Baadhi ya wafanyakazi wa DAWASCO wakiliombea dua shirika hilo ili liweze kutimiza malengo yake ya kutoa huduma ya maji safi na maji taka kwa usalama kwa wakazi wa miji ya Dar es Salaam,Kibaha na Bagamoyo.
NA: Dixon Busagaga
WIZARA ya maji na umwagiliaji, imesema
inaridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mipango ya usambazaji wa huduma za maji,
inayofanywa na shirika la majisafi na majitaka jijini Dar es Salaam (DAWASCO)
na kutoa rai kwa watumishi wa shirika hilo kushirikiana ili kufikia malengo ya
utoaji wa huduma kwa wananchi.
Hayo yalisemwa jana na katibu mkuu wa
wizara hiyo mhandisi Mbogo Futakamba, alipokuwa akiwahutubia wafanyakazi wa
DAWASCO, katika makao makuu ya shirika hilo jijini Dar es Salaam.
Mhandisi Futakamba, alisema kasi ya
utoaji wa huduma bora za maji kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam, imepunguza
malalamiko mengi ya wananchi, na kwamba serikali imeanza kupata matumaini
makubwa na kujenga imani kwa shirika hilo kwa kufanikisha malengo makuu ya
usambazaji wa huduma hiyo kwa wananchi.
Aidha alisema kwa kiwango kikubwa
wizara ya maji na umwagiliaji kwa sasa inajivunia kwa kazi nzuri iliyofanywa na
shirika hilo, hasa kwa kuzingatia kuwa DAWASCO ndio jicho la wizara kutokana na
wingi wa wananchi wanaohitaji huduma za maji zinazosambazwa na shirika hilo.
“Nimeona jitihada zenu, nimependa
jinsi mnavyofanya kazi kama timu, naomba muwe na uaminifu mkubwa sana katika
kazi, kuweni wawajibikaji ili wananchi wapate huduma ya maji”, alisema mhandisi
Futakamba.
Katika hatua nyingine katibu mkuu huyo
alipongeza juhudi kubwa zilizofanywa na shirika hilo za kupunguza kiwango cha
upotevu wa maji pamoja na kudhibiti wizi wa maji, ambavyo vimekuwa kikwazo
kinachochochea malalamiko ya wananchi kwa shirika hilo.
Awali akitoa taarifa ya shirika hilo,
afisa mtendaji mkuu wa DAWASCO, mhandisi Cyprian Luhemeja, alisema shirika hilo
limefanikiwa kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji, baada ya kuongeza
uzalishaji kutoka mita za ujazo 7,834,234 hadi mita za ujazo 8,421,370 kati ya
mwezi Mei hadi Novemba 2015.
Alizitaja sababu za mafanikio ya
ongezeko la kiwango cha maji ni pamoja na udhibiti wa upotevu wa maji katika
bomba kubwa, kufanya matengenezo ya tahadhari, maboresho ya maslahi ya
wafanyakazi na kuboreshwa kwa kitengo cha upotevu wa maji.
Mhandisi Luhemeja alibainisha kuwa
DAWASCO, imefanikiwa kufunga dira katika maungio ya maji, kuziba maeneo
yanayovujisha maji kwa wakati, kupambana na wezi wa maji, kuhakiki ufanisi wa
dira za maji, kusajili maboza ya wauzaji maji na kuboresha usomaji wa dira,
ambavyo viliwezesha kupunguza kiwango cha maji yanayopotea kutoka asilimia 62
hadi 45, kati ya mwezi Mei mpaka Novemba 2015.
Aliongeza kuwa mafanikio ya
utekelezaji wa mipango ya uboreshaji wa huduma za maji yaliwezesha shirika hilo
la DAWASCO, kuongeza makusanyo ya mapato kutoka shilingi bilioni 2.9 hadi
kufikia bilioni 6.2 kati ya mwezi Mei hadi Novemba 2015.
Wakati huo huo shirika hilo limeanza
kutekeleza agizo la serikali linaloitaka DAWASCO, kuongeza idadi ya wateja wake
hadi kufikia milioni moja, katika jiji la Dar es Salaam, miji ya Kibaha na
Bagamoyo mkoani, hadi kufikia mwezi Juni 2016.
Katika utekelezaji wa agizo hilo
DAWASCO iko katika utekelezaji wa Maagizo ya serikali ya kuhakikisha wananchi
waishio katika Jiji la Dar s salaam, Miji ya Kibaha na Bagamoyo Mkoani Pwani
wanaunganishiwa Maji ifikapo Julai 2016. Katika kutekeleza agizo hilo Dawasco
imejipanga katika awamu kuu NNE (4)
1.
Awamu
ya kwanza itawahusu wateja wote walioko katika maeneo ambayo kwa sasa yanapata
maji na kuna miundo mbinu ya mabomba karibu.
2.
Awamu
ya Pili itahusu maeneo ambayo yamepitiwa na mabomba makubwa ya Maji jirani
lakini wananchi wake hawana maji kwa sababu ya kukosekana kwa miundo mbinu ya
usambazaji.
3.
Awamu
ya Tatu itahusisha maeneo yote yaliyopitiwa na mradi maarufu wa Mabomba ya Kichina, Maunganisho katika
awamu hii yataanza baada ya kukamilika kwa Miradi ya Ruvu Chini na Ruvu Juu,
4.
Awamu
ya Nne itaanza katika maeneo yote ambayo
kwa sasa hakuna miundo mbinu ya Maji na yako mbali kutoka katika mabomba
makubwa .
Gharama ya kuunganishiwa huduma ya
Majisafi ni Tsh 200,000 kwa wateja wadogo (Domestic Customers)na Tsh 400,000
kwa wateja wakubwa (Corporate Customers) Mwisho.
|
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.