ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, February 19, 2025

TRA PWANI YATUMIA MIL. 15 KUSAIDIA SEKTA YA AFYA NA ELIMU KWA KUTOA MSAADA KWA JAMII

 


NA VICTOR  MASANGU, PWANI

Mamlaka ya mapato  Tanzania  (TRA) Mkoa wa Pwani imetumia kiasi cha shilingi milioni 15 kwa ajili ya kununua  vifaa na mahitaji mbali mbali  kwa ajili ya kutoa msaada kwa jamii pamoja na maeneo mbali mbali ikiwemo sekta ya afya pamoja na sekta ya elimu ikiwa ni moja ya kurudisha kwa jamii kwa kile ambacho wanakikusanya katika suala zima la  ukusanyaji wa mapato.


Meneja  wa TRA Mkoa wa Pwani  Masawa Masatu  ameyabainisha hayo wakati wa ziara maalumu ya  kwenda kutoa misaada mbali mbali kwa jamii ikiwa ni moja ya utekelezaji   wa Serikali ya awamu ya sita katika kuhakikisha kwamba wanaendelea kudumisha mahusiano mazuri  kwa jamii inayowazunguka  pamoja na walipa kodi.

"Kama tunavyofahamu serikali ya awamu ya sita kupitia kwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan imekuwa na kampeni maalumu kwa lengo la kuhakikisha kwamba TRA inakuwa na mahusiano mazuri na walipa kodi mbali  mbali na kwamba katika Mkoa wa Pwani tunatekeleza kampeni hiyo kwa vitendo ikiwa ni pamoja na kutoa msaada wa mahitaji mbali mbali.

Aidha Meneja huyo amebainisha kwamba wanatambua mchango mkubwa ambao unafanya na walipa kodi ambao wameweza kufanya vizuri katika kipindi cha mwaka wa 2023 na mwaka 2024 ikiwa sambamba na kuwashukuru kwa dhati wale walipa kodi wote ambao wamekuwa mstari wa mbele katika suala zima la ulipaji wa kodi.

  Pia amesema kwamba katika kampeni hiyo wameweza kutoa msaada wa vitu mbali mbali ikiwemo mifuko ya saruji katika zahanati ya misugusugu kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa wodi ya mama na mtoto, vifaa tiba mbali mbali katika kituo cha afya Mkoani, viti mwendo,taulo za watoto, kitanda katika Hospitali ya Kisarawe sambamba na kusaidia mipira  ya kuchezea katika shule msingi Mkoani kitengo cha elimu maalumu.

Kwa upande wake Mganga mfawidhi wa kituo cha afya Mkoani Abdulkadir Sultan ameishukuru kwa dhati TRA Mkoa wa Pwani kwa kuweza kutekeleza ahadi yake kwa vitendo ya kutoa misaada na mahitaji mbali mbali ambayo yataweza kuwa ni  mkombozi mkubwa katika suala zima la kuwahudumia wagonjwa.

Naye Mganga mfawidhi katika  Hospital ya Kisarawe Dkt. Yona Kabata  amesema kwamba msaada ambao wamepatiwa  na TRA ikiwemo kitanda maalumu  kwa ajili ya kujifungulia wakinamama utakuwa ni mkombozi mkubwa kwani hospitali hiyo bado inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa vitanda.

Afisa Elimu kata  ya Tumbi Inocensia Mfuru  amesema msaada ambao wamepatiwa  wa viti maalumu ni moja ya hatua kubwa katika  kuwasaidia watoto hao ambao walikuwa wanapata shida  katika kutembea hivyo kutaweza kuleta mabadiliko chanya katika kuboresha sekta ya elimu hasa kwa watoto wadogo.

Mamlaka ya mapato (TRA) Mkoa wa Pwani imetekeleza kwa vitendo maelekezo ya serikali ya awamu ya sita na kufanikiwa kutembelea katika Wilaya za Kibaha, Kisarawe, na Wilaya ya Kibiti na kukabidhi misaada mbali mbali ikiwemo, vitanda kwa ajili ya kujifungulia,  mifuko ya Saruji,vifaa tiba Vitimwendo , taulo za watoto  na mipira  ya kuchezea  vyote vikiwa na thamani ya kiasi cha shilingi milioni 15.


Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.