ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, April 18, 2023

SUNGUSUNGU WASAKWA KWA KUPIGA KUMJERUHI MWANAMKE


Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga linawatafuta sungusungu zaidi ya 30 waliohusika kumcharaza viboko hadharani na kumsababishia majeraha mbalimbali mwilini, Manka Mushi (26) mkazi wa Kijiji cha Ikoma Kata ya Itilima Halmashauri ya Kishapu kwa madai ya kuiba Sh 420,000/= za mteja wake.

Akizungumzia tukio hilo lilitokea Aprili 14, 2023 na kumsababisha binti huyo kulazwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Janeth Magomi amesema baada ya sungusungu hao wa jeshi hilo la jadi kufanya tukio hilo kwenye uwanja uliopo katika kijiji hicho walikimbia.

Akisimulia mkasa uliomkuta, Manka aliyekuwa akifanya kazi baa na nyumba ya kulala wageni kijijini humo amesema ilikuwa Saa sita usiku ambapo mteja aliyefahamika kwa jina la Julius Tarimo aliagiza kupelekewa shuka, baada ya kumpelekea ghafla alimkaba koo akimtaka kurudisha Sh420, 000 alizohisi binti huyo kachukua.

Manka amesema alikataa kuhusika na wizi huo na kupiga kelele za kuomba msaada kisha Julius kumtishia kuwa atamtambua baada ya binti huyo kumkataa kimapenzi na baadaye alifanikiwa kutoka ndani ya chumba hicho.

 “Kufuatia hatua hiyo niliambiwa na kamanda wa sungusungu twende uwanjani na baada ya kufika nilikuwa mwanamke pekee yangu nikaambiwa ni lale chini katikati ya wanaume zaidi ya 30 ukaletwa mzigo wa fimbo wakaanza kunicharaza viboko kwa zamu nikijaribu kuinuka wengine wanapiga mgongoni na kichwani,” amesema Manka

Amesema aliwapa namba ya mama yake mzazi ambaye anaishi jijini Arusha, walimpigia na kuzungumza naye kisha kumtaka atume hela lakini aliwaomba wampeleke polisi na baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya walimpeleka ofisi ya Kata kutoa maelezo hakupokelewa.

“Namshukuru Mungu kwa sasa naendelea vizuri tofauti na awali ambapo sehemu ya makalio na mgongoni kulikuwa kumejaa vidonda, Naomba Serikali iwachukulie hatua kali sungusungu walionifanyia kitendo hicho,”amesema

Muhudumu wa wodi namba saba ya wanawake na upasuaji katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Weru Kiula amesema walimpokea Manka Aprili 14 mwaka huu akiwa na hali mbaya na vidonda kwenye makalio na mgongoni lakini kwa sasa anaendelea vizuri.

Ofisa Ustawi wa Jamii Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga, Prisila Mushi amesema matukio ya wanawake kupigwa na sungusungu yamekuwa yakitokea mara kwa mara na kuiomba Serikali ichukuwe hatua kali kwa watu waliohusika na ukatili huo.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.