Jeshi la Polisi mkoani Geita linamshikilia mwanamke aitwaye Martha Japhet (44), mkazi wa Kitongoji cha Mzalendo, Kata ya Nyarugusu, Wilaya ya Geita, kwa tuhuma za kumuua mume wake na kumzika ndani ya nyumba yao, kisha kufunika kaburi hilo kwa magunia ya muhogo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Safia Jongo, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, akibainisha kuwa mauaji hayo yalifanyika usiku wa Oktoba 11, 2025, majira ya saa 3:00, na kugundulika Oktoba 16, 2025, majira ya saa 7:00 mchana.
Kwa mujibu wa Kamanda Jongo, uchunguzi wa awali umebaini kuwa mama huyo alimjeruhi mumewe kwa kitu chenye ncha kali baada ya kutokea ugomvi baina yao. Baada ya tukio hilo, watoto wa familia hiyo walianza kumtafuta baba yao bila mafanikio, hali iliyozua mashaka miongoni mwa majirani na hatimaye kufanikisha kugundulika kwa tukio hilo.
Kamanda Jongo ametoa wito kwa jamii kuepuka tabia ya kujichukulia sheria mkononi wanapokumbana na changamoto au migogoro ya kifamilia. Pia, amesisitiza umuhimu wa kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama pale mtu anapopotea au kunapotokea tukio linalotia shaka.
“Wakati mwingine matukio ya watu kupotea huchangiwa na watu wa karibu kabisa, hivyo jamii inapaswa kuwa makini na kutoa taarifa mapema,” alisema Kamanda Jongo.
Tupe maoni yako

0 comments:
Post a Comment