Moshi. Baraza la Madiwani Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro limemuondoa madarakani Meya wa Manispaa hiyo, Juma Raibu kutokana na tuhuma mbalimbali zinazomkabili ikiwamo matumizi mabaya ya madaraka.
Raibu ameondolewa madarakani leo Jumatatu Aprili 11, 2022 baada ya kupigwa kura za siri katika baraza maalumu la madiwani ambapo kura za kumkataa zilikuwa 18 huku za kumkubali zikiwa 10.
Akisoma taarifa ya timu ya uchunguzi ya Mkoa, Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Rashidi Gembe amesema Raibu anakabiliwa na tuhuma mbalimbali ikiwamo kutumia nafasi yake vibaya, kupokea rushwa na kuruhusu ujenzi holela katika eneo la CBD, mienendo mibaya na ukosefu wa adabu dhidi ya madiwani wenzake.
Raibu pia anatuhumiwa kutoa maneno ya kuwatambia madiwani wenzake kuwa yeye ni mteule wa kamati kuu ya CCM Taifa na si ngazi ya wilaya wala mkoa, kuchelewa vikao na kutokaimisha vikao kwa naibu meye hata akiwa nje ya ofisi na vikao vingine kulazimisha kuahirishwa kwa kuwa yeye hayupo na kwamba timu hiyo pia imebaini mwenendo mbaya wa Meya huyo.
"Timu ya uchunguzi ilitekeleza majukumu yake kwa kuzingatia hadidu za rejea kuchunguza na kubaini kama mstahiki meya anatumia nafasi yake vibaya, kushiriki vitendo vya rushwa katika ujenzi holela katika eneo la CBD, kuchunguza mienendo mibaya na ukosefu wa adabu dhidi ya madiwani anaowaongoza, kuchunguza mienendo na tabia ya meya katika jamii kwa kuhusisha na nafasi na wadhifa wake".
Ameongeza kuwa "Pia timu ilichunguza kama Meya anajihusisha na tuhuma zilizotolewa na wananchi na baadhi ya vyombo vya habari kuwa alihudhuria na kushiriki sherehe za kuzaliwa za kijana anayedaiwa kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja (ushoga) na kuona jinsi tukio hilo linavyoathiri utendaji wake wa kazi na kwamba timu ilitumia njia mbalimbali ili kubaini tuhuma hizo kama zinathibitika au la".
Akisoma matokeo ya kura Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Rashid Gembe amesema kwa mamlaka aliyopewa ya kuongoza kura za siri zilizopigwa na madiwani jumla ya kura 28 zilipigwa na kwamba hakuna iliyoharibika.
"Kwa mujibu wa idadi ya wajumbe waliopo na kwa matokeo hayo wajumbe wameunga mkono azimio la kumuondoa meya madarakani na kwa matokeo haya natangaza rasmi kuwa meya ameondolewa madarakani na kwa mujibu wa kanuni naibu meya ataendelea kushika nafasi hiyo mpaka hapo uchaguzi zitakapofanyika na meya anaruhusiwa kukata rufaa kama hajaridhika"
Baadhi ya madiwani wa Manispaa hiyo wamesema wamefanya maamuzi ya kihistoria ya kumuondoa Meya madarakani kwa sababu ya matendo yake na tuhuma zinazomkabili.
"Leo tumefanya maamuzi ya kihistoria na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, Abdulrahaman Kinana amesema cheo kisikufanye ukajitanua, kisikufanye ukawadharau wengine, ametuelekeza namna viongozi wanapaswa kufanya wanapowaongoza wengine, tunapaswa kusikiliza hotuba ya kinana jana Dar es Salaam," amesema Zubery Abdalla.
Diwani wa Kata ya Mji mpya, Abuu Shayo amesema wameandika historia ya kumuondoa Meya madarakani na kwamba hatua hiyo imefikiwa baada ya kuwa na tuhuma mbalimbali.
Katika kikao hicho cha madiwani, Raibu hakuzungumza chochote na baada ya kikao kusitishwa aliondoka kwa kutumia usafiri wa bodaboda.
CHANZO MWANANCHI
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.