CHUO Kikuu Cha Nelson Mandela Sayansi na
Teknolojia (NM-AIST) kimesaini makubaliano ya kiasi cha dola za kimarekani
30,000 sawa na kiasi cha shilingi hamsini na moja milioni kutoka kampuni ya
Huawei Tanzania ikiwa ni katika malengo mahususi ya kuwasaidia wanafunzi wa
shahada ya uzamili katika kufanya tafiti kwenye Nyanja za teknolojia na habari
(TEKNOHAMA).
Akizungumza wakati wa kusaini makubaliano hayo jijini Arusha
mwishoni mwa wiki, Makamu Mkuu wa Chuo Profesa Lughano Kusiluka amesema
kuwa huu ni mwaka wa pili wa makubaliano na Huawei ya kukisaidia chuo kiasi cha
dola 30,000 kila mwaka kwa muda wa miaka mitatu katika mikakati ya kuwainua
wanafunzi wa Teknohama kwenye tafiti.
Profesa Kusiluka aliongezea kuwa msaada huo siyo tu utakisaidia
chuo na wanafunzi kuweza kuisadia nchi yetu ya Tanzania katika kupiga hatua za
kiuchumi na maendeleo kupitia sekta ya mawasiliano na habari.
“Kama mliovyomsikia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
wakati akihutubia wahitimu, amesisitiza kuwa tafiti za kisayansi ni muhimu sana
katika kukuza uchumi wa taifa lolote lile Duniani, hivyo msaada huu kutoka
Huawei utaleta chachu kubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi,” alisema
Aliongezea: “Kwa niaba ya Uongozi wa Chuo, tunaishukuru sana
kampuni ya Huawei Tanzania kwa mchango wake ambao kwa kiasi kikubwa
umefanikisha sana matokeo ya wahitimu hawa tulio nao leo. Huawei wamejitolea
kuchangia utafiti kwa miaka mitatu na huu ni mwaka wa pili, tunawaomba
waendelee kuwa nasi hata baada ya mwaka wa tatu wa makubaliano”
Akizungumza kwa niaba ya wanavyuo wenzake
waliofaidika, Michael Mollel alisema: “Binafsi natoa shukrani zangu za
dhati kwa Huawei Tanzania kwa mchango huu, mimi nilifanya utafiti wangu katika
jiji la Dar es Salaam, ilinichukua miezi mitatu kukamilika, na kwa gharama
zilivyo katika jiji hilo, nimgekuwa katika hali ngumu sana na hata kushindwa
kumaliza utafiti kama siyo kwa msaada kutoka Huawei”
Mollel aliongezea kuwa mafanikio yake hadi kufikia
kutunukiwa shahada ya uzamili yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na msaada huo wa
Huawei waliotoa katika chuo cha NM-AIST.
Kampuni ya Huawei Tanzania mwishoni mwa wiki ilishuhudia
mafanikio makubwa ya mpango wake wa kuchangia utafiti kwa wanachuo wa shahada
ya uzamili katika Taasisi ya Sayansi na Technolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST)
ya Jijini Arusha.
NM-AIST imefanya mahafali yake ya pili ambapo wahitimu wa
shahada ya Uzamili walikuwa 93 na uzamivu walikuwa 13, ambayo ni asilimia 95 na
karibu asilimia 50 ya jumla ya wadahiliwa wa makundi haya.
Wahitimu wa shahada ya uzamili wa kike ni asilimia 33 na wa
shahada ya uzamivu ni asilimia 25.
Mahafali hayo yalihudhuliwa na Rais Jakaya Kikwete, Makamu
wa Rais Dr Mohamed Gharib Bilal pamoja na waziri wa Sayansi na Teknolojia
Profesa Makame Mbarawa.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.