ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, February 21, 2025

TRA PWANI YAPAMBANA VIKALI YAFANIKIWA KUKUSANYA BILIONI 60.69 KWA WALIPA KODI WAO


 NA  VICTOR MASANGU, PWANI

Mamlaka ya mapato Tanzania  (TRA) Mkoa wa Pwani imepata mafanikio makubwa   kwa kipindi cha mwaka wa fedha wa 2023 /2024 baada ya kufanikiwa  kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 60.69 ikiwa ni sawa na kiwango cha utendaji wa asilimi 99.13 ambazo zimetokana na juhudi za kuwaelimisha wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiari bila shuruti.

Hayo yamebanishwa na Meneja wa  TRA  Mkoa wa Pwani  Masawa Masatu wakati wa hafla ya siku ya shukrani kwa mlipa kodi kwa mwaka 2023/2024  ambapo amesema kwamba matokeo hayo ya mafaniko yamekuja kutokana na watanzania wengi kuwa wazalendo na wamehamasika  kwa kiasi kikubwa katika suala zima la ulipaji wa kodi.

"Sisi kama Mamlaka ya Mapato Tanznaia (TRA) tumejitahidi sana katika kutoa elimu kwa wafanyabiashara wetu juu ya umuhimu wa kulipa kodi ndio maana tumeweza kufanikiwa  kwa kiasi kikubwa kukusanya kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 60 na kwamba watanzania wengi kwa sasa wamekuwa wazalendo kwani wanatambua umuhimu wa kulipa kodi ambayo inakwenda kuchangia kuleta maendeleo,"alisema Masatu.
Kadhalika ameongeza  kwamba  anatambua umuhimu mkubwa na mchango  ambao unafanywa na  baadhi ya wafanyabiashara katika suala la kulipa kodi  kwani ndio wamekuwa ni muhimili mkubwa katika kuchochea kasi ya maendeleo na kutekeleza miradi mbali mbali  katika nchi ya Tanzania.


"Tunatambua umuhimu mkubwa wa mchango wa walipakodi wetu na kwamba wamekuwa mstari wa mbele katika kulipa kodi zao kwa hiari na ndio maana  tumeamua kutambua umuhimu wao na kuwapatia vyeti ikiwa kama ni moja ya kuwapa motisha pamoja na kuweza kuwahimiza kuendelea kulipa kodi kwa wakati wakati  bila shuruti yoyote kwa maslahi ya wananchi wa Tanzania,"alisema Masatu.

Pia Masatu amempongeza kwa dhati Rais wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kuwa mzalendo na kutambua mchango wake mkubwa ambao anaufanya katika suala zima la kuhimiza ulipaji wa kodi kwa maslahi mapana kwa wananchi wa Tanzania ikiwemo pamoja na kuleta maendeleo katika nyanja mbali mbali.

Naye Mkurugenzi wa huduma na elimu kwa mlipa Kodi (TRA) Tanzania  Richard Kayombo amebainisha kwamba katika kipindi cha  mwaka wa fedha 2023/2024  wameweza kukusanya  ujumla trioni 27.64  ikiwa ni ukuaji wa wa asilimia 14.45% ukilinganisha na mwaka uliopita.

Kwa  upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Alhaj Abubakari Kunenge ambaye alikuwa mgeni rasmi katika halfa hiyo  ya mlipa kodi ameitaka TRA kuhakikisha kwamba wanakuwa wabunifu na kusimamia vizuri suala zima la ukusanyaji wa mapato ikiwa sambamba na kuweka mikakati ya kuwa na vyanzo vipya.

Naye Mwenyekiti wa  Jumuiya ya wafanya biashara Mkoa wa Pwani  Bundala Ndauka ameipongeza  Mamlaka ya TRA kwa  kuweza kuwapatia elimu mbali mbali juu ya umuhimu wa ulipaji wa kodi sambamaba na kuwawekea mazingira rafiki katika suala zima la utekelezaji wa majukumu yao.

Kauli mbiu  ya mwaka huu  katika  kilele cha maadhimisho ya siku ya shukrani kwa  mlipa kodi kwa kipindi cha mwaka 2023 /2024  inasema kwamba kodi yetu maendeleo yetu

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.