ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, January 17, 2023

MWENYEKITI JUMUIYA YA WAZAZI MKOA WA PWANI AWAFUNDA WANACHAMA KUFUATILIA UTEKELEZAJI WA MIRADI.


Na Victor Masangu,Pwani


MWENYEKITI Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Pwani Jackson Kituka amesema ni jukumu la wanachama wa chama hicho kujiandaa kuelezea wananchi kwenye mikutano ya hadhara kuhusiana na utekelezaji wa miradi mbalimbali uliofanywa na Serikali. 


Kauli hiyo ameitoa wakati alipokuwa akizungumza katika  Baraza la Jumuiya hiyo lililofanyika Kibaha ambapo alisema baada ya kuruhusiwa mikutano ya hadhara yapo mambo mengi yatasemwa na vyama vingine hivyo chama tawala kinatakiwa kujiandaa kujibu kwa vielelezo.


"Inabidi kufika kwenye ofisi za Wakuu wa Wilaya mkapate taarifa za miradi iliyotekelezwa na Serikali ambayo imetatua kero za wananchi, msinyamaze kimya Serikali ikishambuliwa" alisema.


Aidha alisema viongozi waliochaguliwa hivi karibuni wanatakiwa kufanya kazi  kwa ushirikiano na kuepuka migogoro itakayosababisha baadhi ya majukumu kutofanyika kwa ufanisi.


" Sitaki kuwa mwenyekiti wa migogoro kaeni mfanye kazi vizuri jiandaeni kujibu yale yatakayokuwa yanasemwa vibaya kwenye mikutano ya hadhara mkiwa na takwimu ya kila eneo nini kimefanyika na fedha zilizotumika mkajibu pale mnapoona kuna upotoshaji" alisema 

Awali Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Pwani Elisante Msuya  akizungumza kwenye Baraza hilo alisema wajumbe kutoka katika wilaya za mkoa huo wameshiriki katika baraza hilo la siku mbili ambalo liliambatana na kuchagua wajumbe kamati ya Utekelezaji.


Msuya alisema wajumbe wa Baraza walipata fursa ya kupatiwa semina ya Mazingira, changamoto za mazingira zinazoukabili mkoa wa Pwani, Sera ya elimu, Sera ya Malezi na changamoto za kimalezi kwa mkoa huo.


Alieleza kuwa baada ya Baraza hilo wajumbe watakwenda kusimamia yale waliyojifunza kwa kuhakikisha utunzaji mazingira unaimarika pamoja na malezi ya watoto ikiambatana na kuhamasisha jamii ya mkoa huo kujenga tabia ya kuwa karibu na watoto wao kusimamia maadili yao na kuipa elimu kipaumbele.


Katika Baraza hilo Selina Koka alichaguliwa kuwa mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Pwani pamoja na Judith Muluge, Hemed Salim na Dk. Michael Benedict.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.