ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, October 25, 2022

PPROFESA MKENDA ASEMA WANAFUNZI SABA WALIBADILISHIWA NAMBA ZA MTIHANI.

 


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema kuwa ni kweli mwanafunzi wa Shule ya Chalinze Modern Islamic Pre and Primary, Iptisum Slim pamoja na wanafunzi wengine sita walibadilishiwa namba ya mtihani katika mtihani wa taifa wa darasala saba.

Profesa Mkenda amebainisha hayo leo Jumanne Oktoba 25, 2022 akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

“Uchunguzi uliofanywa na Kamati ya Uendeshaji Mitihani ya Mkoa wa Pwani kwa kushirikiana na wataalamu wa maandishi kutoka Jeshi la Polisi (Forensic Bureau) umebainika jumla ya watahiniwa saba walibadilishiwa namba za mtihani katika kituo cha mtihani namba PS1408009 shule ya Awali na Msingi Chalinze Modern Islamic” amesema Profesa Mkenda


Uchunguzi huo ulifanywa baada kusambaa kwa video katika mitandao ya kijamii ikimuonesha mtahiniwa Iptisam Suleiman Slim wa kituo cha mtihani cha shule ya Awali na Msingi Chalinze Modern Islamic akieleza kwamba, alibadilishiwa namba yake ya mtihani wakati akifanya Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE) uliofanyika Oktoba 05 na 06/10/2022.

Profesa Mkenda amesema kuwa baada ya kupata taarifa hiyo Serikali kupitia Baraza la Mitihani ilielekeza Kamati ya Uendeshaji Mitihani ya Mkoa wa Pwani kufanya uchunguzi kuhusu malalamiko ya mtahiniwa na kuwasilisha taarifa Baraza la Mitihani.

Amesema kuwa uchunguzi uliofanyika pia umebaini kuwa mwanafunzi huyo pamoja na wanafunzi wengine sita walibadilishiwa namba ya mtihani katika mtihani wa taifa wa darasala saba.

“Mtahiniwa Iptisam Suleiman Slim alifanya masomo matano kwa kutumia namba PS1408009/0040 na somo la sita (mwisho) kwa kutumia namba PS1408009/0039 na Watahiniwa wengine wanne pia walibadilishiwa namba katika somo la sita katika kituo hicho,” amesema.

Profesa Mkenda pia amesema Shule ya Chalinze Modern Islamic Pre and Primary iliyoko mkoani Pwani imefungiwa kuwa kituo cha mtihani kwa muda usiojulikana.


Vilevile, Profesa Mkenda ameagiza watumishi waliohusika na udanganyifu katika mtihani wa darasa la saba Shule ya Chalinze Modern Islamic Pre and Primary kuchukuliwa hatua.

Pia, Profesa Mkenda ameiagiza Necta kumefanya marekebisho ya namba za mitihani za watahiniwa husika ili kila mtahiniwa aweze kutunukiwa matokeo yake halali.

“Nisisitize kuwa shule yoyote itakayobainika kufanya vitendo vya udanganyifu wa mitihani, itafungiwa na hata kufutwa kabisa kuendesha shughuli za elimu nchini,” anasema.


Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.