ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, December 10, 2021

MRADI WA JNHPP KUTEKELEZWA KWA WELEDI, UFANISI, WAKATI NA GHARAMA ZILIZOPANGWA – WAZIRI MAKAMBA

 

Na Dorina G. Makaya – Rufiji, Pwani.

Waziri wa Nishati Mhe. January Yusuf Makamba amesema Mradi wa Ujenzi wa Bwawa la kuzalisha umeme wa  maji la Julius Nyerere (JNHPP) unatekelezwa kwa weledi, ufanisi, wakati na gharama zilizopangwa

Waziri Makamba ameyasema hayo tarehe 07 Novemba 2021, akiwa kwenye ziara ya kikazi na Waziri wa Nyumba, Huduma na Makazi wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri Mhe. Mhandisi Assem Hafez El Gazar walipotembelea Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (JNHPP)  tarehe 07 Desemba, 2021.


Ameeleza zaidi kuwa, Serikali kupitia Wizara ya nishati inasimamia mradi huo mkubwa wa Ujenzi wa Bwawa la kuzalisha umeme wa maji la Julius (JNHPP) na kuwa mradi huo unagharamiwa kwa fedha za Watanzania shilingi trilioni 6.558 na utazalisha umeme wa Megawatt 2,115.

Waziri Makamba pia amekumbushia kuwa, Ujenzi wa Bwawa la kuzalisha umeme wa  maji la Julius Nyerere (JNHPP),  ni muhimu na ni mradi mkubwa wa kimkakati kwa nchi yetu. “Sisi kama wasimamizi tumepewa jukumu na Rais wetu Mhe Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha kwamba mradi huu unatekelezwa kwa weledi, ufanisi, wakati na gharama zilizopangwa” alisema Waziri Makamba.



Alikumbushia kuwa, wakandarasi wa mradi huu wametoka katika nchi ya Misri na kuwa ziara hiyo ya Waziri wa Nyumba, Huduma na Makazi wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri Mhe. Mhandisii Assem Hafez El Gazar, aliyepewa dhamana ya kusimamia Ujenzi wa Bwawa la kuzalisha umeme wa maji la Julius (JNHPP), inaonyesha namna ambavyo Serikali ya Jamhuri ya Kiarabu ya Misri ilivyochukulia kwa uzito wa hali ya juu katika kuhakikisha kwamba Mradi unatekelezwa kwa weledi, ufanisi, wakati na gharama zilizopangwa


“Tumekuja hapa leo kukagua maendeleo ya mradi, kuangalia tulipofikia, kuangalia kama kuna changamoto kwa upande wa Serikali ya Tanzania na Serikali ya Misri ili tuweze kutatua na kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huu.” Alisema Waziri Makamba.




Waziri January Makamba amesema, baada ya kutembelea mradi, wameona mradi unaendelea vizuri pamoja na changamoto chache zilizopo za Mradi kutokwenda kwa kasi kama iliyokuwa imepangwa. Lakini, alieleza kuwa si jambo la ajabu kutokea kwa miradi mikubwa kama huo kuchelewa kukamilika.

Amesema, jambo jema ni kuwa, mradi uko katika hatua nzuri ya utekelezaji na iwapo italazimu kuongeza muda basi utakuwa ni muda unaokubalika na hakutakuwa na gharama za ziada.

“Sisi tumepewa kazi ya kuhakikisha kwamba mradi unatekelezwa na kukamilika kwa kuzingatia usalama na ubora na kutuhakikishia upatikanaji wa umeme wa uhakika. alisisitiza Waziri Makamba.

Waziri Makamba ameeleza zaidi kuwa, Wizara ya Nishati ingependa pakiwa na changamoto zo zote basi zijadiliwe kidugu kwa kuzingatia matarajio ya viongozi wakuu. wa nchi zote mbili pasipo kuviziana, kushtakiana na kuingiza madai ya kisheria na kuwa  nia iwe kumaliza tofauti ndogo ndogo zozote zilizopo kwa maelewano.

Nae Waziri wa Nyumba, Huduma na Makazi wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Mhe. Mhandisi Assem Hafez El Gazar amesema, Mradi wa JNHPP ni muhimu sana kwa nchi zote mbili za Tanzania na Jamhuri ya Kiarabu ya Misri.


Amebainisha kuwa, wakati alipoteuliwa kushika nafasi hiyo ya Uwaziri wa Nyumba, Huduma na Makazi wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, maelekezo ya kwanza aliyopewa na Raisi Al Sisi ni kusimamia utekelezaji wa Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (JNHPP)

Waziri El Gazar ameuelezea Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (JNHPP) kuwa ni mradi utakaosaidia kuimarisha mahusiano baina ya nchi hizo mbili na kuwa, ukitekelezwa vizuri utajenga imani kwa watanzania kuwa. Jamhuri ya Kiarabu ya Misri ni nchi yenye uwezo wa kutekeleza miradi mingine mikubwa ambayo Tanzania itatazamia kuijenga baadaye.

Aidha, Waziri huyo wa Nyumba, Huduma na Makazi wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri Mhe. Mhandisi Assem Hafez El Gazar, amewataka wakandarasi wajitahidi kukamilisha mradi huo kwa wakati na ubora unaokubalika. 


Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.