Baada ya mabaki ya mwili wa Josephine Mngara (27), mkazi wa Mtemboni, Mji mdogo wa Himo, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro kukaa Mochuari kwa siku 190 sasa familia yake imekabidhiwa mabaki ya mwili huo na kwenda kuyazika katika makaburi ya Mereseni yaliyopo katika Mji mdogo wa Himo.
Mwanamke huyo ambaye aliyekuwa akiishi na mpenzi wake Mtaa wa Mtemboni wilayani hapa inadaiwa kuuawa kikatili na mpenzi wake usiku wa kuamkia Februari 19, mwaka huu kwa kile kinachodaiwa ni wivu wa mapenzi.Februari 23, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kisare Makori aliiambia Mwananchi kuwa usiku wa kuamkia Februari 19 kuna mwili ulikutwa umechomwa moto na kutelekezwa kwenye pagale ambapo polisi katika kuchunguza walikuta michirizi ya damu kutoka nyumba jirani kuelekea eneo ambalo mwili ulikokutwa umeungulia.
Alisema mabaki ya mwili huo, ikiwemo mifupa na sehemu nyingine imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) kwa ajili ya taratibu nyingine za kiuchunguzi ikiwemo vipimo vya vinasaba (DNA) ambavyo vilipelekea kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kujiridhisha na mabaki ya mwili yaliyokutwa eneo la tukio.
Hata hivyo, siku chache baadaye wakati Jeshi la Polisi likimsaka mtuhumiwa huyo, alituma ujumbe mfupi wa maneno (sms) kwa mama mkwe wake, Theodora Msuya, mama mzazi wa binti huyo akiomba radhi na kusema roho ya yake inamuuma kwa kujihusisha na mauaji hayo.
"Mama samahani sio kosa langu, nilimkuta ...na mke wangu kwangu nikavunja mlango tukaaza kupigana na ... mimi nikashika panga na yeye akachukuwa mpini wa jembe akawa anarusha nikakwepa ndiyo akampiga mke wangu mpaka chini, akanipa nauli akanambia sepa niachie mimi ataua mtu, mulize (...) mama mimi sijui roho yangu inauma sana mchana mwema," ilisomeka meseji hiyo kwenye simu ya mama mkwe.
Hata hivyo, Mei 18, mwaka huu baada ya miezi mitatu kupita Jeshi la Polisi Mkoani hapa lilifanikiwa kumtia mbaroni Erasto Gabriel (31) mkazi wa Mtemboni aliyekuwa akiishi na mwanamke huyo (marehemu) kwa madai ya kuhusika na mauaji hayo.
Mama wa marehemu, Theodora Msuya amesema tukio hilo limewaumiza sana familia na ameacha pengo kubwa kwa familia na kwamba marehemu amemwachia watoto wanne wadogo na kwamba hajui atawalea vipi kwa kuwa maisha yake ni duni.
"Tunamshukuru Mungu tumezika mabaki ya mwanangu lakini hili tukio limetujeruhi sana maana hata sijui pakuanzia, mwanangu kaniachia watoto wanne wadogo na hata sijui nawaleaje maana sina uwezo hapa nilipo," amesema.
Mama huyo ameiomba serikali kupitia mamlaka zake kuitendea haki familia hiyo ikiwemo kumchukulia hatua za sheria aliyehusika na mauaji ya mwanaye.
Anna Juma, ambaye ni dada wa marehemu ameziomba mamlaka zinazohusika kumchukulia hatua kijana huyo kwa kukatisha uhai wa ndugu yake ili iwe ni fundisho kwa vijana wengine.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.