TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Freeman Mbowe amesema kuwa hawatashiriki shughuli ya kuapishwa kwa Dk. John Pombe Magufuli inayotarajiwa kufanyika Alhamis, Novemba 5, 2015.
Kauli hiyo ya Mwenyekiti Mbowe aliyoitoa leo, imekuja wakati kukiwa bado kuna sintofahamu kubwa miongoni mwa Watanzania kuhusu mchakato wa uchaguzi hususan upigaji kura, ukusanyaji na ujumlishaji wa matokeo ulivyofanyika hasa katika nafasi ya urais.
"Hatutahudhuria shughuli hiyo ya kumwapisha Magufuli. Tumekubaliana wote kwenye UKAWA, ndani ya CHADEMA, viongozi wetu, wabunge wetu wote hawatahudhuria uapishwaji wala sherehe.
"Tumetoa wito kwa wananchi wote, Watanzania wote, wapenda mabadiliko na wapenda haki wote kwa ujumla kutohudhuria shughuli hiyo," amesema Mwenyekiti Mbowe.
Mwenyekiti Mbowe amesisitiza kuwa UKAWA, wapenda mabadiliko wote na Watanzania wapenda haki hawakubaliani na wanapinga mchakato wa uchaguzi hususan matokeo ya urais ambayo, kwa mujibu wa Katiba ya Nchi aliyosema ni mbovu, yakishatangazwa hakuna haki ya kuyapinga katika mahakama yoyote ile.
"Tunataka nchi na dunia nzima ijue wazi kuwa hatukubaliani na mchakato wa uchaguzi hasa matokeo ya urais ambayo kwa mujibu wa Katiba yetu mbovu, Mwenyekiti wa Tume akishatangaza hakuna mahali pa kuyapinga."
"Matokeo ya ubunge au udiwani yanaweza kupingwa mahakamani, lakini kwa matokeo ya urais Katiba yetu mbovu inawafunga mikono na miguu Watanzania wote ambao wangependa waone haki imetendeka katika nafasi hiyo," amesema Mwenyekiti Mbowe.
"Watawala wamechezea haki ya Watanzania kupiga kura. Kura zimehesabiwa kama karatasi za kawaida tu. Hujuma dhidi ya matokeo ya wagombea wetu imehujumiwa waziwazi. Safari hii hujuma hazikuwa kificho tena. Kila mtu amejionea matokeo yaliyokuwa na Jaji Lubuva si yale ambaye yalikuwa yamebandikwa vituoni. Hayakuwa na uhalisia na matokeo yaliyokusanywa na mawakala. Uchaguzi umefanywa kama ni jambo lisilokuwa na maana yoyote. Hiyo ni hatari sana kwa taifa lolote linalotaka kukuza demokrasia kama mojawapo ya nguzo za maendeleo. Hatuwezi kukubali kufika huko," amesema Mbowe.
Aidha, Mwenyekiti Mbowe ameongeza kusema kuwa vyama vinavyounda UKAWA vimeitisha kikao cha Wabunge wateule wote wa vyama hivyo ambao watakutana Alhamis, saa 4 asubuhi, jijini Dar es Salaam.
Imetolewa leo Jumatano Novemba 3, 2015 na;
Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.