
Mwenyekiti wa MISATAN na MPC, Edwin Soko (kulia) akimkabidhi Mkurugenzi wa BMG Media, George Binagi, tuzo maalum kutoka YouTube baada ya BMG Media kufikisha zaidi ya wafuasi (subscribers) laki moja.
Serikali imeombwa kuendelea kupunguza gharama za usajili wa vyombo vya habari mtandaoni (Online Media) ili kuongeza fursa za ajira na kujiajiri kwa vijana nchini.
.
Ombi hilo limetolewa Jumamosi Januari 24, 2026 na Mkurugenzi wa BMG Media, George Binagi, wakati wa hafla fupi ya kupokea tuzo maalum kutoka YouTube baada ya BMG Media kufikisha zaidi ya wafuasi (subscribers) laki moja.
.
Akizungumza katika hafla hiyo, Binagi amesema licha ya Serikali kupunguza gharama za usajili wa Online Media kutoka shilingi milioni moja hadi shilingi laki tano, bado kiwango hicho ni kikubwa kwa vijana wengi, hususan wahitimu wa taaluma ya uandishi wa habari na wabunifu wa maudhui, hivyo ameomba gharama hizo zishushwe hadi shilingi laki moja.
Ameeleza kuwa hatua hiyo itachochea vijana wengi zaidi kuanzisha vyombo vya habari mtandaoni na kujiajiri, jambo litakalosaidia kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira nchini.
.
Aidha, Binagi amesema kuanzia mwaka 2026, watengeneza maudhui mtandaoni wameanza kukatwa asilimia tano ya mapato yao na kuwasilishwa serikalini, huku wakiendelea kulipa kodi nyingine mbalimbali, hali ambayo imewaongezea mzigo wa kodi na kusababisha kile alichokitaja kama kulipa kodi mara mbili.
.
Kutokana na hilo, ameomba Serikali kulitafutia ufumbuzi suala hilo.
.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa MISATAN na MPC, Edwin Soko, amesema mitandao ya kijamii imeendelea kuwa fursa muhimu kwa vijana katika kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira, hivyo amewahimiza vijana kutumia mitandao hiyo kwa njia sahihi na yenye tija.
.
Kuhusu gharama za usajili na masuala ya kodi, Soko amesema atayawasilisha kwa mamlaka husika kupitia vikao mbalimbali vya wadau wa habari ambavyo vinaendelea kufanyika kwa lengo la kuboresha na kukuza sekta ya habari nchini.
.
#YouTube
#mwanza
#Habari
CC: @bmgonlinetv
Tupe maoni yako


0 comments:
Post a Comment