Na Oscar Assenga,TANGA
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Tanga kwa kushirikiana na (UMIVITA) wametoa elimu ya kodi kwa watu wenye ulemavu ili kuwaongezea uelewa.
Akizungumza wakati wa mafunzo ya elimu ya mlipa kodi kwa watu wenye ulemavu yaliyotolewa na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) Mkoa wa Tanga,Afisa Mkuu Msimamizi wa Kodi Kitengo cha Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano Tanga,Flavian Byabato alisema wameona watoe elimu hiyo ili kuweza kuwapa uelewa jamii hiyo.
Alisema kwamba wanatoa elimu hiyo ikiwa ni muendelezo wa mamlaka hiyo kuhamasisha ulipaji kodi kwa hiari na kutoa elimu ya kodi kwa wadau ili waweze kupata uelewa wa mambo yanayohusiana na kodi katika kuendeleza nchi .
Aidha alisema kwamba maendeleo yanafika kutokana na kulipa kodi hivyo wakaona ni muhimu washirikiane na chama hicho katika kutoa elimu ya kodi kwa manufaa yao na Serikali kwa ujumla.
Hata hivyo alisema kwamba elimu waliyoitoa ni pamoja na usajili wa biashara, kulipa kodi stahiki sambamba na hayo wamewajulisha haki ambazo wanazo katika masuala mbalimbali ya kodi ikiwemo kupewa taarifa na elimu ya kodi.
"Tunashukuru kwamba wameitikia vema na tunategemea kuwa huu ni mwanzo wa hatua ya kukamilisha wajibu wao, tunategemea watakuwa walipaji waziri wa kodi na kuweza kueneza hii elimu ambayo wameipata" amesema.
Awali akizungumza Mwenyekiti wa Umoja wa Miradi kwa Viziwi Tanzania (UMIVITA) alishukuru kwa mafunzo hayo huku akieleza baadhi ya watu wenye ulemavu mkoani humo wameshindwa kurejesha mikopo ya asilimia mbili inayotolewa na Serikali kutokana na kukosa elimu juu ya ufanyaji wa biashara
Alisema hivyo mafunzo hayo wameyapata wakati muafaka na yatawaongezea maarifa ya kuwa na kuona umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari ili kuchochea ukuaji wa maendeleo nchini.
Amesema mikopo hiyo ni mzuri na inawasaidia sana katika kuendesha biashara zao na kujikwamua na umasikini, ambapo wengine wanafanikiwa kurejesha na baadhi kushinda huku wakiishia hata kuhama makazi yao.
Mwenyekiti huyo amebainisha kwamba elimu waliyopata itawanufaisha kutokana na awali hawakuwa na uelewa kuhusu masuala mbalimbali yanayotokana na ulipaji wa kodi hivyo wamepata mwanga mpya.
Kwa upande wake Katibu wa Shirikisho la watu wenye ulemavu Mkoa wa Tanga (SHIVIAWATA) Subira Hoza amesema kabla ya kupata elimu hiyo watu wenye ualbino Mkoa walikuwa wanafahamu kuhusu elimu ya mlipa kodi kwa asilimia 30.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.