ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, January 21, 2026

MBOWE: MZEE MTEI HAKUWA NA SHARI NA MTU.

Mbowe: Mtei hakuwa na shari na mtu

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Freeman Mbowe, amesema Hayati Mzee Edwin Mtei (94), alikuwa ni mtu aliyejenga uhusiano mwema na watu wakati wote.

Mbowe ameeleza hayo Jana Jumanne Januari 20 jijini Arusha, wakati akizungumza na waandishi wa habari alipokuwa msibani.

Akisimulia namna alivyomfahamu Mzee Mtei, Mbowe, amesema hakuwa mtu wa shari, kila alikofanya kazi, alikuwa amejipanga na alikuwa hachagui rafiki ndani na nje ya chama.

Mtei, alifariki dunia usiku wa kuamkia Januari 19 mwaka huu, wakati akikimbizwa kupatiwa matibabu katika Hospitali  ya Selian Jijini Arusha, inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).

"Hakuwa mtu mwenye njaa, alikuwa ni mtu anayejiweza, akifanya siasa za mageuzi katika mazingira yale...misingi mikuu ambayo mzee huyu ametuachia ni sera. Tulikuwa na waasisi 12 wa CHADEMA." amesema Mbowe.

Mbowe amesema Mtei aliwasaidi kupata uzoefu ndani ya chama husuani masuala ya kifedha.

Amesema alikuwa na ujuzi mkubwa wa masuala ya kodi na sera pamoja na uzoefu mkubwa wa masuala ya kidiplomasia.


Wakati wa uhai wake, Hayati Edwin Mtei aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Kanda ya Afrika, Katibu

Mkuu wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC), Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Waziri wa Fedha wakati wa uongozi wa Hayati Julius Nyerere.

MWASISI WA SARAFU

Mbowe amesema: "Mzee Mtei, ndiye aliyekuwa mwasisi wa kwanza wa sarafu ya Tanzania, baada ya ile sarafu ya Afrika ya Mashariki baada ya sisi kuanzisha Benki Kuu ya Tanzania (BoT)".

KUUGUA

Mbowe amesema Mzee Mtei ameugua kwa muda mrefu na familia imepokea kwa uzito msiba huo kutokana na rekodi iliyotukuka, aliyoiweka ndani ya chama na Taifa.

Kwa mujibu wa Mbowe, Mzee Mtei alikuwa akipatiwa matibabu katika hospitali mbalimbali, ikiwemo Hospitali ya Nairobi-Kenya, Dar es Salaam na maeneo mengine kadha wa kadha.

Mbowe alisema: "Natambua CHADEMA  wametuma ujumbe katika msiba huu ili kuungana na familia kwa sababu mzee alikuwa ni mwasisi wa chama chetu. Ni kiongozi ambaye bado tulikuwa tunamuheshimu sana katika njia mbalimbali, kwa sababu misingi yote ya CHADEMA huyu ndiye aliyeianzisha"

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment