Mkuu wa wilaya ya Muheza Halima Bulembo kulia akiwa na Mkuu wa hifadhi wa shamba la miti Lunguza Ellyneema Mwasalanga katikati wakikabidhi msaada huo |
Na Oscar Assenga,Muheza
SERIKALI wilayani Muheza Mkoani Tanga imepiga marufuku shughuli za kibinadamu ikiwemo ukataji wa miti katika maeneo ya Hifadhi ya Msitu wa Miti wa Lunguza huku ikieleza haitasita kuwachukulia hatua watakaokaidi.
Marufuku hiyo ilitangazwa na Mkuu wa wilaya ya Muheza Halima Bulembo wakati akipokea msaada wa vifaa vya ujenzi na vifaa tiba kwa baadhi ya taasisi na shule zilizopo jirani na shamba hilo vyenye thamani ya zaidi ya Milioni 10.
Akitangaza mkakati huo baada ya kupokea vifaa hivyo alisema kuwa ukataji miti hovyo, uchimbaji wa madini ikiwemo na uchomaji misitu vinasababisha madhara ya kimazingira ikiwemo uhaba wa mvua,hivyo ni muhimu Wananchi wakahifadhi mazingira ya msitu huo .
Aliwataka wananchi wanaoishi jirani na msitu huu kushirikiana katika kuhakikisha kunakuwa na usimamizi na matumizi endelevu ya raslimali za misitu ili uweze kuwa endelevu ikiwemo waweze kunufaika na msitu huu
Awali Mkuu wa hifadhi wa shamba la miti Lunguza Ellyneema Mwasalanga amesema kuwa wametoa msaada huo ikiwa ni sehemu ya kurudisha Kwa jamii katika kusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo
Alisema kwamba wameweza kutoa msaada wa saruji mifuko 240,viti na meza 40,vifaa tiba 12 vyenye thamani ya sh Mil 2.5 kwa ajili ya zahanati ya kwafungo ambavyo vyote vina thamani ya sh Mil 10.1.
Alisema faida nyengine ambazo wanazipata wananchi ni kilimo mseto (taungya) ambapo wananchi huruhusiwa kulima katika maeneo yaliyo andaliwa kwa ajili ya kupandwa au yaliyopandwa yenye miti midogo kwa utaratibu maalumu.
Aidha alisema sambamba na hayo wananchi wananufaika na malighafi za kujengea (nguzo,fito) ajira katika maeneo mbalimbali ikiwemo kazi za kuhudumia shamba,uvunaji ,usafirishaji, uchakataji wa malighafi viwandani na kukua kwa biashara mbalimbali katika maeneo ya Muheza.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.