ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, May 22, 2014

TAHADHARI: UGONJWA WA DENGUE WATINGA MWANZA

Mkuu wa wilaya ya Nyamagana Baraka Konisaga (L) akitoa taarifa taarifa ya kuwepo kwa ugonjwa wa Dengue katika Mkoa wa Mwanza ambapo hadi sasa amepatikana mgonjwa mmoja katika Hospittali ya Rufaa ya Sekou-toure ambaye amethibitika kuwa na ugonjwa huo, kulia ni Mganga mkuu wa mkoa wa Mwanza valentino Bangi.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Valentino Bangi akielezea jinsi walivyobaini ugonjwa wa Dengue kupitia mtu aliyefika katika Hospittali ya Rufaa ya Sekou-toure na kuthibitika kuwa na ugonjwa huo ambapo pia alitilia msisitizo njia za kuuthibiti ugonjwa katika jamii. BOFYA PLAY KUMSIKILIZA.
Mganga Mfawidhi Hospitali ya Mkoa Sekou Toure Dr. Onesmo Rwakyendela ametoa wito kwa wananchi hususani wa visiwani kwa sababu ugonjwa huu una dalili kama za maleria basi wanapo jihisi kuwa dalili hizo wakimbilie hospitali kupata vipimo na hatimaye wapate tiba. 
Waandishi wa habari toka vyombo mbalimbali wakisikiliza kwa umakini utolewaji wa taarifa ya kuwepo kwa ugonjwa wa Dengue katika Mkoa wa Mwanza ambapo hadi sasa kuna mgonjwa mmoja katika Hospittali ya Rufaa ya Sekou-toure ambaye amethibitika kuwa na ugonjwa huo.
Ni mazingira ya nje Hospitali ya Rufaa ya Sekou-toure mahali alipolazwa mtu mmoja mtumishi mstaafu mwenye umri wa miaka 62 mkazi wa Kilimahewa wilaya ya Ilemela mkoa wa Mwanza, ambaye amethibitika kuwa na ugonjwa wa Dengue.

 KUWEPO KWA UGONJWA WA DENGUE   KATIKA MKOA WA MWANZA

TAARIFA  KWA  UMMA

Ndugu, Waandishi wa habari, wawakilishi wa vyombo vya habari na wananchi wote. Napenda kutoa taarifa ya kuwepo kwa ugonjwa wa Dengue katika Mkoa wa Mwanza. Hadi sasa kuna mgonjwa mmoja katika Hospittali ya Rufaa ya Sekou-toure ambaye amethibitika kuwa na ugonjwa huo.  Kufuatia taarifa hii  napenda wananchi wafahamu machache kuhusu ugonjwa wa Dengue. Ugonjwa wa Dengue husababishwa na VIRUS vinavyoitwa “Dengue Virus”  na vinaenezwa na mbu aina ya Aedes.

Mbu hawa hupendelea kuzaliana kwenye maji yaliyotuama karibu na makazi ya watu au kwenye vyombo vya kuhitadhia maji majumbani.

JINSI UGONJWA WA HOMA YA DENGUE UNAVYOENEZWA

Binadamu hupata ugonjwa huu baada ya kuumwa na mbu wa aina ya Aedes aliye na Virusi vya ugonjwa huu.  Mbu  hawa hupendelea kuuma wakati wa mchana.

Ugonjwa huu huwapata wetu wa rika zote aidha watoto wenye umri chini ya miaka mitano na mama wajawazito huathirika zaidi.

Ndugu wananchi

Dalili za Ugonjwa wa Homa ya Dengue

Asilimia 90 ya wagonjwa walioambukizwa ugonjwa huu uonyesha dalili awali kuanzia siku ya 3 hadi 14 baada ya kuumwa na mbu mwenye virusi vya ugonjwa huu dalili hizi ni kama zifuatazo:
·        Homa kali ya ghafla
·        Kuumwa kichwa hususani sehemu za machoni
·        Maumivu makali ya misuli pamoja na viungo vya mwili
·        Kichefuchefu au kutapika
·        Kuvimba tezi
·        Kupatwa na harara
Asilimia 10 ya wagonjwa hupatwa na dalili kali kama kutokwa na damu kwenye sehemu za uwazi za mwili mfano mdomoni, masikioni pamoja na sehemu za kutolea haja ndogo na kubwa.

Ndugu wananchi,
Njia za kujikinga na Homa ya Dengue
Ugonjwa wa dengue unazuiliwa kwa njia zifuatazo:-
·        Kuangamiza mazalio ya mbu
·        Kufukia madimbwi ya maji au nyunyizia dawa ya kuua viluwiluwi vya mbu kwenye madimbwi hayo
·        Kuondoa  vitu vyote vinavyoweza kuwa mazalia ya mbu kama vile vifuu vya nazi, makopo, chupa na magurudumu ya gari ambavyo vinaweza kufanya maji kutuama karibu na makazi.
·        Kufyeka nyasi na vichaka vilivyo karibu na makazi.
·        Kuhakikisha maua yanayopandwa kwenye makopo au ndoo hayaruhusu maji kutuama
·        Kufunika mashimo ya maji taka kwa mfuniko
·        Kusafisha mitaro na  gata za paa la nyumba ili kutoruhusu maji kutuama.

Kuzuia kuumwa na mbu kwa:-
·        Kutumia dawa za kufukuza mbu  (Repellents)
·        Kuvaa nguo ndefu
·        Kuweka wavu wa kuzuia mbu kwenye madirisha na milango
Kwa kufanya hayo, tunaamini tunaweza kuzuia maambukizi ya ugonjwa huu yasiendelee kutokea.  Naomba kila mmoja atimize wajibu wake.

Asanteni kwa kunisikiliza,



Baraka M. Konisaga
KAIMU MKUU WA MKOA
MWANZA


Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.