ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, February 9, 2023

KAULI YA DKT MWIGULU ‘UGANGA WA KIENYEJI’ YAFUTWA KWENYE KUMBUKUMBU ZA BUNGE.

Dodoma. Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amefuta katika kumbukumbu rasmi za Bunge kauli iliyotolewa na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba kuhusu wabunge kumuacha ajadili masuala ya uchumi na wao wajadili uganga wa kienyeji.


Dk Tulia ameyasema hayo leo Alhamis Februari 9, 2023 wakati akijibu utaratibu uliombwa na Dk Mwigulu wakati Mbunge wa Tandahimba (CCM) Katani Katani akichangia taarifa za kamati Februari 7, 2023.


Wakati akichangia taarifa za shughuli za Kamati wiki iliyopita Dk Mwigulu, alisema “Embu tujadili mambo mengine yanayohusu uganga wa kienyeji kwenye uchumi this is my profession (hii ni taaluma yangu), mnajadilije vitu ambavyo viko wazi”


Hata hivyo, Februari 7, 2023, Katani akichangia taarifa ya shughuli ya Kamati ya Hesabu za Serikali, (PAC) alisema kuwa waziri huyo amewatukana wabunge.


“Tunakwenda wapi. Mwigulu (Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba) umetutukana wabunge sana na unapaswa utafakari utakapokaa. Hakuna anayeweza kujadili waganga wakienyeji hapa. Haya tunayoyajadili ni maisha ya Tanzania na tumeletwa bungeni na Watanzania hata Iramba wanataka uwasaidie,”alisema Katani.


Kauli hiyo ilimfanya, Dk Mwigulu kuomba utaratibu ambapo alisema kanuni za Bunge zinazuia kusema uongo na mbunge anapojulisha Bunge kwamba yeye ametukana wabunge ni tuhuma kubwa.


“Bunge lako haliruhusu, mimi nisingeweza kutukana wabunge na kiti kikiwepo pamoja aepuke kuwajumuisha,”alisema Dk Mwigulu.


Akijibu kuhusu suala hilo, Dk Tulia amesema ni kweli Dk Mwigulu alitamka kauli hiyo bungeni, iliyowafanya baadhi ya wabunge kuirejea kwa mtazamo hasi.


Mbunge Katani afoka Bungeni "ulitutukana sana Wabunge" akimuunga Mpina ishu ya Bashe na Mwigulu

Hata hivyo, amesema kanuni ya Bunge ya 71 inataka wabunge kutumia lugha ya staha wakati wakiwa bungeni.


“Wabunge wakati mwingine tukichangia hatuendi na hoja bali mtu na yeye waziri ama naibu analazimika kwenda kwa mtu badala ya hoja. Kila upande ufanye kulingana na kanuni kuchangia kuhusiana na hoja na si mtu binafsi,”amesema.


Amesema lengo hasa la Dk Mwigulu lilikuwa ni kumjibu Mbunge wa Kisesa (CCM) Luhaga Mpina lakini baada ya maelezo mafupi baadaye akajikuta anasema kwa Bunge zima.


Amesema Katiba inalinda uhuru wa majadiliano na maoni ili mbunge aweze kuihoji Serikali na kuisimamia lakini kwa kuwa maneno yaliyosemwa na Dk Mwigulu yameendelea kusemwa bungeni ameagiza yafutwe kwenye kumbukumbu rasmi za Bunge.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.