Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa |
"Hakuna mtoto aliyefufuka" ndiyo kauli aliyoitumia Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa kuelezea majibu ya uchunguzi wa tukio la mtoto, Mabirika Wilson (8) kudaiwa kufariki, kuzikwa kisha kuonekana akizurura kwenye majaruba yaliyoko kijiji cha Mwangika Wilaya ya Kwimba mkoani humo.
Mtoto huyo ambaye
ni Mkazi wa Kijiji cha Salong'we Wilaya ya Magu mkoani Mwanza alifariki Aprili
16 mwaka huu nyumbani kwao baada ya kuugua maradhi yanayodhaniwa kuwa ni homa
na kuzikwa nyumbani kwao Aprili 17 mwaka huu.
Siku 13 baada ya
maziko ya mtoto huyo, Jeshi la Polisi mkoani humo lilitoa taarifa ya kuibuka
sintofahamu kuhusu kifo cha mtoto huyo kufuatia wazazi wa Mabirika, Wilson
Bulabo (35) na Helena Robert (32) kudai kwamba mtoto aliyeokotwa ni wao jambo
lililoibua taharuki na kuwalazimu polisi kufukua kaburi ili kuchukua sampuli
kwa ajili ya kipimo cha Vinasaba (DNA).
Akizungumza na
Waandishi wa habari leo Jumamosi Mei 5, 2023 Kamanda Mutafungwa amesema
uchunguzi wa awali wa vinasaba uliofanyika kwa watu wanne wakiwemo wazazi, babu
wa marehemu na mtoto aliyeokotwa umeonyesha wazazi hao wa marehemu Mabirika
hawana Unasaba (uhusiano) na mtoto aliyeokotwa katika kijiji cha Mwangika bali
wazazi hao walitaka kumuiba.
"Uchunguzi
wa Vinasaba tulioufanya kwa mtoto aliyeokotwa tumebaini siyo mtoto wa wazazi
hao badala yake mtoto wao ni aliyefariki. Hivyo, tunawashikilia wazazi hao
ambao walidanganya na kuzua taharuki kuwa mtoto aliyeokotwa ni wa kwao
amefufuka tukikamilisha uchunguzi tutawafikisha Mahakamani kwa tuhuma za kuibua
taharuki na kutaka kuiba mtoto," amesema Mutafungwa
Kuhusu mtoto
aliyeokotwa, Mutafungwa amesema baada ya kumfanyia mahojiano chini ya usimamizi
wa Ofisi ya Ustawi wa Jamii amejitambulisha kwa jina moja la Mussa (8) huku
akiwaomba wazazi ambao mtoto wao amepotea kufika Kituo Kikuu cha Polisi mkoani
humo kwa ajili ya kumtambua mtoto huyo.
Kwa upande wake,
Mwenyekiti wa Kijiji cha Salong'we, Geremanus Masala amewataka wakazi wa mkoa
huo kuacha kuzusha taarifa za imani potofu na kishirikina kuwa mtu akifa
anaweza kufufuka jambo linaloweza kuzua taharuki kwa Umma.
"Nitawafikishia
ujumbe wakazi wa kijiji changu cha Salong'we kuachana na imani potofu, watambue
kuwa mtoto huyu siyo aliyefariki na pia tunaenda kukemea imani potofu,"
amesema Masala
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.