Dodoma. Mbunge wa Kisesa, Luhwaga Mpina (CCM) kwa mara nyingine ameendeleza moto wake bungeni kuhusu malimbikizo ya kodi zaidi ya Sh360 trilioni zinazotajwa kuwa zinatokana na makinikia.
Jana Jumatano Novemba 2, Mpina amesema ni wakati sasa Watanzania kujua nani alitoa kauli ya kusamehe kodi hiyo kwa nchi masikini kama Tanzania ambayo inahitaji kodi ili iweze kupanga maendeleo.
Katika mchango wake alijikita kwenye taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) akiuliza mambo matatu ambayo ni deni la Taifa ambalo hata hivyo hakulizungumzia zaidi, kodi ya makinikia na uhamishaji wa bidhaa na mauzo.
“Lakini kingine ninajiuliza nani aliruhusu Serikali kulipa kampuni ya Symbion kiasi cha Sh350 bilioni kwa haraka bila kuidhinishwa na Bunge wakati kampuni hiyo inadaiwa mabilioni mengi na Serikali lakini ghafla fedha hizo zililipwa bila kujua zilitoka mfumo upi na kwa ruhusa ya nani,” amehoji Mpina.
Mpina ameitaka Serikali kueleza wazi nani waliosababisha serikali kuingia hasara hiyo kwenye mkataba na kwa nini hawatajwi na hatua gani zichuliwe.
Hoja nyingine ameuliza ni kwa nini Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inashindwa kukusanya malimbikizo ya kodi ya Sh7.54 trilioni ambazo hazina kesi mahakamani na kati ya hizo Sh3.87 trilioni ni za mwaka mmoja wa 2020/21.
Kuhusu mikopo ya asilimia 10 katika mapato ya halmashauri amesema kumekuwa na kichaka cha kula fedha badala yake mfumo ubadilishwe ili kusudi zianze kukopeshwa kwa njia ya kupitia mabenki ili waweze kuzifuatilia.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.