ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Sunday, April 10, 2022

RAILA AKWAA KISIKI AZIMIO LA UMOJA.

 

Mgombea urais mtarajiwa kwa tiketi ya Azimio la Umoja na One Kenya Alliance (OKA), Raila Odinga amekwaa kisiki na kulazimika kuweka gia ya kurudi nyuma ili kutii msimamo wa vyama washirika.


Vyama vinavyounda Azimio la Umoja na OKA, vilimgomea Raila kuhusu sera yake ya kugawa nchi kwa pembe, hivyo kumfanya arudi nyuma ili kufanya mashauriano ya pamoja kabla ya kuendelea na safari ya kampeni.


Raila alifanya uamuzi wa kusalimu amri kwa vyama washirika wa Azimio la Umoja Alhamisi (juzi), baada ya kumaliza kikao cha pamoja na viongozi wote wa muungano huo, uliofanyika makao makuu ya kampeni za Raila, Lavington, Nairobi.


Pamoja na kukubali kuaihirisha sera yake ya kugawa nchi kwa pembe ili kungoja mashauriano, vilevile Raila alikubali kupokea ushauri kabla ya kuteua mgombea mwenza.


Kwa sasa, mvutano ni mkubwa kuelekea uteuzi wa mgombea mwenza kwa sababu ndani ya Azimio la Umoja na OKA, baadhi wanapendekeza ‘patna’ wa Raila atoke Mlima Kenya ili kujenga ushawishi mkubwa eneo hilo.


Mlima Kenya ni eneo la kimkakati katika Uchaguzi Mkuu Kenya unaotarajiwa kufanyika Agosti 9, mwaka huu. Tathmini mbalimbali zimeonyesha kuwa mgombea atakayezoa kura nyingi Mlima Kenya, atakuwa na nafasi kubwa ya kushinda urais.


Changamoto iliyopo ndani ya ushirika wa vyama vya Azimio la umoja na OKA ni kuwa Kalonzo Musyoka ambaye ni kiongozi wa chama cha Wiper, alisimama kama mgombea mwenza wa Raila kwenye Uchaguzi Mkuu 2013 na 2017, hivyo naye anapigiwa chapuo. Hata yeye ameshajitangaza.


Kuhusu kukwama kwa sera ya kugawa nchi kwa pembe, vyama vidogo ndani ya Azimio la Umoja na OKA, vilikataa mpango huo wa Raila kwa hoja kwamba “wao wadogo wangeumia mbele ya wakubwa”.


Utetezi wa vyama vidogo ni kuwa endapo sera ya Raila ya kugawa nchi kwa pembe itatimia, vyama vitakavyonufaika zaidi ni Jubilee kinachoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta, Wiper cha Kalonzo na Orange Democratic Movement (ODM) cha Raila.


Kutokana na mvutano huo ndani ya Azimio la Umoja, sasa Katibu Mkuu wa zamani wa chama cha Jubilee, Raphael Tuju ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Sekretarieti ya Azimio, ndiye atasimamia mpango wa ugawaji nchi kwa pembe kwa mtindo ambao utakinufaisha kila chama mshirika.


Msemaji wa kampeni za Raila, Makau Mutua Alhamisi iliyopita alisema kuwa kiongozi wa ODM alikutana na mabosi wote wa vyama vyenye ushirika kwenye Azimio, ili kuweka sawa suala la masilahi ya vuguvugu lao la kisiasa na kuwekana vizuri katika masuala kadhaa ambayo hakuyafafanua.


Mutua alisema kuachana na mpango wa kugawa nchi kwa pembe ni sehemu ya maazimio ya mkutano huo, uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwemo kiongozi wa Narc, Martha Karua na Gavana wa Kitui, Charity Ngilu ambaye naye anatokea Narc.


Wengine ni Alfred Mutua wa MCC na Kivutha Kibwana (Muungano), vilevile vyama vingine vyote vilituma wawakilishi walioshiriki kutengeneza maazimio ya pamoja.


“Hakutakuwa na pembe ambayo chama fulani kitakabidhiwa. Mazungumzo yamekuwa shirikishi, yaliyozingatia usawa na mashauriano. Kila kilichozungumzwa na kujadiliwa kililenga kutoa mwongozo wenye kuimarisha umoja wetu kuelekea uchaguzi wa Agosti,” alisema Mutua.


Kuhusu suala la mgombea mwenza, Mutua alisema iliamuliwa kwenye mkutano kwamba atapatikana baada ya kufanya mashauriano na vyama vyote washirika kwenye Azimio la Umoja na OKA katika wakati mwafaka.


“Kulikuwa na azimio pia la kutanua Baraza la Umoja, ambacho ni chombo kikuu cha uamuzi cha Azimio hadi kufikia wajumbe 11 na kwamba idara za Azimio la Umoja hazitashirikisha kambi za vyama wala ushirika wa vyama,” alisema Mutua.


Akifafanua zaidi, Mutua alisema, “Vyama vidogo kwenye ushirika wetu wa Azimio la Umoja, waliibua hoja na tulitakiwa kuwapa uhakika kuwa hakutakuwa tena na mgawanyo wa pembe. Mahali ambapo Azimio la Umoja kutakuwa na mgombea zaidi ya mmoja, tutafanya majadiliano na kumpitisha yule ambaye atakuwa imara zaidi, halafu wagombea wa vyama vingine watajitoa. Tutaacha watu wagombee zaidi ya mmoja kwenye baadhi ya maeneo ambayo tutakosa mwafaka”.


Mutua aliweka wazi kwamba wazo la awali la kugawa nchi kwa pembe na kila chama kupewa pembe yake ili kisimamishe wagombea, lengo lake lilikuwa kuzuia kuwa na mgombea zaidi ya mmoja kwenye eneo moja ndani ya vyama vya Azimio la Umoja na OKA.


“Kusimamisha wagombea wawili au zaidi kutoka Azimio la Umoja na OKA, kutafungua milango kwa United Democratic Alliance (UDA), hususan Nairobi na miji mingine yenye mchanganyiko wa watu,” alisema Mutua na kueleza kuwa umoja wao upo makini na hautaruhusu UDA wapate ushindi kwa urahisi kwa sababu ya Azimio kushindwa kujipanga.


UDA ni chama kipya ambacho kimejipatia umaarufu haraka Kenya. Kiongozi wake ni Naibu Rais, William Ruto ambaye ndiye mshindani mkuu wa Raila katika Uchagzi Mkuu utakaofanyika Agosti 9, mwaka huu.


Sera ya kugawa nchi kwa pembe utekelezaji wake ulilenga eneo la Mlima Kenya waachiwe Jubilee kwa sababu ndiyo ngome yao. Maana yake, Jubilee wangemuumiza kiongozi wa Nark Kenya, Martha Karua, vilevile Gavana wa Meru, Kiraitu Murungi wa Chama Devolution Empowerment (DEP), ambao nao ni watu wa Mlima Kenya.


Mashariki chini, ambako Kalonzo ndiyo ngome yake, kama Wiper wataachiwa pembe hiyo maana yake Gavana Ngilu, Kibwana, Mutua na Mnadhimu wa zamani wa Ikulu, Nzioka Waita wa Chama cha Uzalendo wangeathirika.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.