ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, July 29, 2025

HATIMAYE CCM YAWAWEKA WAZI WAGOMBEA WAKE, BAADHI YA VIGOGO WAENGULIWA KULETA MABADILIKO

 




Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Chama cha Mapinduzi (CCM) kupitia Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, CPA Amos Makalla, kimetangaza rasmi majina ya wagombea watakaoshiriki Uchaguzi Mkuu wa 2025 kwa nafasi za Ubunge wa Majimbo, Viti Maalum na Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi, baada ya kukamilika kwa mchakato wa kuchuja na kupitisha majina uliochukua muda mrefu.

Akizungumza leo Julai 29, 2025, CPA Makalla amesema uteuzi huo uliofanywa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM umehusisha majimbo 272 kwa upande wa Tanzania Bara na ulihitaji umakini wa hali ya juu zaidi kuliko wakati mwingine wowote kutokana na wingi wa maombi ya wagombea.

“Majimbo zaidi ya elfu tano yalipokea maombi ya wagombea,kazi hii ilikuwa kubwa na ilihitaji umakini mkubwa,Kwa wale ambao hawajapata uteuzi, niwaombe waendelee kuwa watiifu kwa chama kwani bado CCM inawathamini,” amesema CPA Makalla.
Aidha, Makalla amezungumzia shauku kubwa ya Watanzania waliofuatilia mchakato huo kwa hamu, akibainisha kuwa hali hiyo inaonyesha nafasi muhimu ya CCM katika maisha ya watanzania na imani yao kwa chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu.

Katika orodha iliyotangazwa, baadhi ya vigogo wa chama hicho, akiwemo Luhaga Mpina, Mrisho Gambo, Angelina Mabula na January Makamba, hawajarejea kwenye majina ya mwisho ya wagombea, hatua inayotafsiriwa kuwa ni sehemu ya mabadiliko makubwa yanayolenga kuboresha uongozi wa chama hicho.

Taarifa za awali zinaonyesha kuwa baadhi ya majimbo yalikuwa na idadi kubwa ya wagombea, ikiwemo Arusha Mjini (wagombea 7), Dodoma Mjini (wagombea 8), Jimbo la Mtumba (wagombea 4), Busanda (wagombea 4) na Chato Kaskazini (wagombea 5).

CPA Makalla alisisitiza kuwa vigezo vya uadilifu, uwezo wa uongozi na kukubalika kwa wananchi vilitumika kuhakikisha chama kinapata wagombea bora watakaotekeleza kwa ufanisi Ilani ya CCM na kuendeleza kasi ya maendeleo ya Taifa.

Wagombea waliopitishwa sasa wanatarajiwa kuanza maandalizi ya kampeni rasmi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, huku chama kikiahidi kampeni za kistaarabu, zinazolenga masuala ya maendeleo kwa Watanzania wote.


Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment