ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, November 3, 2022

HIZI NDIZO SABABU KWA RAIS SAMIA KUJA NA MJADALA WA KUSAKA NISHATI YA KUPIKIA

  Katika nchi nyingi za kusini mwa janga la Sahara, njia kuu ya kupika ni kwa kutumia mkaa, kuni na mafuta ya taa.


Kwa mujibu wa shirika la Clean cooking aliance Watu milioni 950 wanategemea kuni na mkaa kupikia, idadi inayokadiriwa kukua hadi bilioni 1.67 ifikapo 2050.


Njia hizi za kupikia hutumiwa sana kutokana na kuwa nafuu kwa familia nyingi za kipato cha chini.


Katika meneo ya mjini na vijijini, ni kawaida kukuta majiko ya kupikia yenye mkaa kwenye makazi yao.


Lakini njia hizi za kupikia huwa na madhara ya muda mrefu ya kiafya kwa mujibu wa wataalamu.


Kuna athari za kiafya kwa wazalishaji wa mkaa na watumiaji. Mkaa kimsingi ni kaboni tupu, na mkaa unaochomwa hutoa viwango vya juu vya kaboni dioksidi, kaboni monoksidi, na vichafuzi kama vile masizi, ambavyo vinaweza kuingia ndani kabisa ya mapafu, hasa katika majiko yasiyokua na sehemu za kutolea hewa ya kutosha.


Uzalishaji huu unaweza kuwa na madhara sana, kwa mujibu wa shirika la afya duniani WHO karibu watu milioni 4 kote ulimwenguni hufa kabla ya wakati kila mwaka kutokana na kupikia kwa moto na nishati ngumu kama mkaa.


 Watafiti wanaongeza kuwa huenda athari ikawa kubwa zaidi kutokana na kutokua na takwimu za kutosha katika nchi hizi za kusini mwa janga la Sahara.


Athari za  kiafya

Matumizi ya mkaa na kuni hutoa moshi ambao huleta madhara kwa binadamu


 Kwenye Kuni na mkaa pia hutoa chembembe ndogo ambazo huweza kupenya katika njia ya hewa na kuleta athari kiafya


 Na pia hewa ya Kaboni monoksidi inayotolewa na mkaa na kuni huweza kuingia mwilini na kupenya hadi kwenye damu kisha inaanza kuondoa hewa ya oksijeni kwenye damu, na kusababisha madhara ya muda mrefu na hata kifo kama itaingia kwa wingi.


Kaboni monoksidi, oksidi za nitrojeni, oksidi za sulphate na misombo mingine tete inayotolewa wakati wa usindikaji na uchomaji wa mkaa inaweza pia kusababisha matatizo ya kupumua na hatimaye magonjwa kama vile maambukizi yanjia ya hewa (ARI), ugonjwa sugu wa mapafu (COPD), pumu, saratani ya mapafu au kwa wajawazito kujifungua watoto wenye uzito wa chini.


 ‘’Mkaa na kuni kwa ujumla inaweza kuathiri njia ya hewa na damu lakini mtu akishapata matatizo ya njia ya hewa kutokana na matumizi ya mkaa na kuni, inakua chanzo cha matatizo mengine ya kiafya kama moyo, unakuta mgonjwa moyo umefeli lakini sababu inakua ni matatizo yanatokana na shida ya mapafu ambayo imesbabishwa na matumizi ya mkaa na kuni''. anasema Dkt. Elisha Osati, Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani.


Mbali na athari za ndani ya mwili, matumizi ya mkaa hususani unaotokana na kuni huweza kuathiri macho kutokana na moshi na chembembe zinatolewa.


''Katika maeneo mengi ya vijijini wanatumia sana kuni kupikia pamoja na mkaa, ule moshi mara nyingi husababisha macho kuathiriwa na mwisho yanakua na rangi nyekunduna wakati mwingine mtu anaweza kushindwa kuona''. anasema dokta Osati.


Kaboni monoxide

Kaboni monoxide (CO), ni gesi isiyo na harufu na isiyo na rangi, na ni gesi yenye sumu ambayo inaweza kukufanya mgonjwa sana ukiipumua.  Inaweza kutengenezwa kwa moto na vifaa vinavyochoma gesi, kuni, mafuta au makaa ya mawe.


 Katika majiko ya kupikia yenye sehemu ndogo za kutolea hewa, mkaa unaweza kutoa viwango vya sumu vya kaboni Monoksidi (CO). Kiasi cha kidogo tu cha mkaa wa kupikia kinaweza kuzalisha viwango vya sumu ya CO.


''Kaboni monoxide ikiingia kwenye damu inaweza kuondoa oksijeni kwenye damu na ikakaa yenyewe na ikiingia kwa wingi huweza kusababisha kifo, na madhara yake ya muda mrefu yapo'' Anaongeza dkt. Osati.


Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali watu hufa kila mwaka kutokana na sumu ya kaboni monoksidi wanapochoma mkaa katika maeneo yaliyofungwa kama vile nyumba zao, kwenye kambi au magari ya kubebea watu, au kwenye mahema. Baadhi ya waathiriwa wanakufa kutokana na sumu ya kaboni monoksidi baada ya kuchoma mkaa kwenye hema la chumbani au kambi ili kupata joto.


Nini cha kufanya?

Jamii nyingi barani Afrika hutumia mkaa na kuni kama njia kuu ya kupikia vyakula. Kuacha kabisa matumizi ya mkaa huenda isiwe jambo la uhalisia kwa sasa wakati maeneo mengi hasa ya vijijini hayajafikiwa na teknolojia mbalimbali za majiko ya kisasa.


Hakikisha unapikia na mkaa katika eneo lenye hewa ya kutosha katika nchi nyingi zilizoendelea matumizi ya mkaa kupikia si makubwa, na hufanywa nje maeneo ambayo yana hewa ya kutosha.


Lakini nchi zinazoendelea ni ngumu bado kuepuka matumizi ya mkaa. Kama jiko lako lina dirisha dogo, basi wataalamu wanashauri kupikia nje, eneo la wazi, lenye hewa ya oksijeni ya kutosha.


"Usijaribu kupika na mkaa ndani ya nyumba - haijalishi unafikiri nyumba yako ina hewa ya kutosha kiasi gani," anasema Nicole Rodriguez, RDN, mtaalamu wa lishe na mkufunzi wa kibinafsi anayeishi New York. "Kwa kweli, Tume ya Usalama wa Bidhaa za Wateja inaonya dhidi ya hata kuhifadhi jiko ndani ya nyumba lenye mkaa uliomaliza kutumia"


Kutafuta mbadala wa kuni na mkaa

Teknolojia imeweza kusaidia mapinduzi ya matumizi ya mkaa na kuni katika maeneo mengi duniani, lakini barani Afrika, hususani kusini mwa janga la Sahara bado kuni na mkaa ni njia nafuu kwa familia nyingi


Njia mbadala za mkaa ni pamoja na majiko yanayotumia umeme, gesi ya petroli iliyoyeyuka (LPG), ethanoli, majiko ya gesi yenye ufanisi kwa kutumia biomass (yaani, pellets) na biogas. Aina mbalimbali za teknolojia za kibunifu zinapatikana pia ili kuongeza ufanisi, uwezo wa kumudu, na upatikanaji wa nishati hizi mbadala.


Ingawa mtazamo wa sasa wa biashara ya mkaa na matumizi yake yalyozoeleka si mazuri kwa Afrika hususani Kusini mwa Jangwa la Sahara, bara hili lina uwezo mkubwa wa kutumia nishati safi.


Kwa msaada kutoka kwa serikali, mashirika ya kiraia, na wajasiriamali wa sekta binafsi kupitia kupitishwa kwa kiwango cha nishati ya jua na njia nyingine mbadala za mkaa kunaweza kusababisha mamilioni ya maisha kuboreshwa na maelfu ya jamii safi na zenye afya.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.