wa pili kutoka kushoto) akimkabidhi moja ya vifaa vya kisasa vya kupima ulevi kwa madereva vilivyotolewa na Barrick kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama barabarani kanda maalum ya Dar es Salaam, Mohamed Bahashwan, katika hafla ya kukabidhi msaada wa vifaa hivyo kwa Jeshi la Polisi iliyofanyika katika Kituo cha Oysterbay jijini Dar es Salaam , wengine pichani ni Kamanda wa Polisi wa Kinondoni SACP Mtatiro Kitinkwi (kushoto) na Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani wa Dar es Salaam SACP William Mkonda.

Na Mwandishi Wetu.

Katika kuendeleza mkakati wa kuhamasisha jamii kuzingatia usalama wakati wote, kampuni ya Barrick kupitia kampeni yake ya ‘Journey to Zero’ imekabidhi Jeshi la Polisi msaada wa vifaa vya kupima ulevi kwa madereva wa vyombo vya moto vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 100 katika hafla iliyofanyika katika kituo cha polisi cha Oysterbay kilichopo wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Akiongea katika hafla ya kupokea vifaa hivyo,Kamanda wa Polisi wa kanda ya Kinondoni, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Mtatiro Kitinkwi,alisema msaada huyo wa vifaa vya kisasa vya kupima kilevi umetolewa kwa wakati mwafaka ambao Jeshi hilo linaendelea na mikakati ya kukomesha vitendo vya ulevi kwa madereva wanaoendesha vyombo vya moto ambao umekuwa ni chanzo kikubwa cha ajali nyingi za barabarani zinazotokea nchini.

“Tunawashukuru Barrick kwa kuendelea kuwa wadau wakuu wa kusaidia kampeni za ualama barabarani nchini na sisi tunawahodi kuwa vifaa hivi tutavitumia vizuri ili vifanikishe lengo lililokusudiwa la udhibiti wa madereva kutumia vinywaji vyenye kilevi kupita kiasi”.alisema Kitinkwi.

Alisema Jeshi la Polisi kupitia kikosi chake cha Ualama Barabarani pia litaendelea kutoa elimu ya unywaji kistaarabu kwa madereva wa vyombo vya moto ili kuhakikisha ajali nyingi zinazotokana na ulevi zinatokomezwa nchini na alitoa wito kwa wadau mbalimbali kuunga mkono jitihada hizi kwa kuwa suala la usalala linamgusa kila mwananchi.

Kwa upande wake Meneja Mawasiliano (Corporate Communications and Country Liaison Manager) wa Barrick, Georgia Mutagahywa, alisema kuwa msaada huo ni mwendelezo wa kampeni ya Barrick ya Journey to zero ambayo inalenga kuhamasisha afya na usalama kwa wafanyakazi wake na wadau wengine wote kwenye jamii.

“Kampeni yetu ya 'Journey to Zero' inalenga kuhakikisha wafanykazi wote wa kampuni wanakuwa salama wakati wote wanapokuwa kazini hadi wanaporudi nyumbani hivyo tumehakikisha kampeni hii inavuka mipaka hadi nje ya kampuni kuhakikisha jamii nzima inakuwa salama na ndio maana tunaendelea kuunga mkono Serikali kupitia Jeshi la Polisi kupambana na changamoto ya ajali za barabarani.

Mutagahywa alisema Barrick, siku zote itaendelea kuwa mstari wa mbele kushirikiana na wadau mbalimbali kuunga mkono kampeni hizi za usalama barabarani na inaamini vifaa hivi vya kisasa vya kupima kilevi vilivyokabidhiwa kwa Jeshi la Polisi vitasaidia kuwabaini madereva wanaoendesha vyombo vya moto wakiwa wamelewa na kuchukuliwa hatua za kisheria ili kudhibiti na kupunguza matukio ya ajali za barabarani.

Naye Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Kamati za Usalama barabarani nchini, Idd Azzan, aliishukuru Barrick, kwa kutoa msaada huo na kwa kuwa mdau mkuu wa kusaidia kampeni ya usalama , alitoa rai kwa watumiaji wa vifaa hivyo kuvitunza vizuri ili kuweza kufanikisha malengo mazuri yaliyokusudiwa sambamba na kuwarahisishia kazi, “Katika dunia ya sasa ya matumizi ya teknolojia nina imani vifaa hivi vitarahisisha kazi ya polisi wetu kuwanasa madereva walevi” alisisitiza.
Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Kamati za Usalama barabarani nchini, Idd Azzan akiongea katika hafla hiyo.
Maofisa mbalimbali waandamizi wa Jeshi la Polisi wakifuatilia matukio katika hafla hiyo
Maofisa mbalimbali waandamizi wa Jeshi la Polisi walipata fursa ya kuongea katika hafla hiyo.
Viongozi wa kamati za usalama barabarani, Jeshi la Polisi na Barrick walipata fursa ya kupiga picha ya pamoja na wageni waliohudhuria katika hafla hiyo.

RC BATILDA –TANGA TUMEPOKEA ZAIDI YA TRILIONI 2 ZA MIRADI YA MAENDELEO

 

 


MKUU wa Mkoa wa Tanga Balozi Batilda Burian akiwa kwenye futari iliyoandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Pangani (CCM) na Waziri wa Maji 
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga Rajab Abdurhamani akizungumza katika halfa hiyo 
WAZIRI wa Maji Jumaa Aweso akitunzwa baada ya kusoma Quarn Tukufu katika halfa hiyo 




Na Oscar Assenga, PANGANI.

MKUU wa Mkoa wa Tanga Balozi Batilda Burian amesema katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais Dkt Samia Suluhu mkoa huo umepokea fedha kiasi cha Sh.Trilioni 2.6 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Balozi Batilda aliyasema hayo wakati wa Dua Maalumu ya Kumuombea Rais Dkt Samia Suluhu iliyokwenda sambamba na Futari iliyoandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Pangani (CCM) na Waziri wa Maji Jumaa Aweso iliyofanyika wilayani Pangani.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo wa Serikali,Chama na Taasisi mbalimbali akiwemo Naibu Waziri wa maji Mhandisi Mathew Kundo, Katibu Mkuu Wizara ya Maji,Mkurugenzi wa Ruwasa na wataalamu mwengine.

Mkuu huyo wa Mkoa alisema fedha hizo zimeelekezwa kwenye miradi ya maendeleo likiwemo Daraja la Mto Pangani na Barabara ya Pangani pamoja na mengine ikiwemo ya elimu ambapo wanamshukuru Rais kwa ujenzi wa mabweni ya watoto wenye mahitaji maalumu yamejengwa,zahanati,nyumba za walimu na miradi ipo mingi kazi kubwa imefanywa.

“Katika hili tunamshukuru sana Mh Rais Dkt Samia Suluhu kwa kutuletea fedha hizi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo lakini namshukuru kwa imani kubwa kwangu ninahaidi sitamuangusha nitajitahidi kwa ushirikiano wenu na dua zengu niweze kutimiza yale ambayo anakusudia nitimize nikiwa hapa Tanga”Alisema RC Balozi Batilda

Alisema kwamba wataendelea kuhakkikisha fedha zinazokuja zinatekeleza kazi iliyokusudiwa na sio vyenginevyo pamoja na usimamizi mzuri katika miradi inayotekeleza ili iweze kuleta tija inayotakiwa.

“Nimshukuru Waziri Aweso amefanya jambo kubwa na ameendelea kufanya mambo mengi kwenye Sekta ya Maji nimetoka Tabora kwenye miradi 28 nasi tulikuwa tunanufaika nimekuja hapa Tanga nimeambiwa napo ipo ni kijana mdogo lakini mwenye hekima,hofu ya mungu ,mchapakazi “Alisema RC Balozi Batilda.

Alisema kwa hakika dhamana aliyopewa na Rais Dkt Samia Suluhu kuhakikisha anawatua wakina mama ndoo kichwani ameitekeleza vizuri kwa kushirikiana na wataalamu wa wizara maji wanaendelea na kazi nzuri.

Akizungumzia suala la mabadiliko ya tabia ya nchi hasa kwenye wilaya ya Pangani RC Balozi Batilda alisema wilaya hiyo ni moja ya maeneo yaliyoathirika na kuna maeneo yakichimbwa visima kuna maji ya chumvi ndio maana kwenye mradi wa maji ya miji 28 na wao wamepelekewa na maeneo watachimba visima ili wananchi waweze kunufaika kwa kupata maji safi na salama.

Akizungumzia suala la uvuvi RC huyo alisema suala hilo katika mkoa huo ni moja ya maeneo ya uvuvi hivyo suala la maboti na vifaa vya uvuvi vitaendelea kupatikana kwenye mji wa Pangani na maeneo mengine.

“Tunapozungumzia masuala ya mazingira niwape kongole Pangani mazingira mmeendelea kuyatuza na msitu wenu wa asili unapendeleza”Alisema

Mkuu huyo wa mkoa alisema katika moja ya kuendeleza ukwekezaji Serikali kupitia Wizara Madini ilisaini mkataba na wawekezaji wa madini ya Ndovu au tembo ambayo yatachimbwa kwenye Mwambao wa Pangani karibu kilomita 15 ya ufukwe.

Alisema walichowaambia wahakikisha hawawanyi ruhusu ya wavuvi kutumia mwambao huo na matumbawe hayatavurugwa ikiwemo mikoko iliyopo wakati wanaendelea kunufaika na mradi huo na kuendelea na uvuvi,matango pori yote kuhakikisha wanakuwa na shughuli mbalimbali zinaendelea.

Hata hivyo Mkuu huyo wa mkoa alisema mkoa wa Tanga ndio ambao kila kitu kinaweza kuota hivyo lazima wahakikishe utajiri huo unawanufaisha wananchi wao wote kwa kuhakikisha wanachangamkia fursa zilizopo.

“Katika ujenzi wa bomba la mafuta litapita kwenye wilaya kadhaa tunataka wana tanga wanufaike na miradi hiyo na kazi yake katiba tawala na wakuu wa wilaya na makatibu tawala ni kuwawezesha wananchu kuona fursa za uwepo wa mradi huo ili waweze kuchangamkia fursa hizo”Alisema RC Balozi Batilda ,

Awali akizungumza katika futari hiyo Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Kundo Mathew alisema kwamba maadili mema ambayo tumeyaonyesha katika kipindi cha mwezi mtukufu wa ramadhani tuendelee kuifanya na kufanya ibada ndio tunaweza kuwaponya wengi na kujiponya na sisi.

Mhandisi Mathew alisema pia waendelee kumuombea Rais Dkt Samia Suluhu ili aendelea kuifanya kazi nzuri anaoendelea kuifanya na kuhakikisha wanashirikiana na Mbunge wao na kamwe wasimwangushe .

“Nataka kuwaambie wana Pangani “Dhahabu ya Pangani tunaijua wana Pangani na Dhahabu ya Tanzania tunaijua na tusije kudanganyika na kuachia dharabu hii na kwenda kuokota mawe”Alisema

Hata hivyo alimshukuru Waziri Aweso kwa jambo kubwa alilolifanya kwa wananchi wake kutokana na uwepo wa umoja na mshikamano kwa wananchi wake ambao wameitika kwa wingi kwenye tukio hilo.

Naye kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga Rajab Abdurhaman alisema safari ya kuifungua pangani kimaendeleo itafanywa na wana Pangani wenyewe na mimi ni miongoni mwa watu walishawishika na Waziri Aweso kipindi kile kwa maneno yake kwa dhamira iliyojificha ndani ya moyo wake akanitamkia ya kutaka kuwatumikia wananchi wa Jimbo hilo.

Alisema kwa sasa tunayaona maendeleo makubwa sana kwenye Jimbo la Pangani ikiwemo ujenzi wa barabara ya Tanga-Pangani –Saadani ambayo itaifungua wilaya hiyo pamoja na uwepo wa miradi ya maji ambayo awali wananchi walikuwa wakiifuata umbali mrefu.

Tuesday, April 9, 2024

KINANA, RC KUNENGE WAFIKA RUFIJI KUWAFARIJI WANANCHI WALIOPATWA NA MAFURIKO


VICTOR MASANGU,
RUFIJI

Wananchi wa wilaya ya Rufiji kata  chumbi A na kata ya Muhoro Mkoa wa Pwani  wamehakikishiwa kupatiwa misaada ya haraka kulingana na mahitaji ambayo wanatakiwa kupatiwa kwa kipindi hiki ambacho wameathirika kutokana na janga la mafuriko. 


Kinana ameyasema hayo leo 9 , 04 ,2024 Mhe . Abdulirahmani Kinana wakati alipoenda kutoa pole kwa waathirika hao pamoja na kutoa salamu za Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassani kwa wananchi wote ambapo ameahidi kuwa ataagiza kila kinachowezekana kifanyike ili wananchi wasiendelee kuathirika .


Pia Mhe . kinana amesema kuwa nae Waziri mkuu Kassim Majaliwa tayali anashughulikia swala hilo ambapo mpaka kufikia kesho baadhi  ya vifaa vitakua vimeshafika lakini kwasasa miongoni mwa vifaa vilivyopo ni pamoja na blanketi , magodoro , mahema na vyakula ila havitoshelezi kwa wahanga hao .


 Aidha  Makamu mwenyekiti Kinana ametumia nafasi hiyo kuwapongeza viongozi wawili ambao ni mbunge wa jimbo la ikwiriri pamoja na mbunge wa jimbo la kibiti kwakua na ushirikiano kwa wananchi wake wanaowaongoza . 


 Nae Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe . Abubakar Kunenge amesema kuwa Maeneo ambayo yaliopatwa na  athari ni jumla ya ekali elfu 34 ,na  wananchi waliopata athari ni takribani kaya elfu 33 na jumla ya idadi yao ni elfu 88 lakini pia katika wilaya hiyo ya chumbi vifo vilivyopatikana ni wiwili ambavyo ni mama pamoja na mtoto .


Sambamba na hilo Mhe. kunenge ameomba kuwa miongoni mwa misaada ambayo itatolewa kwa wahanga  iweze kuwafikia kwa wakati  walengwa wote wenye uhitaji wa misaada hiyo .








WATANZANIA WATAKIWA KUIENZI NA KUITUNZA AMANI ILIYOPO NCHINI

 

 


Mchungaji wa Kanisa la Waadventista Wasabato Korogwe Julius Mbwambo akizungumza wakati wa halfa ya Futari iliyoandaliwa na Kanisa hilo kwa makundi maalumu yaliyopo kwenye hali ya chini na kufanyika katika Stendi ya Kijazi wilayani Korogwe mkoani Tanga




Na Oscar Assenga,KOROGWE.

WATANZANIA wametakiwa kuienzi amani iliyopo hapa nchini ambayo ni tunu kubwa iliyoacha na waasisi wa Taifa hili na wasikubali kamwe ichezewe kutokana na kwamba kufanya hivyo itaondoa umoja wetu ambao ni chachu ya maendeleo.

Wito huo ulitolewa na Mchungaji wa Kanisa la Waadventista Wasabato Korogwe Julius Mbwambo wakati wa halfa ya Futari iliyoandaliwa na Kanisa hilo kwa makundi maalumu yaliyopo kwenye hali ya chini na kufanyika katika Stendi ya Kijazi wilayani Korogwe mkoani Tanga

Alisema wao kama Kanisa wanatambua kwamba amani ni kitu muhimu sana kwa ustawi wa jambo lolote lile hivyo ni lazima itunze na iendelee kuenziwa na ndio maana wameona mwezi Mtukufu wa Ramadhani kufuturisha kutokana na umoja uliopo na kwamba wao ni ndugu moja.

Futari hiyo iliandaliwa na Kanisa hilo na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali ambapo ililenga makundi ya Makondakta,Waendesha bajaji,Wajasiriamali ,Wamachinga ambapo pia viongozi wengine wa kiserikali nao walishiriki lengo likiwa ni kuhimiza umoja na kudhimisha amani.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa futari hiyo Mchungaji wa Kanisa hilo Mbwambo alisema kwamba wao kama viongozi wa dini ni kuonyesha umma kwamba katika suala la mungu ni lazima kuwe na umoja na mshikamano kutokana na kwamba wao ni wametoka kwa baba mmoja.

“Futari hii ni kuonyesha umoja sisi kama kanisa na tunaendelea kusisitiza mshikamano na amani kwa sababu hivyo ndio vitu muhimu kwa ustawi wa jamii yoyote ile hivyo tuendelee kuitunza na kuienzi na tusiwafumbie macho wale ambao watakaojaribu kuichezea”Alisema

Hata hivyo alitoa wito kwa taasisi na watu wenye uwezo kuona namna ya kuwasaidia wahitaji wanapokuwa kwenye mwezi mtufuku wa ramadhani kuhakikisha wanayagusa makundi yaliyokuwa kwenye hali ya chini.

Monday, April 8, 2024

RWANDA YAADHIMISHA MIAKA 30 YA MAUAJI YA KIMBARI

 


TAIFA la Rwanda limeadhimisha miaka 30 tangu yafanyike mauaji ya kimbari dhidi ya jamii ya Watutsi na Wahutu, ambayo yalichukua uhai wa watu takribani 800,000 ikiwa ni tukio baya zaidi la mauaji ya karne ya 20 yaliyowahi kushuhudiwa katika bara la Afrika.


Wakati wa maadhimisho hayo yaliyofanyika jana Rais wa Rwanda Paul Kagame, aliwasha mwenge ikiwa ni ishara ya kuwakumbuka wahanga wa mauaji hayo kwenye eneo la kumbukumbu ya mauaji ya kimbari katika mji wa Kigali.

Mauaji hayo yalitokea Aprili 7 mwaka 1994 na kwamba zaidi ya wahanga 250,000 wanaaminika walizikwa katika eneo hilo la kumbukumbu.


Bendi ya jeshi ilipiga nyimbo za huzuni, wakati Rais Kagame alipoweka mashada ya maua kwenye makaburi ya halaiki, akiwa amezungukwa na viongozi wa kigeni wakiwemo wakuu kadhaa wa nchi za Afrika na aliyekuwa Rais wa Marekani wakati wa mauaji hayo Bill Clinton.

MKUU WA MKOA WA LINDI ASISITIZA UBORA WA MIRADI KUELEKEA MBIO ZA MWENGE.

 

Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack amewataka wakurugenzi na waratibu wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kuzingatia ubora wa miradi itakayopitiwa katika Halmashauri za Mkoa wa Lindi.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack amewataka wakurugenzi na waratibu wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kuzingatia ubora wa miradi itakayopitiwa katika Halmashauri za Mkoa wa Lindi.
Na Fredy Mgunda, Lindi.

Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack amewataka wakurugenzi na waratibu wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kuzingatia ubora wa miradi itakayopitiwa katika Halmashauri za Mkoa wa Lindi.


Mhe. Telack ameyasema hayo jana jumamosi tarehe 06 Mei 2024 kwenye kikao cha pili cha maandalizi ya mbio za Mwenge zinazotarajiwa kukimbizwa Mkoa wa Lindi mwezi Mei mwaka huu 2024.


Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Telack amesema kuwa miradi yote itakayochaguliwa kupitiwa na Mwenge wa Uhuru ni lazima iwe na ubora wa viwango vya kuridhisha ikiwemo uhalisia wa fedha iliyotumika.


Ameongeza kuwa pamoja na kuzingatia ubora wa miradi hiyo lakini pia uwepo Wahandisi ujenzi waliosimamia miradi hiyo ni muhimu hasa kwenye ufafanuzi wa taarifa za mradi husika kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru.


Mhe. Telack amewasisitiza Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha uandaaji wa miradi hiyo unazingatia maelekezo yote ya Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2024 ikiwemo ujumbe wake unaolenga utunzaji wa Mazingira.

Sunday, April 7, 2024

TTCL KUJA NA INTERNET YENYE KASI ZAIDI YAFICHUA SIRI WAKATI WA KUFUTURISHHA JIJINI MWANZA

 

NA ALBERT G.SENGO/MWANZA
"TTCL tunataka kuleta uhuru wakuweza kutumia WIFE yenye nguvu na kasi, bila kila mtu kwenye familia kulazimika kuwa na bando lake, na hiyo ni katika kutimiza ahadi aliyoitoa Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa wananchi wake kwamba 'Mawasiliano ni haki ya kila Mtanzania' " amesema Zuhura Muro, Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL, katika Hotel ya Malaika wakati wa kufuturisha wakazi wa jiji la Mwanza. Haya yanajiri wakati Serikali ikiwa tayari meanza mradi wa ujenzi wa minara mipya 758 kwa ajili ya kupanua wigo wa mawasiliano (coverage) itakayowanufaisha watanzania zaidi ya milioni 8 nchini na kupunguza gharama za kuweka mkongo kwenye hifadhi za barabara. #ttcl #samiasuluhuhassan #mwanza #jembefm

Friday, April 5, 2024

SIMBA AU YANGA NANI KULIHESHIMISHA TAIFA HII LEO

 NA ALBERT G. SENGO/MWANZA

Hizi hapa tambo za mashabiki wa soka toka jijini Mwanza wa timu zilizoishangaza Afrika, Simba na Yanga kwa kuwa timu mbili kutoka taifa moja Tanzana kutinga hatua ya Robo fainali na sasa zikiwa katika safari kuelekea michezo yao ya marudiano kuwania nafasi ya kutinga nusu fainali Klabu Bingwa Barani Afrika. Swali jeh ni nani atakaye liheshimisha Taifa hilo lililopo Afrika Mashariki, ni Simba au Yanga au pengine wababe wote hao? ........................ KWA UPANDE WA UFUNDI. KOCHA Mualgeria wa Simba SC, Abdelhak Benchika amesema kwamba mchezo wa kesho dhidi ya wenyeji, Al Ahly Jijini Cairo utakuwa mgumu, lakini wamejipanga kuwakabili mabingwa wa Afrika. Akizungumza katika mkutano na Waandishi wa Habari mapema jana Alhamisi Jijini Cairo, Benchika amesema kwamba hawapo Misri kwa ajili ya kufungwa, bali kushindana na hawahofii chochote. Kwa upande wa pili Yanga Africans, kocha wake Muargentina Miguel Angel Gamondi amesema kwamba leo anaweza kumpata mchezaji mmoja tu kati ya wanne aliowakosa kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini. Waliokosekana kwenye mchezo wa kwanza wa nyumbani ni mabeki Kibwana Shomari, Kouassi Attohoula Yao (Ivory Coast)na viungo Peadoh Pacome Zouazoua (Ivory Coast) na Khalid Aucho (Uganda.

Thursday, April 4, 2024

PAULMAKONDA AKIAPISHWA IKULU AKIANDIKA HISTORIA MPYA

 MAKONDA AANDIKA HISTORIA MPYA UENEZICCM

- Ni kuwa Mwenezi aliyehudumu muda mfupi kuliko wenezi wote tangu CCM iundwe - licha ya mbwembwe na sarakasi zake amedumu kwa miezi mitano na wiki moja tu kitini, muda mchache kuliko Shaka aliyekaa miaka miwili kasoro na Sofia Mjema aliyekaa miezi kumi kwa awamu ya sita - kuondolewa kwake kwaibua mijadala wengi wakimpongeza Rais Dkt Samia kuendelea kuisuka vyema sektetarieti ya CCM na kuimarisha Serikali - wengine wasema hawakutaraji kama angefika hata miezi miwili kwenye kiti hicho kutokana na kauli na matendo yake - Kibarua kigumu kwa mrithi wake Akitarajiwa kutekeleza hasa shughuli za kikatiba za mwenezi badala ya kujikita kwenye maigizo mfano wa sinema za kihindi kama kwa mtangulizi wake "Idara ya Itikadi na Uenezi ni kitengo nyeti na muhimu ndani ya CCM...Miongoni mwa majukumu ya idara hiyo ni kushughulikia na kueneza masuala ya itikadi na Sera za CCM, kupanga na kusimamia mafunzo na maandalizi ya makada na wanachama na kusimamia vyombo vya habari vya chama, mawasiliano na uhamasishaji wa umma. sio kitengo cha maigizo, majigambo na ngonjera za kupanda mara farasi mara sijui trekta. Itikadi ni maarifa itikadi ni maoni, anahitajika mtu atakaelewa hilo sio ujanjaujanja" Mjumbe wa NEC, jina kapuni Na. Mwandishi wetu, Katika hali isiyo ya kawaida wanachama wa chama cha mapinduzi (CCM) wamejikuta wakishangilia kuenguliwa kwa aliyekuwa katibu wa itikadi na uenezi wa chama hicho Paul Christian Makonda na kuteuliwa kuwa mkuu wa mkoa wa Arusha. Makonda ambaye alitangazwa kuwa Mwenezi wa CCM Oktoba 22 mwaka jana 2023 akichukua nafasi ya Sophia mjema aliyekalia kiti hicho tangu Januari mwaka huo ambaye pia alichukua kiti hicho kutoka kwa Shaka Hamdu Shaka aliyepokea kijiti kutoka kwa Polepole alisifika kwa mbwembwe na sarakasi nyingi katika kipindi chake cha miezi mitano na wiki moja ya uenezi wake tofauti na malengo ya uwepo wa nafasi hiyo nyeti ndani ya chama hicho Katika hali isiyokuwa ya kawaida mwenezi huyo 'aliyerumbuliwa ni kama alipagawa hivi kuona ameteuliwa kuhudumu kiti hicho na kuanza kuropoka ropoka katika kila alipopanda jukwaani bila kujali aina ya hadhira "Miongoni mwa vituko vya ajabu kufanywa na mwenezi wetu huyu kwa kweli ni kutufundisha ujinga watanzania, yaani ametuambia tusiende mahakamani tukipata changamoto sasa tusipoenda mahakamani si tutauana kweli vijijini huko. Kiongozi anayetamba kukagua utekelezaji wa ilani hawezi kuropoka kijinga namna hii". Anasema Salum Kabambe mwanachama wa CCM Alipoulizwa kutoa maoni yake na gazeti hili mmoja wa wajumbe wa halimashauri kuu ya chama hicho (jina kapuni) juu ya uongozi wa makonda na kutolewa kwake alisema kuwa ameshangaa imekuwaje ameweza kufikisha hadi miezi mitano kwa kuwa siku ya kwanza tu alipozungumza na wanachama pale Lumumba alimuona kuwa hawezi kudumu kitini humo akiamini bado ana mawenge "Kwa kweli hata kumthibitisha ni kwa sababu tu tunampenda mheshimiwa Rais na kumheshimu, hivyo isingekuwa vyema kumkatalia pendekezo la huyu bwana kuwa mwenezi, wengi wetu tulijua hawezi hii nafasi". Amesema MNEC huyo "Kwa asili Mwenezi wa CCM anapaswa kuwa mtu mwenye maarifa, anayeweza kuunganisha wenzake, anayeweza kujifunza ili akafundiashe wengine, ndiye mtangazaji mkuu wa itikadi ya chama chetu, kwa hiyo ndio muuzaji hasa wa sura na roho ya CCM lazima mtu huyo asiwe mropokaji kama Makonda. Makonda ni jasiri sana akiambiwa nenda kaseme hili hapo utampenda lakini sio yeye kwenda kuanzisha na kuongoza idara muhimu kama hii". Aliongeza MNEC Alipoulizwa kama ni hivyo aliwezaje kuwa mkuu wa mkoa wa Dar es salaam na sasa anaenda kuwa mkuu wa mkoa wa Arusha, alisema kuwa ukuu wa mkoa sio sawa na ukatika wa uenezi wa chama. Mtu yeyote anaweza kuwa mkuu wa mkoa lakini si kila mtu anaweza kuwa katibu mwenezi anayefaa na kuongeza kuwa hata huko Arusha akienda na mitazamo yake ile ile hatotoboa. "Idara ya Itikadi na Uenezi ni kitengo nyeti na muhimu ndani ya CCM...Miongoni mwa majukumu ya idara hiyo ni kushughulikia na kueneza masuala ya itikadi na Sera za CCM, kupanga na kusimamia mafunzo na maandalizi ya makada na wanachama na kusimamia vyombo vya habari vya chama, mawasiliano na uhamasishaji wa umma. sio kitengo cha maigizo, majigambo na ngonjera za kupanda mara farasi mara sijui trekta. Itikadi ni maarifa itikadi ni maoni, anahitajika mtu atakaelewa hilo sio ujanjaujanja" aluongeza Mjumbe huyo

YANGA SC KILA GOLI MILIONI 100 ZA KITANZANIA DHIDI YA MAMEMLODI.

 


YANGA SC KILA GOLI MILIONI 100 ZA KITANZANIA DHIDI YA MAMEMLODI.

RASMI: Muwekezaji wa klabu ya Yanga , Gharib Said Mohamed maarufu kwa jina la GSM ametoa ahadi kwa wachezaji wa klab ya Yanga kuwa atanunua kila goli litakalofungwa dhidi ya klabu ya Mamelodi Sundowns  kwa Tsh 100 Milioni,


👉Gsm 100 Milioni

👉Raisi Samia Suluhu 10

👉01 Milion - Aziz Ki 

👉05 Milion - Mwigulu

👉02 Milion - Mavunde


#SPORTSRIPOTI

Wednesday, April 3, 2024

ANGEL BENARD AOLEWA TENA.

 


Baada ya ndoa yake ya mwanzo kupasukiana, Msanii wa injili Angel Benard aolewa tena na mwanaume mwingine anayeishi nchini Marekani

Angel Benard aliyefahamika kwa nyimbo kadhaa ikiwemo Siteketei, watu walidhani ndoa yake ya mwanzo yeye na mumewe walikuwa na furaha sana kwa jinsi walivyokuwa wakiwaona ikiwemo mitandaoni, hivyo minong'ono imeibuka kuguata kuolewa tena nchini Marekani
Huku taarifa zikidai kuwa miezi mingi iliyopita Angel alikimbilia mahakamani kutaka talaka yake toka kwa mumewe wa mwanzo ili awe huru kuendelea na maisha yake mengine na alipopata talaka yake rasmi hakusubiri ameolewa tena na mwanaume anayeishi Marekani.

Monday, April 1, 2024

WANAOTOROSHA KOROSHO KWENDA NJE YA NCHI WAONYWA, SIKU ZAO ZINAHESABIKA

 

 



Na Oscar Assenga, TANGA.

BODI ya Korosho Tanzania Mkoani Tanga imewaonya wakulima wenye tabia za kutorosha Korosho kwenda kuuza nje ya nchi kuacha mara moja kufanya hivyo kwani siku zao zinahesabika kutokana na vyombo vya dola vinawatambua na watapokamatwa watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

Moja ya athari za utoroshaji wa Korosho kwenda nje ya nchi ni pamoja na kutokufikia malengo ya uzalishaji ikiwemo nchi mapato ambayo yangeweza kusaidia katika kuchochea maendeleo kwa wananchi wake.

Onyo hilo na Kaimu Meneja wa Bodi ya Korosho Mkoa wa Tanga Atufigwege Mwakyagi wakati akizungumza na waandishi wa habari namna bodi hiyo ilivyojipanga kukabiliana na vitendo hivyo huku wakiwataka wenye tabia hizo kuacha mara moja

Alisema kwani kufanya hivyo maana yake ni kulihujumu zao hilo pamoja na juhudi za Serikali ni kuhakikisha wakulima wanapata bei nzuri na bora ili kuweza kujikwamua kiuchumi kupitia kilimo hicho chenye tija.

“Ndugu zangu mnaotorosha korosho kufanya hivyo ni kosa na vyombo vya dola hivyo tambueni siku zenu zinahesabika sisi kama bodi hatutakubali kuona watu wanahujumu zao hilo kwani zinatakiwa kumnufaisha mkulima na Rais wetu Dkt Samia Suluhu ameweka nguvu kuhakikisha mkulima anapata bei nzuri na bora”Alisema

Aidha alisema kwamba wale ambao wanafanya hivyo wanataka kufifisha juhudi za Serikali ambazo ni kuona wakulima wa zao hilo wananufaika nalo na hatimaye kuweza kujikwamua kiuchumi na kubadilisha maisha yao hivyo hawatakuwa tayari kuona zinakwamishwa kwa namna yoyote ile.

Kaimu Meneja huyo alisema mauzo ya korosho msimu uliopita yalikuwa ni tani 741 kwenye mnada uliofanyika wilayani Mkinga na kufanikisha kuingiza fedha kiasi cha Sh.Milioni 703 ambazo wakulima wa zao hilo wameweza kunufaika nalo.

Akizungumzia suala la udhibiti ubora wa zao hilo alisema kwamba wa sasa wamekuwa wakitoa mafunzo kwa wakulima ili kuweza kulima kilimo chenye tija ili kudhibiti ubora kuhakikisha unakuwa mzuri kabla ya kwenda sokoni ambapo wamekuwa wakiuza kwenye mfumo rasmi.

Saturday, March 30, 2024

TEMESA TANGA YAZIDAI TAASISI ZA SERIKALI MADENI ZAIDI YA BILIONI 1.8 ,YAMO MADENI SUGU

 

Na Oscar Assenga,TANGA.

WAKALA wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA) Mkoani Tanga umesema kwamba unazidai Taasisi za Serikali madeni sugu ya zaidi ya Bilioni 1.8 ambao walikwenda kutengeneza magari yao katika karakana ya wakala huo ambapo mengine ni ya muda mrefu.

Hayo yalisemwa na Meneja wa Temesa Mkoa wa Tanga Mhandisi Jairos Nkoroka wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake ambapo alisema wanaziomba taasisi hizo kulipa madeni yao ili kuuwezesha wakala huo kuendelea kutekeleza shughuli zao kwa ufanisi.

Meneja huyo aliziomba taasisi hizo nazo ziweze kulipa madeni yao kutokana na kwamba nao pia wanadaiwa Bilioni 1.4 na wazabuni ambao wamekuwa wakipeleka vifaa kwa ajili ya kutengeneza magari

“Tunawakumbusha watulipe ili tuweze kuendelea kuwapa huduma kwani kutokufanya hivyo kunaweza kusababisha kutokupata huduma kwa wakati “Alisema

Aidha alisema kwamba madeni mengi ni ya nyuma ambayo wameyarithi na mengine wameyapeleka makao makuu yao kwa utaratibu mwengine na ya mwaka huu wanaendelea kuwadai kuhakikisha wanalipa

“Tumeanzia kitengo cha mahusiano kupitia mabalozi kwa kujenga mahusiano na hivyo kuzaidia wanaodaiwa kuanza kulipa madeni yao na tunaamini tutaendelea kupata mafanikio”Alisema

Aidha alisema ili kuweza kukabiliana na wadai hao sugu Temesa umeingia mkataba na wazabuni wakubwa (40) wa vipuri vya magari mkoani Tanga ili kuondoa ucheleweshaji ambao ulikuwepo hapo awali badala ya kuanza taratibu za manunuzi ambazo siku za nyuma zilikuwa zinawachelewesha.

Alisema wameamua kufanya hivyo ili kuweza kuhakikisha wanaondokana na ucheleweshwaji huo na kwa sasa wanachukua muda mfupi baada ya siku mbili.

Alisema mpango huo utasaidia kuwawezesha kupata vifaa ambavyo walikuwa hawana na vile vyengine ambavyo kwa hiyo kwa sasa ivi magari ya serikali yanayokwenda kufanyiwa matengenezo yanachukua muda mfupi sana na hatimaye kuruhusiwa kuendelea na shughuli zao.

“Hivi sasa tumeingia mikataba na wazabuni wakubwa na matengenezo ya magari ya Serikali yanatakiwa kutengenezwa na Temesa na tukishindwa kutengeneza kutokana na kitaaluma au vifaa kuna utaratibu ambao unafahamika na tunatoa vibali kwenda kwenye karakana nyengine na yanatrngezwa chini ya usimamizi wao”Alisema

“Katika ishu ya vifaa vya matengenezo ya magari tunatumia muda mfupi kulikagua gari na kubaini changamoto zake kutokana na uwepo wa vifaa vya kisasa “Alisema Jairos

Friday, March 29, 2024

AJALI YAUWA MASHABIKI WAWILI WA SIMBA KAMANDA AZUNGUMZA

VICTOR MASANGU/PWANI WATU wawili wamepoteza maisha na wengine watatu kujeruhiwa vibaya baada ya gari dogo la abiria aina ya Costa kupata ajali kwa kugongana na Lori katika eneo la Vigwaza Mizani Halmashauri ya Chalinze Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Pius Lutumo amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo majira ya saa 12:15 asubuhi ya leo. Kamanda Lutumo ameongeza kuwa katika ajali hiyo basi dogo lililokuwa likitokea Mkoani Mbeya kuelekea Jijini Dar es Salaam lilikuwa limebeba mashabiki wa klabu ya Simba. Aidha Kamanda Lutumo aliwataja marehemu katika ajali hiyo kuwa ni Oleison Mwakasila, anaekadiriwa kuwa na miaka 42-45, mkazi wa Kiwila mkoani Mbeya na Dereva wa gari hilo dogo aitwaye Moses Mwaisela mwenye umri wa miaka (40,). Ikumbukwe siku ya jana katika eneo la bonde la mto Ruvu Wilayani Kibaha kulitokea ajali nyingine iliyohusisha magari matatu kugongana na kupelekea vifo vya watu watatu.