Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Iringa ACP Allan Bukumbi akiongea na waandishi wa habari juu ya matukio mbalimbali ambayo yametokea katika mkoa huo
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Iringa ACP Allan Bukumbi akionyesha silaha aina ya mapanga ambayo hutumiwa na waalifu
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Iringa ACP Allan Bukumbi akionyesha silaha aina ya bunduki ambazo hutumiwa na waalifu.
Na Fredy Mgunda, Iringa.
JESHI la polisi mkoa wa Iringa kwa kushirikiana na Askari wa Uhifadhi kutoka hifadhi ya Taifa Ruaha wanamshikilia Cyprian Kasula miaka 42, mkulima na mkazi wa kijiji cha Kipera kwa tuhuma za kukutwa na Kichwa cha Tembo kikiwa na meno yote mawili katika hifadhi ya Taifa ya Ruaha.
Akizungumza na waandishi wa habari Iringa, Kamanda wa polisi mkoa wa Iringa ACP Allan Bukumbi alisema kuwa wanamshikilia Cyprian Kasula miaka 42, mkulima na mkazi wa kijiji cha Kipera akiwa na Kichwa cha Tembo kikiwa na meno yake mawili,Nyama ya Tembo,Mkia wa Tembo,Silaha tatu za kienyeji aina ya Gobore,Vipande vya nondo 35,makopo matatu ya unga wa baruti na Panga moja.
ACP Bukumbi alisema kuwa mtuhumiwa huyo alikutwa amekaa porini chini ya mti pamoja na mwenzake mmoja ambaye alifanikiwa kukimbia baada ya kuona Askari wamefika eneo hilo na juhudi za kumtafuta zinaendelea.
Kamanda wa polisi mkoa wa Iringa alisema kuwa Agnes Chaula miaka 38, mama lishe na mkazi wa Mwangata D kwa tuhuma za kukutwa na vipande vitano vya meno ya Tembo.
ACP Bukumbi alisema kuwa Mama lishe huyo anatuhumiwa kujihusisha na uwindaji haramu na taratibu za kumfikisha Mahakamani zinaendelea.
Alisema kuwa jeshi la polisi mkoa wa Iringa linamshikilia Christina Mponzi, miaka 34, mkulima na mkazi wa Kihesa akiwa na Madawa ya kulevya yanayodhaniwa kuwa ni Heroine kete 33, mtuhumiwa alikutwa ameweka kete hizo kwenye mkoba baada ya kufanyiwa upekuzi aligundulika kuwa na hayo na anashikiliwa kwa ajili ya upelelezi zaidi na kielelezo kimehifadhiwa kituoni.
Katika hatua nyingine Jeshi la polisi mkoa wa Iringa linamshikilia Gwelino Mwanzasi miaka 91, mkulima wa Image mkazi wa kijiji cha Kilangali Kata ya Image Tarafa ya Mazombe Wilaya ya Kilolo kwa kukutwa na Silaha nne aina ya Gobore na Shortgun moja,Gololi za Gobore thelathini,Risasi za Shortgun nne,Risasi za G3 tatu,Risasi ya Rifle 404 moja,Ganda la risasi Rifle 375 moja,Baruti ujazo wa nusu lita pamoja na Jino la kiboko moja,Kipande cha ngozi ya Nyati kimoja naGamba la kakakuona moja.
Kamanda polisi mkoa wa Iringa ACP Allan Bukumbi alimazia kwa kusema kuwa wanamshikilia Raymond Mgao miaka 28, mkulima wa kijiji cha Mapogoro na Brown Sangwa kwa kukutwa na Meno ya Tembo mazima sita baada ya kuwekewa mtego ambapo watafikishwa Mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
Jeshi la Polisi mkoa wa Iringa kuelekea kwenye sikukuu za mwisho wa mwaka tutaendelea kufanya misako na operesheni ya nguvu zaidi ili kudhibiti uhalifu wa kijinai na ajali za barabarani na walitoa wito kwa wakazi wote wa mkoa wa Iringa kujiepusha na vitendo vya kihalifu kuelekea sherehe za sikukuu za mwisho wa mwaka.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.