Kutoka kushoto ni Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa
Mataifa nchini, Alvaro Rodriguez, Mkurugenzi Mkazi na Mwakilishi wa Shirika la
Kupambana na UKIMWI la Umoja wa Mataifa (UNAIDS) nchini, Dk. Leo Zekeng
(katikati) pamoja na Mratibu wa UKIMWI Shirika la Kazi Duniani (ILO), Bi.
Getrude Sima (wa tatu kulia) pamoja na baadhi ya wafanyakazi wengine wa
mashirika ya Umoja wa Mataifa wakisubiria kuwasili kwa Mgeni Rasmi, Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa kutembelea banda hilo wakati wa hafla ya kilele cha
maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani yaliyofanyika Desemba Mosi 2018 jijini
Dodoma.
Mgeni rasmi Waziri Mkuu wa Tanzania, Mh. Kassim Majaliwa
akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkazi na Mwakilishi wa Shirika la
Kupambana na UKIMWI la Umoja wa Mataifa (UNAIDS) nchini, Dk. Leo Zekeng kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanywa na UN
nchini alipokuwa akitembelea mabanda ya maonyesho wakati wa hafla ya kilele cha
maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani yaliyofanyika Desemba Mosi jijini Dodoma.
Kushoto kwa Waziri Mkuu ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge,
Kazi, Vijana, Ajira na Wenyeulemavu Mhe. Jenista Mhagama.
Mgeni rasmi Waziri Mkuu wa Tanzania, Mh. Kassim Majaliwa
akihutubia wananchi (hawapo pichani) wakati wa hafla ya kilele cha maadhimisho
ya siku ya UKIMWI duniani yaliyofanyika Desemba Mosi 2018 jijini Dodoma.
Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, Alvaro
Rodriguez akitoa salamu kutoka kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wakati wa
hafla ya kilele cha maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani yaliyofanyika Desemba
Mosi 2018 jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mkazi na Mwakilishi wa Shirika la Kupambana na
UKIMWI la Umoja wa Mataifa (UNAIDS) nchini, Dk. Leo Zekeng akitoa salamu kutoka
wa wahisani wa maendeleo wa UKIMWI wakati wa hafla ya kilele cha maadhimisho ya
siku ya UKIMWI duniani yaliyofanyika Desemba Mosi 2018 jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wezee na
Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile akizungumza kwa niaba ya Waziri mwenye dhamana
wa wizara hiyo wakati wa hafla ya kilele cha maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani
yaliyofanyika Desemba Mosi 2018 jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Baraza la Watu Wanaosihi na Virusi vya UKIMWI
Tanzania (NACOPHA), Bi. Leticia Mourice akitoa salamu za baraza hilo kwa mgeni
rasmi Waziri Mkuu wa Tanzania, Mh. Kassim Majaliwa wakati wa hafla ya kilele
cha maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani yaliyofanyika Desemba Mosi 2018
jijini Dodoma.
Pichani juu na chini ni sehemu ya washiriki wakiwemo
wanafunzi wa shule mbalimbali za jijini Dodoma, Maafisa wa jeshi la Polisi,
wakazi wa jiji la Dodoma, Wafanyakazi wa taasisi mbalimbali za serikali,
viongozi wa dini pamoja wafanyakazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa
waliohudhuria hafla ya kilele cha maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani
yaliyofanyika Desemba Mosi 2018 jijini Dodoma.
Kikundi cha ngoma za asili cha Hiari ya Moyo (Mwinamila)
kikitoa burudani ya nyimbo za kuelimisha umma kuhusu masuala ya VVU kupitia
sanaa ya ngoma wakati wa hafla ya kilele cha maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani
yaliyofanyika Desemba Mosi 2018 jijini Dodoma.
UN yahimiza mapambano dhidi ya UKIMWI
Na Mwandishi wetu
UMOJA wa Mataifa umesema jamii ina wakati mgumu wa
kutengeneza mikakati ya kumaliza tatizo la UKIMWI ifikapo mwaka 2030 au la
kizazi kijacho kitabeba mzigo mzito wa kuendelea kupambana na janga hili la
kidunia.
Tamko hilo limetolewa wakati inatambulika kwamba watu
milioni 77 duniani wameambukizwa UKIMWI huku wengine milioni 35 wakiwa wamekufa
kutokana na magonjwa nyemelezi.
Kauli hiyo imetolewa juzi na Mratibu wa Mashirika ya Umoja
wa Mataifa nchini Alvaro Rodriguez wakati wa maadhimisho ya siku ya UKIMWI
duniani, akikariri waraka wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwenye siku hiyo.
Alisema miaka 30 tangu kuanzishwa kwa siku ya UKIMWI duniani,
bado hali ni tete na kwamba juhudi zozote tunazochukua sasa zinaweza kuonesha
kama tutazika UKIMWI ifikapo mwaka 2030 au la.
Alisema pamoja na dunia kupiga hatua kubwa katika kung’amua na
kutibu ugonjwa huo, hatua zilizofikiwa bado hajazifikia nia ya dunia ya
kuondokana na tatizo hilo.
Katibu Mkuu huyo alisema kwamba maambukizi mapya hayapungui
kwa jinsi dunia inavyotaka huku baadhi ya maeneo yakiwa nyuma zaidi huku
raslimali fedha zikizidi kupungua.
Pia hali ya unyanyapaa inazidi kuwa mbaya zaidi na huduma
kwa wahitaji zikiwa za kibaguzi na kusababisha kutokuwapo kwa uwazi.
Katibu mkuu huyo alitaka dunia kubadilika kuondokana na unyanyapaa
na ubaguzi na kuhakikisha kwamba huduma zinatolewa kuudhibiti na kuumaliza
ugonjwa huo.
Akizungumza katika siku ya UKIMWI mbele ya Waziri Mkuu wa Tanzania,
Kassim Majaliwa, Mratibu huyo wa Umoja wa Mataifa ameipongeza serikali ya
Tanzania kwa kuendeleza mapambano dhidi ya UKIMWI na kusema UN ipo sanjari na
juhudi za Tanzania.
Alisema amefurahishwa na ukweli kuwa mipango mikakati
iliyofanywa na serikali pamoja na mashirika ya Umoja wa Mataifa umeleta pamoja
wadau wengi katika mapambano hayo na kuwezesha kupata dola milioni 550 kutoka
Global Fund zitakazotumika katika mpango kazi wa mwaka 2018 hadi 2020.
Alisema kwa kushirikiana na TACAIDS na uongozi wa udhibiti
wa UKIMWI nchini Umoja wa Mataifa na wadau wengine wamewezesha Tanzania kupiga
hatua katika kukabiliana na maambukizi mapya.
Aidha alisema kampeni mbalimbali hasa za wanaume zimeanza
kufanikiwa na kwamba elimu inayotolewa inafanya wananchi kuwa wazi na kutafuta
huduma za kupima na dawa ili kuwa na taifa lenye afya.
Mratibu huyo alisema kwamba Umoja wa Mataifa uko tayari
kuendeleza ushirikiano wake na Tanzania ili ifikapo mwaka 2030, UKIMWI usiwe
tishio.
Alisema hilo litawezeka na kwa kuendelea kufanya kazi na
serikali na wadau mbalimbali Kwanza,katika harakati za kuzuia maambukizi mapya,
Pili: kuondoa kabisa mambukizi ya Virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama kwa mtoto
na tatu kupunguza ukatili wa kijinsia na kusaidia upatikanaji wa huduma za afya
zinazohusiana na UKIMWI kwa ujumla.
Naye Dk Leo Zekeng,
ambaye ni Mkurugenzi mkazi wa Shirika la UNAIDS alisema amefurahishwa na kuwapo
kwa utashi wa kisiasa kukabiliana na maradhi ya UKIMWI kutokana na serikali
kutumia mbinu mbalimbali kushawishi
uelewa na uwazi.
Alisema shirika lake litaendelea kufanyakazi na Tanzania
katika kuwezesha kupatikana kwa ruzuku mbalimbali za kusaidia kukabiliana na
maambukizi ya UKIMWI.
Alisema kutokana na juhdui za pamoja kati ya mashirika ya Umoja
wa Mataifa na serikali ya Tanzania watanzania wanakufa kwa sababu ya maambukizi
yamepungua kwa asilimia 70 kutokana na tiba za kufubaza virusi vya UKIMWI.
Alisema kuna watanzania 1,000,000 wanaotumia dawa za
kufubaza Virusi vya UKIMWI na kwamba lengo ni kuwa na asilimia 95 ya watu
wanatambua hali zao za kiafya.
Na kwamba 95% yao wanatumia dawa huku asilimia 95 wanaotumia
dawa wakifanikiwa kufubaza virusi hivyo.
Pamoja na kufurahishwa na serikali kuruhusu kujipima wenyewe
HIV Dk Leo ametaka jamii kuhakikisha inajikita kukabilina na maambukizi ya UKIMWI.
Wakati huo huo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kwamba
serikali ya Rais John Magufuli itaendelea kutekeleza na kuboresha huduma za
upimaji wa Virusi vya UKIMWI, kuzuia kabisa maambukizi ya kutoka kwa mama
kwenda kwa mtoto, matibabu ya magonjwa nyemelezi pamoja na kupiga vita
unyanyapaa wa aina zote kwa WAVIU.
Hata hivyo ametaka kila mmoja katika nafasi yake kuendelea
kuwakumbusha wanaoishi na VVU (WAVIU)kuendelea kutumia dawa za kufubaza makali
ya VVU bila kuacha.
Pia aliitaka jamii jamii kutowanyanyapaa au kuwabagua WAVIU
huku akitoa wito kwa watu wote hususan wanaume kujitokeza kupima ili wajue hali
zao.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.