HOTUBA YA
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI, MATHIAS CHIKAWE (Mb) ALIYOTOA KATIKA MKUTANO
NA WAANDISHI WA HABARI TAREHE 21 OKTOBA,
2015 KATIKA UKUMBI WA MIKUTANO WA WIZARA
Ndugu
Waandishi wa Habari,
Mabibi na
Mabwana,
Kama mnavyojua tarehe 25
ya mwezi huu wa Oktoba mwaka 2015 siku ya Jumapili katika nchi yetu kutafanyika
Uchaguzi Mkuu kwa ajili ya kuchagua rais,
wabunge na madiwani zoezi ambalo litawashirikisha watanzania wote
waliojiandikisha kupiga kura kwa mujibu wa sheria.
Zoezi hili kwa mujibu wa sheria za
uchaguzi litasimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi yaani NEC kama ambavyo
imekuwa ikifanyika katika chaguzi mbalimbali zilizopita ama kuwahi kufanyika
katika nchi yetu.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
inalo jukumu kubwa la kuhakikisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao
unaimarishwa kabla, wakati na baada ya zoezi hilo la Uchaguzi Mkuu katika
maeneo yote ya nchi yetu, ili wananchi waweze kuwa salama na kuendelea na
maisha yao ya kila siku.
Ndugu Waandishi wa habari,
Kumekuwepo na taarifa mbalimbali za vitisho zinazosambazwa kwenye
mitandao ya kijamii na hata mitaani na watu wasio na nia njema kwa taifa letu, zikiwataka wananchi wanunue mahitaji yao
mbalimbali ikiwemo vyakula na kuvihifadhi kwa ajili ya kuja kuvitumia wakati na
baada ya uchaguzi kwa ubashiri wa kuwepo kwa vurugu wakati ama baada ya
uchaguzi.
Taarifa hizi
zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii na mitaani kwa ujumla ni taarifa
potofu ambazo zinalenga kuwajengea wananchi hofu na mashaka, wasiwasi na
vitisho pasipo sababu zozote zenye tija kwa taifa
letu.
Ndugu zangu Waandishi wa
habari,
Nitoe rai
kwa Raia wote waishio hapa nchini yaani Watanzania na Wageni kupuuza taarifa
zote zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii na mitaani kwa kuwa taarifa hizo
si za kweli, na wala hazilengi kulinda amani iliyopo nchini kwetu.
Pamoja na hayo kumekuwa na matamko kwa
baadhi ya wanasiasa katika kampeni zao kudai kuwa Serikali itasitisha posho za askari
mara baada ya Uchaguzi Mkuu, Taarifa
hizi si za kweli kwani Posho za Vyombo vyote vya dola vilivyopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya
Nchi ni za kudumu kama ilivyoelekezwa
katika waraka wetu, hazitafutwa wala kubadilika na iwapo zitabadilika ni kwa
kupandishwa na wala si kufutwa.
Nawaomba wananchi wote watii sheria za nchi na zile za Tume ya Uchaguzi zinazoongoza Uchaguzi
Mkuu sambamba na kufuata Maelekezo yatakayotolewa na Tume hiyo kabla, wakati na
baada ya kupiga kura jambo litakalosaidia kuilinda amani ya nchi yetu, kwani
kila Mtanzania anao wajibu wa kuilinda amani kwa kufuata sheria za nchi bila
kushurutishwa.
Wananchi wanapaswa kutambua kuwa
baada ya uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 25 mwaka huu maisha ya watanzania
yanapaswa kuendelea kama kawaida hivyo itikadi zao za vyama vya siasa
zisiwatofautishe na kuwajengea chuki, uhasama ama uadui kwani watanzania ni
wamoja na wamekuwa wakiishi kwa amani, umoja na ushirikiano katika kuendeleza
taifa hili.
Ndugu waandishi wa Habari,
Wananchi
hawapaswi kuwa na hofu yoyote kwa kuwa Serikali ya awamu ya nne ambayo
imeongoza na kuwatumikia wananchi kwa kipindi cha miaka kumi inakusudia kwa dhati kukabidhi madaraka kwa
serikali iyajo ya awamu ya tano katika hali ya amani na utulivu.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama inawahakikishia wananchi kuwa itahakikisha
hali ya amani na utulivu inakuwepo na kuimarishwa kabla, wakati na baada ya
Uchaguzi Mkuu mpaka pale ambapo Uongozi wa
serikali ya awamu ya tano utakapoingia
madarakani.
Wananchi watoe taarifa Polisi pale
watakapoona kuna dalili za uvunjifu wa
amani kwa kupiga simu ya bure namba 112.
Nawashukuru kwa kunisikiliza,
Asanteni .
Imeandaliwa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.