ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, March 16, 2017

QUALITY GROUP KUANZISHA KAMPUNI LUKUKI KUUNGA MKONO JUHUDI ZA RAIS MAGUFULI

 Ofisa Mtendaji Mkuu  wa Kundi la Kampuni za Quality Group Limited (QGL), Nicholas Ralph akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam, kuunga mkono jitihada za Rais John Magufuli katika mapambano dhidi ya rushwa, ufisadi na juhudi za kuliletea Taifa maendeleo endelevu katika nyanja mbalimbali. (PICHA NA RICHARD MWAIKENDA;KAMANDA WA MATUKIO BLOG)
 Ralph akielezea jinsi uongozi ulivopanga mikakati ya kuboresha kampuni zilizopo na kuanzisha nyinginezo nchini na nje ya nchi.
Sehemu ya wanahabari wakiwa katika mkutano huo

Suleiman Msuya
KAMPUNI ya Quality Group Limited (QGL), imesema inaunga mkono jitihada za Rais John Magufuli katika mapambano dhidi ya rushwa, ufisadi na juhudi za kuliletea Taifa maendeleo endelevu katika nyanja mbalimbali.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari katika ofisi za kampuni hiyo Barabara ya Nyerere, Dar es Salaam leo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa QGL, Nicholas Ralph alisema katika kuunga mkono vita dhidi ya ufisadi wameanzisha mfumo unaotambua na kudhibiti uhalifu huo kwenye taasisi (e-Governance).

Alisema mfumo huo wa utambuzi na udhibiti unapaswa kuwepo katika idara zote za Serikali kwani una utija ni salama zaidi hasa katika kulekea katika Tanzania ya maendeleo endelevu.

Ralph alisema QGL imewekeza katika sekta mbalimbali  kama afya ambapo wanatarajia kujenga vituo 4,000 vya afya nchini kote pamoja na vioski vya kutoa afya ili kuendana na teknolojia ya sasa na kurahisisha kila mwananchi anapata huduma bora ya afya.

Alisema pia wamekubaliana na kampuni kutoka nchini Urusi ili kusambaza vifaa tiba na kampuni nyingine kutoka Marekani itatoa huduma ya ndege katika huduma ya dharura.

“Pia kampuni ya QGL imeingia makubaliano na kampuni kutoka nchini Ireland kujenga na kuwekea uongozi katika utawala ambapo itasaidia kuongeza teknolojia kwa kampuni za ndani,” alisema.

Mkurugenzi huyo alisema kampuni ya QGL imekuwa ikisadia wavuvi katika Kanda ya Ziwa kwa kuwapatia vitendea kazi na matibabu, kusaidia elimu na pia ilisaidia mapambano ya ugonjwa wa Ebola.

Alisema kampuni yao imefanikiwa kuongeza ajira, mafunzo, kukuza uchumi ili kuhakikisha inaunga mkono  mpango wa maendeleo wa Serikali wa 2025.

Ralph alisema wamekuwa wakitoa mafunzo kwa viongozi na waajiriwa vijana kupitia program ya Moreh Derech ambayo imekuwa na mafanikio makubwa.

Aidha, alisema katika kuhakikisha kuwa wanapanua ushirikiano na taasisi za kimataifa wamesaini makubaliano na Kampuni ya  Solanika International Tractors Limited ya India ambao watakuwa wanaingiza matrekta 1,000 kwa mwaka hivyo kuongeza ajira 1,200 ifikapo mwaka 2018.

“Pia tumesaini barua katika miradi ya madini ambapo tunarajia kuuzungumzia vizuri pindi hatua zote zikiwa zimekamilika,” alisema.

Halikadhalika alisema wamewekeza katika viwanda vya sukari na maziwa ambapo wananchi wengi wa Kitanzania ndio watafaidika kwa kuuza bidhaa husika katika viwanda hivyo vyenye teknolojia ya kisasa na uongozi kutoka Israel, Ulaya na Afrika Kusini.

Ralph alisema QGL imekuwepo kwa zaidi ya miaka 30 ambapo inashirikiana na kampuni kubwa duniani kama General Motors (GM), Honda, Isuzu, Bridgestone na Chevrolet.

Alisema kutokana na ushirikiano huo QGL imeajiri zaidi ya watu 667,300 na kupata faida ya dola za Marekani bilioni 348.6 hayo yakichangiwa na uwajibikaji, uwazi, uaminifu na mafanikio.


Alisema mikakati yao ni kuhakikisha kuwa wanakuwa ni sehemu sahihi ya kuchochea maendeleo ya nchi na wananchi wa Tanzania. 

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.