ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, March 25, 2025

MSIGWA AKANUSHA TAARIFA ZA KURUDI CHADEMA.

 

Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Peter Msigwa amekanusha vikali taarifa zilizosambaa mitandaoni zikidai kuwa amerejea katika chama chake cha zamani, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). 

Uvumi huo umeenea kwa kasi kupitia mitandao ya kijamii, lakini baadaye Mbunge huyo wa zamani wa Iringa Mjini, alizikanusha rasmi.

KUPITIA AKAUNTI YAKE YA X ALIANDIKA:-

"Puuzeni uvumi wowote unaotengenezwa na kuenezwa dhidi yangu kuhusu mustakabali wangu wa kisiasa. Hakuna mtu niliyemteua kuwa msemaji wangu kwa mambo ya kisiasa. Msijibebeshe majukumu ya kunisemea huku mkijua ninao uwezo wa kujisemea mwenyewe. Ni kijani, kijani, I’m here to stay."

Akizungumza na Nipashe Digital kwa njia ya simu, Msigwa amesisitiza kuwa hana mpango wa kurudi CHADEMA, na kudai kuwa taarifa hizo ni njama za wapinzani wake wa kisiasa wanaotaka kumchafua ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

"Niliondoka nikiwa na akili yangu timamu, siwezi kurudi CHADEMA kamwe. Kile kilichosambazwa mitandaoni ni uzushi wa kutengeneza. Wanataka kuniharibia huku niliko," amesema Msigwa.

Alipoulizwa kama amewahi kuombwa kurejea CHADEMA, alikiri kupokea maombi kutoka kwa wanachama wa chama hicho, lakini akaweka wazi kuwa hatarudi.

"Ni kweli wanachama wa CHADEMA wananiomba sana nirejee, lakini siwezi kamwe kurudi tena huko," amesisitiza.

Hata hivyo, Msigwa amebainisha kuwa urafiki wake na Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Tundu Lissu, utaendelea, lakini hilo halimaanishi kwamba atarejea kwenye chama hicho.

Mchungaji Msigwa alihama kutoka CHADEMA na kujiunga na CCM mwezi Juni mwaka jana.



Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.