Halmashauri ya Jiji la Ilala imekuwa ya mwisho katika shughuli ya uwekaji wa anuani za makazi katika Mkoa wa Dar es Salaam kwa kufikia asilimia saba hadi sasa huku Kinondoni ikiongoza kwa kuandikisha asilimia 37.
Hayo yamesemwa Jumatatu Aprili 11, 2022 na Mkuu wa Mkoa huo, Amos Makalla kwenye majumuisha ya ziara yake ya kukagua miradi inayotekelezwa na fedha za tozo za miamala ya simu Wilaya ya Kinondoni.
Pamoja na mambo mengine katika majumuisho hayo aligusia kuhusu shughuli ya uwekaji wa anauani za makazi na kueleza kuwa haridhishwi na maendeleo ya shughuli hiyo.
"Siridhishwi namna ya uwekaji anuani za makazi unavyoenda mkoani hapa na sioni sababu ukizingatia ni Jiji linaloongoza kwa mapato, wakati Ilala ina miundombinu mizuri na baadhi ya mitaa tayari ina majina.
"Hamna kisingizio katima hili kwani wenzetu wenye miundombinu mibovu wamewezaje kufanya vizuri halafu sisi tunashindwa,?" amehoji Makalla.
Amesema katika suala hilo atahakikisha anakula sahani moja na wakuu wa wilaya, maofisa tawala na wakurugenzi na kubainisha kuwa hatakuwa tayari kibarua chake kiharibike kwa sababu ya wao kushindwa kuwajibika katika jambo hilo.
Katika uwekaji anuani huo, Kigamboni inashika nafasi ya pili kwa kufikia asilimia 27 ikifuatiwa na Temeke iliyoandikisha kwa asilimia 20.
Kuhusu miradi aliyoikagua Makalla amesema ameridhishwa nayo huku akiahidi kuhakikisha wanasimamia ujenzi huo uendane na thamani ya fedha zilizotolewa.
Katika fedha hizo za tozo, Dar es Salaam imepatiwa Sh6.2 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa shule huku kwa vituo vya afya wakiwa wamepatiwa Sh2.5 bilioni.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.