LUIS Diaz anatarajiwa kujiunga na Bayern Munich baada ya mabingwa hao wa Ujerumani kuafikiana na Liverpool dili la thamani ya pauni milioni 65.5 ikijumuisha nyongeza.
Liverpool ilikataa ombi la awali la pauni milioni 58.6 kutoka kwa Bayern kwa mshambuliaji huyo wa Colombia mapema mwezi huu.
Diaz mwenye umri wa miaka 28, aliachwa nje ya kikosi cha Liverpool kilichofungwa 4-2 Jumamosi na AC Milan katika mechi ya kirafiki ya kujiandaa na msimu mpya huko Hong Kong, kwa sababu ya uvumi kuhusu mustakabali wake.
Alipewa ruhusa na Liverpool kurudi Ulaya kutoka Asia kukamilisha uchunguzi wa afya yake kabla ya kusaini mkataba.
Liverpool tayari imewasajili washambuliaji, Florian Wirtz na Hugo Ekitike msimu huu wa joto na wanamtaka Alexander Isak wa Newcastle United.
Diaz aliwasili Anfield akitokea FC Porto ya Ureno kwa ada ya awali wa pauni milioni 37 Januari 2022 na amefunga mabao 41 katika mechi 148, yakiwemo 13 wakati Wekundu hao wakishinda taji la Ligi Kuu England, msimu uliopita.
Mabao yake 17 katika mashindano yote msimu wa 2024-25 yalimfanya kuwa na msimu mzuri zaidi wa maisha yake ya soka.
Bayern walishinda taji lao la 34 la Ligi Kuu Ujerumani, Bundesliga, msimu uliopita na kufunga mabao 99, lakini waliondolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya robo fainali.
Diaz atatoa chaguo la safu ya ushambuliaji kutokana na Bavaria hao kumkosa fowadi wake, Jamal Musiala kwa kipindi kirefu baada ya kuvunjika mguu kwenye Kombe la Dunia la Klabu.
Tupe maoni yako

0 comments:
Post a Comment