NAIBU wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja amewaonya askari wa Jeshi la Uhifadhi kujiepjiepusha kushirikiana na wahalifu kuhujumu rasilimali za misitu na wanyamapori.
Alitoa onyo hilo mwishoni mwa wiki wakati wa hitimisho la mafunzo ya miezi sita ya kijeshi kwa askari na maofisa wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) katika Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi, jijini hapa.
“Baadhi yenu sio waaminifu kwani wanashirikiana na wahalifu kwa kuvujisha siri za serikali ili kufanikisha uhalifu wa rasilimali za nchi.”
“Niendelee pia kuwakumbusha kwamba mnaenda kutekeleza majukumu yenu kwa mfumo wa kijeshi, lakini hiyo isiwaondelee utu pamoja na weledi mlionao. Epukeni kutumia nguvu kupita kiasi maana mnaenda kukutana na wananchi wanaoishi kando ya maeneo yaliyohifadhiwa,” alisema.
Wakati huohuo, Masanja aliwataka wananchi kutovamia maeneo yaliyohifadhiwa kwa shughuli zinazoruhusiwa kama vile uvunaji misitu, uchimbaji wa madini na ufugaji nyuki, bali wafuate sheria na kanuni zilizopo.
Alisema watu ambao tayari wamevamia maeneo hayo wanaondoke kwa faida ya kizazi cha sasa na baadae. Kamishna wa Uhifadhi TFS, Dos Santos Silayo alisema wakala hiyo inaeendelea kutoa mafunzo ya utayari kwa waliopo katika ajira, ambapo watumishi takribani 1,958 wamenufaika sawa na asilimia 99 ya watumishi wote na mchakato unaendelea ili kuwafikia wote.
“Mafunzo haya yanalenga kujenga mfumo imara katika sekta ya misitu na rasilimali nyuki na kusaidia kupunguza uhalifu katika maeneo mbalimbali ikiwamo wa misitu.”
“Lakini tumeona pia maeneo ya uhifadhi yakiongezeka na mengine kupandishwa hadhi ili kujenga mfumo thabiti wa usimamizi. Yapo pia masuala ya kuongeza mifumo ya ikolojia hasa upandaji miti nchini na kuongezeka kwa uzalishaji na uendelezaji wa sekta ya nyuki,” alisema.
Kaimu Mkuu wa taasisi hiyo, Jeremia Msigwa alisema wahitimu 43 walifundishwa pamoja na mambo mengine, matumzi ya silaha na kufanya doria, usalama na uraia, utunzaji mazingira, upelelezi na kukabiliana na majanga.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.